Loading...

Jiji lawatimua WALIOGEUZA MAKAZI Kituo cha Mabasi Ubungo.


Baadhi ya watu waliokuwa wakiishi katika Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT), Dar es Salaam wakitoka katika ofisi za gazeti la Mwananchi jana kulalamikia kitendo cha mgambo wa jiji kuwatimua mwishoni mwa wiki iliyopita . Picha na Anthony Siame.

Dar es Salaam. Baadhi ya watu waliokuwa wakiishi katika Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT) wamedai kuporwa mali zao na kudhalilishwa na mgambo wa jiji la Dar es Salaam, wakati wakiwatimua mwishoni mwa wiki.

Madai hayo waliyatoa jana katika ofisi za gazeti hili zilizopo barabara ya Mandela Tabata jijini hapa.

Kuanzia Alhamisi iliyopita, gazeti hili limekuwa likiripoti habari za kuwapo kwa watu wanaoishi kituoni hapo kwa miaka kadhaa wakijifanya kuwa ni wasafiri bila ya uongozi kuchukua hatua.

Baada ya habari hizo, mgambo hao waliendesha operesheni kuwatimua watu hao kituoni hapo.

Hata hivyo, Meneja wa UBT, Juma Iddy alisema hawezi kufahamu kama watu hao walikuwa wakiishi kituoni hapo kwa sababu wamekuwa wakifanya operesheni mara kwa mara ya kuwatimua.

“Operesheni hapa ni endelevu kwa sababu kila siku watu wanaingia na kutoka, miundombinu ya kituo chetu ni vigumu kuwadhibiti wasiingie, hivyo mara kwa mara tunawaondoa na wengine kuwafikisha polisi,” alisema.

Wakizungumza jana, watu hao walisema wanatoka mikoa mbalimbali nchini na kwamba walifika jijini Dar es Salaam kupatiwa matibabu, kufuatilia mirathi, mafao ya uzeeni huku mmoja akidai kutelekezwa na mume wake.

Askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Hamisi Mohamed (101) mkazi wa Ngara, mkoani Kagera, alisema yupo Dar es Salaam kupatiwa matibabu ya mguu katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, lakini hana ndugu jijini hapa, hivyo amelazimika kuishi kituoni hapo.

“Nilikuwa mmoja wa wapiganaji wa vita ya Tanzania na Uganda, nikapigwa risasi ya mguu, nilifanyiwa upasuaji na kuondolewa risasi, lakini kikabaki kipande ndicho ambacho kinanisumbua hadi sasa,” alisema.

Alisema wakati anasubiri kufanyiwa upasuaji hawezi kulazwa kwenye wodi za hospitali hiyo, hivyo amelazimika mwezi mzima kulala katika kituo hicho.

“Juzi usiku walikuja mgambo wamenipiga, wakanimwagia maji na kuchukua simu zangu mbili na kutufukuza na watu wengine,” alilalamika na kusisitiza kuwa yeye na wenzake leo watakwenda kutoa taarifa za upotevu wa mali zao Kituo cha Polisi cha Urafiki.

Kwa upande wake, mmoja wa wafanyakazi wastaafu wa Jiji la Dar es Salaam, mkazi wa Kihesa mkoani Iringa, ambaye aliomba asitajwe jina lake, alisema anafuatilia mafao yake, lakini kwa sababu hana ndugu, amekuwa akiishi katika kituo hicho.

Alisema katika oparesheni ya kuwafukuza, begi la nguo lilipotea katika mazingira ya kutatanisha na anahisi mgambo walilichukua.

Kwa upande wake, Catherine Raphael kutoka mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, alisema yuko Dar es Salaam kushughulikia mirathi ya marehemu mumewe Mahakama Kuu.

Agnes Daniel (20), mkazi wa Singida akiwa amembeba mwanae wa mwaka mmoja, alidai alitelekezwa na mumewe na kuamua kuishi kituoni hapo. Alisema alipoteza begi lenye nguo na Sh30,000 za nauli ya kurudi kwao Singida.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Jiji lawatimua WALIOGEUZA MAKAZI Kituo cha Mabasi Ubungo. Jiji lawatimua WALIOGEUZA MAKAZI Kituo cha Mabasi Ubungo. Reviewed by Zero Degree on 1/11/2016 01:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.