Ni busara KUPUNGUZA MAKALI Bomoabomoa.
MAISHA BONDE LA MKWAJUNI: Mkazi wa Bonde la Mkwajuni, Dar es Salaam, Zamoyoni Kadelu akiosha vyombo kwenye dimbwi la maji juzi.
Juzi, Serikali ilitangaza mambo ya kuzingatia katika operesheni ya ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria na taratibu baada ya wananchi kutoa kilio chao kuwa kazi hiyo inawanyima haki zao za msingi licha ya kukiri kukiuka sheria.
Operesheni hiyo ilianza katikati ya mwezi uliopita kwa kuwabomolea nyumba wakazi wa mabondeni, maeneo ya wazi, pembeni mwa fukwe na kwenye kingo za mito, lakini ilifanywa kwa kutumia taarifa zilizowahi kutolewa huko nyuma za kuwataka wananchi kuhama.
Kwa maana hiyo, Serikali haikutoa muda bali ilianza kubomoa nyumba na kusababisha baadhi ya wakazi kukosa mahali pa kwenda na hivyo kulazimika kulala juu ya vifusi na baada ya kilio kikubwa, mawaziri wanaohusika na suala hilo walikutana na kusitisha kwa siku 14 kuwapa nafasi waondoe vifaa vyao na kubomoa nyumba zao wenyewe.
Hata hivyo, imebainika kuwa kumekuwapo na ukiukwaji mkubwa wa taratibu wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo, huku watendaji wa Serikali wakibainika kuidhinisha ujenzi kwenye maeneo hayo na hivyo kuwalazimisha mawaziri watatu kukutana tena na kujadili suala hilo na hivyo kuja na maazimio ambayo yanaweka unafuu kwenye kazi hiyo.
Katika taarifa yake, Serikali ilisema nyumba zitakazobomolewa kwenye awamu hii ni zile zilizo kwenye maeneo hatarishi ya Bonde la Mto Msimbazi, yaani waliojenga ndani kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na kwenye kingo za mto.
Pia, imesema wale watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma, zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo, hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga, lakini itachukua hatua kwa watumishi wa umma waliowamilikisha.
Pia Serikali itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi wa mabondeni na itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaosimamia kazi hiyo kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa na kinyume na misingi ya haki na uwazi.
Serikali pia imeanzisha dawati la malalamiko kwenye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupokea malalamiko au maswali kuhusu operesheni hiyo.
Taarifa hiyo pia inasema nyumba na majengo yaliyokuwapo kabla ya kutungwa kwa sheria zinazotekelezwa katika ubomoaji hazitabomolewa, isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo hatarini.
Serikali imesema kuwa inaweka uratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake ili hatua za utekelezaji wa sheria za nchi zisiwe chanzo cha taharuki katika jamii.
Kwa kuangalia taarifa hiyo, inaonekana dhahiri kuwa Serikali imesikia kilio cha wananchi waishio mabondeni na wengine na sasa inaweka utaratibu ambao utafanya utekelezaji wa sheria zake ufanyike kwa njia ambayo haitawaumiza wananchi na haitakuwa kero kwao.
Tunapenda kuipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kutekeleza operesheni ya ubomoaji kwa kuweka taratibu ambazo zitatakiwa zifuatwe ili kuondoa usumbufu, mateso na kadhia kwa wananchi.
Ni dhahiri kuwa hakuna mtu ambaye anataka wananchi waishi kwenye mabonde ambayo ni hatarishi, wajenge kwenye maeneo ya wazi, au kwenye fukwe na kingo za mito kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa.
Hali kadhalika, hakuna ambaye angependa kuona mwananchi aliyekiuka sheria na taratibu hizo akiondolewa bila ya utaratibu utakaoheshimu utu na maisha yake.
Tunatoa rai kwa wizara husika kuangalia kwa makini zitawezaje kutekeleza operesheni hiyo kwa njia ambayo itawanusuru wananchi wasikumbwe na majanga kama ya mafuriko, lakini pia wasitaabike, kuteseka na hata kuhatarisha maisha yao kwa sababu tu ya kujenga sehemu zisizoruhusiwa.
Source:Mwananchi
Comment & Share this!!
Ni busara KUPUNGUZA MAKALI Bomoabomoa.
Reviewed by Zero Degree
on
1/10/2016 12:02:00 PM
Rating: