Loading...

Askofu ATIMULIWA kwa UBADHILIFU wa milioni 500.


Mwenyekiti wa nyumba ya wahudumu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza, Mchungaji Andrew Kashilimu, akisoma tamko la wachungaji jana.


Mwanza. Wachungaji wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) wametangaza kumfukuza kazi Askofu wa Dayosisi hiyo, Boniface Kwangu kwa madai ya kuhusika na ubadhilifu wa Sh500 milioni.

Hii si mara ya kwanza kwa wachungaji wa kanisa hilo kumkataa Askofu Kwangu, baada ya mpango kama huo kushindikana Septemba 2012 walipomtaka ajiuzulu kwa sababu mbalimbali.

Akisoma tamko la kumfukuza kazi askofu huyo jana mbele ya waumini wa kanisa hilo, Mwenyekiti wa wahudumu wa kanisa, Mchungaji Andrew Kashilimu alidai askofu huyo amekikuka viapo vyake, Katiba ya Jimbo hilo, Katiba ya DVN, utumiaji mbaya wa madaraka, mali na fedha za kanisa, kanuni na maadili ya kanisa hilo.

Mchungaji Kashilimu alidai baada ya kikao cha wachungaji kilichofanyika Septemba mwaka jana kilithibitisha kwamba askofu huyo hafuati kanuni na taratibu za kanisa Anglikana Tanzania na amekuwa akiendeleza matabaka ndani ya wahudumu na waumini na utoaji ajira ndani ya DVN kinyume na taratibu za kanisa.

“Baada ya kuchanganua mambo yote kwa ujumla, kikao kikaridhia Askofu Boniface Kwangu ajiuzulu kwa ajili ya afya ya Kanisa la Mungu. Taarifa zilifika Jimbo Kuu Anglikana Tanzania na Jimbo kupendekeza iundwe Tume ya kushughulikia mgogoro wa DVN,” alisema Mchungaji Kashilimu na kuongeza:

“Baada ya kuundwa kwa tume hiyo, taarifa ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya shule ya Isamilo ambayo inamilikiwa na kanisa ilibainisha kwamba kulikuwa na upotevu wa zaidi ya Sh500 milioni. Katika hili Askofu Kwangu alihusika na ufisadi huo.”

Kashilimu alidai askofu huyo aligundulika kufungua akaunti binafsi katika benki ya Mkombozi anayotumia kujipatia fedha kutoka kwa wahisani kwa kutumia jina la dayosisi hiyo.

“Mbali na yote alichukua dola 3,000 ambazo ni sawa na Sh6,000,000 kutoka kwa mhasibu wa shule ya Isamilo kwa ahadi ya kuzirejesha, baada ya kudaiwa aliamua kumfukuza kazi na mpaka sasa hajazirejesha. Kipindi cha mwaka 2008/2012 alichukua tena Sh15,364,560 kutoka kwa mhasibu huyo nazo hajazirejesha,” alidai.

Kashilimu alidai kutokana na tuhuma hizo Askofu huyo amesababishia dayosisi hiyo kudaiwa na waajiriwa waliofukuzwa na kusimamishwa kazi kinyume na utaratibu wa utumishi wa umma, hivyo kanisa hilo lina deni la zaidi ya Sh60 milioni na kwamba ameuza gari la dayosisi hiyo.

“Kutokana na mambo yote aliyoyafanya Askofu, kanisa limekosa imani naye na limeridhia kwa kauli moja afukuzwe kazi, kwani amefanya ubadhirifu mkubwa kwa kanisa na kwamba kwa kipindi cha miaka saba aliyokuwa askofu hakuna taarifa ya mapato na matumizi aliyoitoa.

Katika hatua nyingine Kashilimu alisema wametoa taarifa dhidi ya askofu huyo katika Kituo cha Polisi Mkoa wa Mwanza na kupewa RB namba MW/RB/265/2016.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mwanza, Justus Kamugisha alipoulizwa alisema hajapata taarifa hizo na kuahidi kufuatilia tuhuma hizo kwa kuwa zinahitaji uchunguzi ili kutolea ufafanuzi.

Juhudi za kumpata askofu aliyeelezwa kuwa yuko nchini Marekani kwa miezi mitano sasa ili azungumzie tuhuma hizo zilishindikana na hata alipoandikwa ujumbe kwa baruapepe gazeti halikupata majibu hadi linakwenda mitamboni. Pia juhudi cha kuwapata Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jacob Chimeledya na Katibu mkuu wa kanisa hilo, Johnson Ching’ole hazikuzaa matunda baada ya simu zao za kiganjani kutopatikana.



Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Askofu ATIMULIWA kwa UBADHILIFU wa milioni 500. Askofu ATIMULIWA kwa UBADHILIFU wa milioni 500. Reviewed by Zero Degree on 1/11/2016 01:00:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.