Loading...

Waziri Maghembe awasimamisha kazi maofisa misitu wa mikoa yote.



Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohammed Kilongo na maofisa wa misitu wa mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.

Akizungumza jana na waandishi wa habari wizarani, Profesa Maghembe alisema agizo hilo limetokana na ubadhirifu unaofanywa na maofisa wa ukusanyaji maduhuli ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika mikoa na wilaya kutoyawasilishwa katika mfuko mkuu wa Serikali.

Ameagiza pia maofisa hao wanaokusanya maduhuli hayo katika wilaya, watumie siku 10 kuanzia jana, kuhakikisha maduhuli yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Waziri Maghembe alisema Kilongo ambaye idara yake ndiyo inayotoa vitabu kwa ajili ya kukusanya maduhuli ya Serikali katika mikoa na wilaya zote, amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Katika hatua nyingine, waziri huyo ameuapa uongozi wa TFS siku saba kurudi katika jengo la wizara ‘Mpingo House’ ambalo walihama mwishoni mwa Septemba mwaka jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF, Mafao House lililopo Ilala.

 “Tumejenga jengo hili kama la misitu ndiyo maana linaitwa Mpingo House kwa maana ni jengo la misitu, ninyi wenyewe mmejenga jengo kubwa hili mmemaliza mmehama, naagiza hadi Januari 11 muwe mmesharudi katika jengo hili, ghorofa ya tatu nikija kukagua niwakute, haiwezekani mueleze matatizo yote mliyonayo mhame nyumba ya Serikali mkapange jengo hapo jirani,” alisema.

Katika hatua nyingine ya kuboresha uhifadhi wa misitu nchini, Waziri Maghembe ameiagiza Idara ya Misitu na Nyuki kuhakikisha inajiimarisha katika lengo lake kuu la uhifadhi kwa kushirikiana na wadau wanaohusika kuhakikisha mamlaka iliyolengwa ya uhifadhi misitu inakamilika.

“Tunataka tutoke kwenye wakala wa huduma za misitu twende kwenye mamlaka ya uhifadhi wa misitu ili tuweze kufanya vizuri zaidi kwenye eneo la uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini, katibu mkuu tunaomba pia usaidie kufanikisha hili,” alisema Profesa Maghembe. Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema maagizo yote yaliyotolewa na waziri yatafanyiwa kazi kwa kuwa lengo lake ni kuona dhamira ya msingi ya Serikali ya awamu ya Tano ya kubana matumizi, kuongeza mapato ya Serikali na kuhifadhi maliasili za Taifa ikiwamo misitu inafikiwa.

Mwigulu awasimamisha viongozi wa tumbaku

Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mwigulu Nchemba amewasimamisha viongozi wa vyama vya msingi vya tumbaku mkoani Iringa wanaotuhumiwa kushiriki katika ufisadi wa mkopo wa matrekta tisa kupitia mgongo wa vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku na kujimilikisha wenyewe.

Nchemba alifikia hatua hiyo baada ya wakulima wa tumbaku kulalamikia viongozi wa vyama hivyo na kuwataka wakabidhi ofisi.

Awali, mwanachama wa Chama cha Msingi cha Mfyome, Francis Kilatu alisema Benki ya CRDB inawakata fedha zao huku wamiliki wa matrekta hayo wakiwa ni wengine hivyo alimuomba waziri kulishughulikia mara moja.


Source:Mwananchi

Comment & Share this!!
Waziri Maghembe awasimamisha kazi maofisa misitu wa mikoa yote. Waziri Maghembe awasimamisha kazi maofisa misitu wa mikoa yote. Reviewed by Zero Degree on 1/06/2016 11:48:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.