Loading...

Iringa wapigwa marufuku kuuza mbao.


Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela

Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ameipiga marufuku Idara ya Maliasili na Misitu kuuza mbao na rasilimali zitokanazo na misitu zinazokamatwa.

Sambamba na agizo hilo, Kasesela amedai kuanzia sasa mbao zitakazokamatwa zitatumika kutengenezea madawati ambayo yatapelekwa katika shule mbalimbali wilayani humo.

Pia, ameiagiza idara hiyo kuwakamata watu wanaojihusisha na uvunaji wa misitu bila vibali na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua.

Kasesela alitoa kauli hiyo juzi, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Igingilanyi kilichopo katika Tarafa ya Isimani pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa katika siku ya upandaji miti ambayo kiwilaya ilifanyika kijijini hapo.

“Kuanzia leo katibu tawala waandikie barua, zile mbao zilizokamatwa hakuna kuuza kwa sababu nimegundua wanazikamata wanauza, kwa hiyo wanawapa fursa wahusika kuendelea kupasua miti yetu na kutusababishia jangwa,” alisema.

Kuhusu vibali vya kuvuna misitu, mkuu huyo wa wilaya alisema anajua vimekuwa vikisuasua kutolewa na kuwataka wahusika kufuata utaratibu wa upatikanaji wake ili waweze kuvipata.

Alisema wilaya hiyo imetenga maeneo makubwa ya kuhifadhi misitu na mazingira kwa ajili ya kuongeza kiwango cha maji katika tarafa za Mlolo, Ismani, Kalenga, Pawaga na Idodi na kwamba, miti iliyopandwa inapaswa kulindwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Diamond Trust ambaye benki yake ilifadhili kazi ya upandaji wa miti hiyo, Meneja wa benki hiyo tawi la Iringa, Beda Magwira alisema kupanda miti na kutunza mazingira ni moja ya nguzo kuu ya shughuli zao katika maeneo wanayofanyia biashara.

Alisema benki hiyo imeitikia wito wa mkuu huyo wa wilaya kwa kuunga mkono programu ya upandaji miti kwa mchango wa Sh5 milioni ambazo zimetumika kuwezesha kazi ya upandaji wa miche 500 katika kijiji hicho.

Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa halmashauri hiyo, Dornald Mshana alisema miti 3,458,541 imepandwa katika maeneo mbalimbali wilayani humo kwa kushirikiana na watu binafsi pamoja na taasisi binafsi. “Leo tumefanikiwa kupanda miche 500 ya aina ya mijohoro na ni maalumu kwa ajili ya kuhimili ukame, tunaamini itasaidia kubadili mazingira yetu,” alisema Mshana.



ZeroDegree.
Iringa wapigwa marufuku kuuza mbao. Iringa wapigwa marufuku kuuza mbao. Reviewed by Zero Degree on 1/21/2016 02:41:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.