Morogoro: Mvua iliyoambatana na upepo mkali yaezua nyumba za kaya 360 na kuwaacha wakazi 1600 bila makazi.
Dk Haji Mponda.
Malinyi. Wakazi zaidi ya 1,600 wa kaya zaidi ya 360 za vijiji mbalimbali wilayani hapa, Mkoa wa Morogoro, wamekosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo jana.
Mvua hiyo imesababisha familia hizo kukosa mahali pa kuishi, huku wengi wa waathirika wakipewa hifadhi kwenye majengo ya umma ikiwamo shule, bohari na wengine kwa majirani.
Wakizungumza na gazeti hili, wananchi hao walisema kuanzia Januari 28, mwaka huu mvua kubwa iliyoambatana na upepo ilinyesha na kusababisha madhara mbalimbali.
Mmoja wa waathirika hao, Jackson Msambila alisema kutokana na madhara ya mvua hizo, barabara ziliharibika na kusababisha mawasiliano kuathirika.
Kadhalika, waathirika hao waliiomba Serikali na wahisani kuwapa misaada mbalimbali, ikiwamo ya ujenzi na uezekaji wa nyumba, chakula, magodoro, madaftari na vifaa vya shule kwa ajili ya watoto ambavyo vingi vimesombwa na maji.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Said Msomoka na Mbunge wa jimbo hilo, Dk Haji Mponda kwa nyakati tofauti walitembelea maeneo yaliyokumbwa na maafa na kushuhudia uharibifu huo.
Msomoka alisema wengi wa walioathirika wamehifadhiwa katika Shule ya Sekondari Itete ambayo nayo jengo la darasa na maabara yamebomolewa na mvua. Dk Mponda alisema Serikali inaendelea na tathmini kujua athari zilizosababishwa na mvua hizo na kuangalia namna itakavyowasaidia kupitia kamati ya maafa.
ZeroDegree.
Morogoro: Mvua iliyoambatana na upepo mkali yaezua nyumba za kaya 360 na kuwaacha wakazi 1600 bila makazi.
Reviewed by Zero Degree
on
1/31/2016 03:55:00 PM
Rating: