Loading...

Dawa za ARV zabainika kujenga usugu.


Dar es Salaam. Tumaini kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) sasa linayeyuka mithili ya barafu kwenye moto baada ya dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo (ARV) kubainika kuwa zinajenga usugu.



Ripoti mpya iliyotolewa jana na jarida la kisayansi la Lancet, imeeleza kuwa usugu wa dawa hizo utasababisha matibabu kwa watu wanaoishi na VVU duniani kuwa magumu.

“Kutokana na hali hiyo, matibabu na usimamizi kwa watu wanaoishi na VVU ni lazima yaboreshwe na wagonjwa wafuatiliwe,” inasema ripoti hiyo.

Kisayansi, dawa za ARV zinapojenga usugu maana yake ni kuwa hazitaweza tena kupambana na VVU hivyo mgonjwa kuendelea kupata magonjwa nyemelezi.

Kadhalika ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa dawa za ARV ambazo zimejenga usugu ni pamoja na Tenovofir efavirenz na lamivudine.

“Kama dawa zinajenga usugu, basi hiyo ni hasara kubwa,” mwandishi wa utafiti huo, Dk Robert Shafer amesema.

Ripoti hiyo inasema watu wenye VVU hujenga usugu wa dawa aina ya Tenovofir kwa namna mbili, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kutotimiza masharti ya dawa na hivyo virusi kuzaliana au pengine wamepata maambukizi kwa mtu ambaye tayari ana virusi vilivyojenga usugu.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangala alisema kama kweli dawa hizo zimekuwa sugu, basi lazima mabadiliko ya sera za matibabu yabadilike na mfumo wa usimamiaji wa matibabu ya ARV pia ubadilike.

“Nitakuwa kama mbumbumbu kama nitakuambia chochote sasa. Hizo taarifa ni nzito na zinaweza kubadili chochote katika matibabu kama ni kweli,” alisema Dk Kigwangalla ambaye aliahidi kuzungumzia suala kwa kina atakapojiridhisha kuhusu suala hilo.

Watafiti wa Lancet wanasema walitumia taarifa kutoka kwenye sampuli ya watu 1926 wenye VVU kutoka nchi 36 ambao wanatumia ARV.

Utafiti huo ulibaini kuwa tenovofir ilijenga usugu kwa asilimia 20 ya wenye VVU barani Ulaya na zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa hao kutoka kusini mwa jangwa la Sahara.

Chanzo cha Tenovofir kujenga usugu kunatajwa na watafiti hao kuwa ni pamoja na kuanza dawa wakati kinga ya mwili (CD4) ipo chini na matumizi ya dawa muambata za ARV.




ZeroDegree.
Dawa za ARV zabainika kujenga usugu. Dawa za ARV zabainika kujenga usugu. Reviewed by Zero Degree on 1/31/2016 03:45:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.