Loading...

Katibu mkuu aanza kazi kwa mgomo TRL.


Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Dk Leonard Chamuliho ameingia ofisini kwa mara ya kwanza jana na kukabiliana na mgomo wa wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) wanaoshinikiza kulipwa stahiki zao.

Katika mgomo huo ulioanza chinichini kwa zaidi ya siku mbili, wafanyakazi wa TRL wanadai malimbikizo ya nyongeza ya mshahara kuanzia Julai hadi Novemba, 2014 na fedha za kazi za muda wa ziada ya Novemba mwaka jana.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), Boaz Nyakeke alimwambia Dk Chamuliho kuwa wafanyakazi hao hawaridhishwi na utendaji wa menejimenti hivyo ni bora akauondoa na kuweka mpya ili kuongeza ufanisi.

“Fedha za wafanyakazi haziendi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kama inavyotakiwa. Kuna mwingiliano wa kimasilahi kati ya Kampuni ya Rasilimali za Reli (Rahco) na TRL unaofanya mali kuharibika wakati bado zinahitajika kufanyiwa marekebisho mbalimbali ya reli na vifaa vyetu,” alisema Nyakeke.

Dk Chamuliho alisema kwa kuwa ilikuwa ni siku yake ya kwanza kuingia ofisini na kukutana na madai hayo, ni vyema wampatie muda ili leo akutane na viongozi wa wafanyakazi kutafuta suluhu jambo ambalo wafanyakazi hao walilikubali.

“Japo nimeingia ofisini leo nimeona bora nije nisikilize masuala yenu. Madai mengine hapa ni ya kihistoria na yapo kwenye ripoti za makabidhiano, hivyo tutayafanyia kazi yakiwamo yale yanayotakiwa tufuate sheria,” alisema.

Jana, wafanyakazi wa TRL waliongeza kasi ya mgomo na kuutaka uongozi wa Trawu kumleta Dk Chamuliho katika karakana ya Kapuya Complex kusikiliza madai yao.

Katika kushinikiza madai yao, wafanyakazi hao walilazimisha treni za abiria la Dar es Salaam ‘Treni ya Mwakyembe,’ kusitisha huduma za jioni kwa kuchomoa baadhi ya vifaa vinavyounganisha kichwa na mabehewa baada ya dereva wake kutaka kuanza kazi.

Tukio hilo lililazimu abiria waliokuwa wamepanda saa 3.50 alasiri kushuka na kudai fedha zao huku wakilalamikia usumbufu na kupoteza muda. Utawala uliwarudishia nauli zao.

Awali, Meneja wa Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez alikana kuwapo wa mgomo wala mgogoro wa aina yoyote baina ya menejimenti na wafanyakazi hao akidai kuwa yaliyokuwa yakisemwa ni maneno tu ya viongozi wa Trawu akitumia utoaji wa huduma ya treni ya abiria ya Dar es Salaam iliyofanya kazi asubuhi kama ushahidi wa maelezo yake.


Source: Mwananchi


Comment & Share this!!
Katibu mkuu aanza kazi kwa mgomo TRL. Katibu mkuu aanza kazi kwa mgomo TRL. Reviewed by Zero Degree on 1/05/2016 03:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.