Loading...

Ukizifuata HATUA HIZI HUWEZI kubomolewa nyumba yako.


Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wakazi wa mabondeni wakisaka hifadhi baada ya nyumba zao kubomolewa, wataalamu wa ardhi na maendeleo ya makazi wametoa njia za kumaliza adha hiyo zikiwamo Serikali kurahisisha mfumo wa urasimishaji ardhi na wananchi kufuata taratibu stahiki za ujenzi ili nyumba zao zisibomolewe.

Wataalamu hayo walisema kwa nyakati tofauti kuwa tatizo kubwa lililosababisha dhahama hiyo ni ukosefu wa elimu ya ardhi na mipango miji miongoni mwa wananchi na Serikali kulegalega katika kusimamia mambo hayo.

Mkurugenzi wa kampuni ya maendeleo ya makazi ya Space and Development, Renny Chiwa alisema uelewa mdogo katika matumizi ya ardhi na mipango miji umewafanya Watanzania wengi kujenga kiholela katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya wazi na mabondeni.

“Kwa sasa mtu akiona ardhi tu anataka kujisitiri bila kuulizia na kufuata taratibu. Serikali na wadau wanatakiwa kutoa elimu ya kutosha juu ya umiliki wa ardhi na matumizi yake,” alisema.

Chiwa aliwataka wataalamu wa wizara ya ardhi washirikiane na taasisi zinazotoa huduma muhimu kwa jamii kama Shirika la Umeme (Tanesco) na Kampuni ya huduma ya Majisafi (Dawasco) katika kudhibiti uendelezaji wa maeneo hatarishi na wazi.

Alisema Tanesco na Dawasco wamechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia watu kujenga katika maeneo yasiyotakiwa kwa kuwa waliunganisha huduma kwa wakazi hao wakati wakijua bayana hapafai.

“Yale maeneo ya mabondeni yote yalikuwa na umeme na maji ya Dawasco. Wao wanawaza kuongeza wateja na fedha tu lakini kwa nchi kama Kenya taasisi hizo zinashirikiana na wataalamu wa ardhi kuzuia uendelezaji huo holela,” alisema.

Njia nyingine ya kukomesha ujenzi holela, Chiwa alitaja kuwa ni Serikali kuyabaini maeneo yote ya wazi, kuyawekea alama na kuyaendeleza ili yasivutie watu kuyavamia.

Alisema Serikali inaweza kutafuta wawekezaji wa sekta binafsi ambao wataendeleza kwa kutoa huduma za burudani katika maeneo hayo ya wazi kuliko kuyaacha bila kuyaendeleza.

Ili kumaliza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa, Chiwa alishauri kuchochea ukuaji wa sekta binafsi katika uendelezaji wa ardhi na makazi kwa kuwa Serikali ina watumishi wachache ambao hawawezi kumudu mahitaji ya sasa ya upimaji na uendelezaji ardhi.

Chiwa alipendekeza ramani za mipango miji zipelekwe ngazi za kata badala ya kukaa wizarani na watumishi wa kada za chini za ardhi wenye elimu ya vyeti na stashahada wapelekwe kila kata kutoa huduma hizo kwa ushirikiano na viongozi wa Serikali za mitaa.

“Hii itafanya watu wengi wapime ardhi zao kwa hiari kwa kuwa hakuna urasimu na hatimaye wataacha kuvamia ardhi na tabia ya kujenga kiholela bila kufuata mipango miji,” alisema Chiwa.

Ofisa Mipango Miji wa Manispaa ya Ilala, Alfred Mbyopyo alisema wananchi wanaweza kuepuka kujenga kiholela kwa kununua viwanja vilivyopimwa au kurasimisha maeneo yao waliyoyanunua kienyeji.

Alisema kwa wale walionunua viwanja vya halmashauri za wilaya vikiwa vimepimwa na kupatiwa hati wanatakiwa kuandaa michoro yao kupitia kwa msanifu majengo yoyote na kuipeleka halmashauri kupata vibali vya kujenga ili kuepusha matatizo.

Mbyopyo alisema kwa wale wanaonunua mashamba au maeneo kienyeji wanaweza kurasimisha na kupata hati za umiliki sawa na walionunua viwanja vikiwa vimepimwa wakianzia na ngazi za Serikali za Mitaa.

“Ukishauziwa eneo lako kama ni miguu 20 kwa 20 kama ambavyo wengi hupima unatakiwa uwatafute maofisa ardhi wa halmashauri au wataalamu binafsi kupima. Ningeshauri wafanye upimaji kwa makundi ili kuokoa gharama,” alisema.

Kwa wapimaji binafsi alisema, watapata vibali vya kupima eneo husika kutoka kwa halmashauri ya Manispaa kuruhusu upimaji wa maeneo husika.

