Loading...

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aongoza ubomoaji wa uzio wa Hoteli ya Golden Tulip.


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akiwa na watendaji wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakisimamia ubomoaji wa uzio wa Hoteli ya Golden Tulip jana. 

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi jana aliongoza watendaji wa Manispaa ya Kinondoni kubomoa uzio wa Hoteli ya Golden Tulip na kuonya matajiri kuwa fedha zao haziwezi kununua kila kitu.

Uzio huo wa kiwanja namba 2048 cha hoteli hiyo, kilikuwa kimezungushiwa mabati kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Lakini jana, watendaji wa manispaa hiyo walifika eneo hilo saa 3:45 asubuhi na kukuta wafanyakazi wa idara ya ujenzi wa kampuni ya Indian Ocean Hotel Ltd, inayomiliki hoteli hiyo, wakiwa wameanza kazi ya kubomoa uzio huo.

Pamoja na hoteli hiyo kuanza ubomoaji, tingatinga la Manispaa ya Kinondoni liliingia kwenye kazi ya kubomoa uzio na kusababisha wafanyakazi wa kampuni hiyo kuacha kazi hiyo.

Akizungumza kwenye eneo la tukio, Lukuvi alisema kuna matajiri ambao wanadhani kwamba fedha zao zinaweza kumnunua kila mtu, jambo ambalo alisema si kweli.

“Kulikuwa na mkutano wa (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) Sadc, hoteli ya Golden Tulip waliomba eneo la kiwanja hiki walitumie kuegesha magari wakati wa mkutano ule na walikubaliwa na Serikali,” alisema.

Alisema baada ya Serikali kuwapa eneo kwa ajili ya maegesho, wakaona waanze harakati za kulimiliki moja kwa moja eneo hilo.

Lukuvi alisema kampuni ya Indian Ocean Hotel Ltd ilipewa hati ya kiwanja namba 2048 kiujanja ujanja na watendaji wa wizara wasio waaminifu.

Alisema mwaka 2015 manispaa ya Kinondoni ilitoa kibali cha ujenzi kwenye kiwanja hicho, lakini baadaye walikifuta.

Baada ya kukifuta, uongozi wa kampuni hiyo ulikwenda Mahakamani ya Ardhi kupinga kufutiwa kibali, lakini juzi mahakama hiyo imetupilia mbali ombi lao.

“Ndiyo maana leo tumeamua kubomoa ili kutoa somo kwa wengine kuwa kuna umuhimu wa kufuata sheria. Hata Rais John Magufuli alikuwa akisikitishwa na ujenzi huu, lakini leo atafurahi na nina uhakika atafuta hati ya kiwanja hiki,” alisema.

Waziri aliutaka uongozi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) na Wizara ya Ardhi kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa waliohusika katika utoaji wa vibali vya kiwanja hicho.

Pia, aliitaka Takukuru kushirikiana na wizara hiyo ili kuwashtaki maofisa wote walioshiriki katika utoaji wa vibali vya kiwanja hicho.

Lukuvi alisema wanataka eneo hilo liwe wazi kwa ajili ya wananchi kwenda kupumzika na kwamba wakipewa wawekezaji watatoza viingilio.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema kampuni hiyo iliomba kumilikishwa eneo hilo, lakini ikakataliwa na kupewa notisi ya kuvunja uzio huo Oktoba, 2015.

“Licha ya manispaa kukataa kusaini fomu za kuombea hati, walituzunguka na kwenda wizarani wakapewa hati,” alisema. Kwa upande wake, Vedasto Makota ambaye ni mkurugenzi wa habari, mawasiliano na uenezi wa Nemc, alisema eneo hilo linatakiwa kuwa wazi kwa ajili ya mpango mpya wa kuendeleza ufukwe wa Bahari ya Hindi kutoka mnara wa kuongozea meli Oystebar hadi Hoteli ya Seacliff eneo la Masaki.



ZeroDegree.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aongoza ubomoaji wa uzio wa Hoteli ya Golden Tulip. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aongoza ubomoaji wa uzio wa Hoteli ya Golden Tulip. Reviewed by Zero Degree on 1/31/2016 03:49:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.