Baada ya kupimiwa na kupata vipimo vya ardhi zao na kubainishiwa havina matatizo yoyote, wanapaswa waende halmashauri husika kwa ajili ya kuhakikisha michoro ya eneo na matumizi yake.

Alisema wapimaji hao watachukua nyaraka hizo na kwenda nazo Wizara ya Ardhi na kupatiwa namba ya kiwanja kupitia idara ya upimaji.

Baada ya kupatiwa namba mwombaji au mtaalamu wake watarudi halmshauri kwa ajili ya kibali cha umiliki baada ya ofisa ardhi na mipangomiji kujiridhisha na mpango wa hati utaandaliwa tayari kupelekwa kwa Kamishna wa Ardhi wa Kanda kwa ajili ya usajili na hati ambayo hutolewa na msajili wa ardhi.

Mbyopyo alisema suala la hati halihusishi kundi kwa waliopima kwa pamoja, bali ni la mtu binafsi kwa kuwa kuna gharama zake, hivyo ni bora wataalamu waliohusika kupima wakatumika kufanikisha upatikanaji wa hati hizo.

Kama ilivyo kwa wenye viwanja vilivyopimwa, Mbyopyo alisema wamiliki wa maeneo ya kienyeji yaliyopatiwa hati na Serikali watafuata taratibu za kupeleka michoro na kuruhusisha kujenga.



Lukuvi aja na mkakati mpya

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema jana kuwa wananchi wanapaswa kuthibitisha matumizi ya ardhi husika kabla kununua ili kuzuia hasara.

Alisema kuna baadhi ya maeneo yanaonekana ni mapori ila ni sehemu za wazi au kwa ajili ya huduma hivyo uthibitisho kwa Serikali za Mitaa na Halmashauri ni nguzo ya kuzuia utapeli na kadhia ya kubomolewa.

“Watu wengi wanakurupuka tu kupata viwanja na kujenga. Wengine wanaanza kujenga halafu ndiyo wanaanza kutafuta hati, baadaye wanakuta eneo lile ni la wazi au la huduma za shule na kutakiwa kubomoa,” alisema Lukuvi.

“Hakikisha unapata kibali cha kujenga kwa sababu ukipata kibali unampa kazi mtoa kibali kufuatilia undani wa eneo lako na iwapo akikuruhusu ujenge halafu mambo yabadilike, watalazimika wakulipe fidia.”

Lukuvi alisema ili kurahisisha mchakato wa upimaji ardhi, wizara inazidi kusajili kampuni nyingi binafsi za kupima ardhi kwa kuwa Serikali haina wataalamu wengi wa kupima.

Mbali na kuongeza wapimaji, alisema ataanza kuzidhibiti bei kubwa za uuzaji wa viwanja zinazotumika sasa na halmashauri nchini na kusababisha wananchi wengi kukosa viwanja.

Alisema halmashauri zimegeuza upimaji na uuzaji wa viwanja kama chanzo kikubwa cha mapato huku zikiwanyonya wamiliki wa mashamba ambayo huchukuliwa kwa kuwapa fidia kidogo.

“Nataka baada ya kupima eneo, wanavyoleta michoro ya eneo nataka walete na mapendekezo ya bei zao tuzione na kutoa bei elekezi. “Wananchi wengi wenyeji wameshindwa kununua viwanja kwa sababu ya bei kubwa. Wao hulipwa fedha kidogo za fidia na kuuziwa kwa gharama za mara 500 au 1,000, safari hii hatutakubali,” alisema Lukuvi.

Alisema Serikali imeagiza vifaa vingi vya kupimia ardhi vitakavyowekwa kwenye ofisi tisa za kanda na halmshauri zote zisizokuwa na vifaa zitakuwa zinaenda kuchukua pale kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Katika mipango hiyo mipya, Lukuvi alisema shughuli za uthamini ardhi na majengo, utoaji wa vibali vya mikopo kupitia ardhi, usajili na utoaji wa hati zinafanyika ofisi za kanda na kwamba hakuna haja ya mwananchi kwenda wizarani.

“Kamishna Mkuu wa Ardhi sasa hatatia sahihi mambo yote yafanyike huko. Nataka muda wa chini kupima hadi kuchukua hati uwe mwezi mmoja na kipimo cha juu miezi mitatu. Mwananchi yoyote atakayepata hati baada ya miezi mitatu anijulishe niwashughulikie maofisa wa halmashauri hiyo,” alisema Lukuvi.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Ukizifuata HATUA HIZI HUWEZI kubomolewa nyumba yako. Ukizifuata HATUA HIZI HUWEZI kubomolewa nyumba yako. Reviewed by Zero Degree on 1/11/2016 12:54:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.