Kesi ya mbunge wa singida mashariki [ Tundu Lissu ] kupinga ushindi wake, yafutwa.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu (katikati) akitoka Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma baada ya kufutwa kwa kesi ya kupinga ushindi wake. Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Wilaya ya Dodoma Mjini na Wakili mwenzake, Fred Kalonga.
Mbeya\Dodoma. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma jana ilifuta kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu baada ya mdai kuamua kutoendelea nayo.
Mdai huyo ambaye alikuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Jonathan Njau (CCM), aliamua kuondoa kesi hiyo kwa madai kuwa inampotezea muda wa kufanya shughuli nyingine na kumuingiza gharama ambazo alitakiwa kulipa kiasi cha Sh15 milioni.
Mbele ya Jaji Barker Sahel, Wakili wa Njau, Geofrey Wasonga alisema mteja wake ameamua kufuta kesi hiyo ili kumpa nafasi ya kutekeleza majukumu mengine na kumpa uhuru Lissu wa kuwatumikia wapigakura wake.
Akizungumza nje ya mahakama baada ya uamuzi huo, Lissu alisema kesi hiyo ililenga kumfunga ‘speed’ ili asiendelee na shughuli nyingine, lakini alikuwa na uhakika wa kushinda.
Mkoani Mbeya
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imeiondoa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Mbarali kwa maelezo kuwa mwombaji kupitia mawakili wake, hakuwasilisha vielelezo vya msingi katika kesi hiyo.
Aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Mbarali, Liberatus Mwang’ombe (Chadema) alifungua kesi hiyo akiiomba mahakama hiyo kutengua matokeo yaliyompa ushindi Mbunge Haroon Pirmohamed wa CCM kwenye uchaguzi uliofanyika nchini Oktoba 25, mwaka jana.
Jaji wa Mahakama hiyo, Atuganile Ngwala alitoa uamuzi huo jana na kusema mwombaji kupitia kwa mawakili wake, Benjamin Mwakagamba na Adrian Mhina, hakuambatanisha vielelezo muhimu katika kesi hiyo, ikiwamo hati ya fomu ya matokeo ya ubunge ambayo ndiyo msingi wa kesi. Hata hivyo, Mwang’ombe kupitia kwa wakili wake, Mhina alisema hawakuridhishwa na uamuzi uliotolewa mahakamani hapo wa kuiondoa kesi hiyo, hivyo wanakusudia kukataa rufaa.
Source: Mwananchi
Kesi ya mbunge wa singida mashariki [ Tundu Lissu ] kupinga ushindi wake, yafutwa.
Reviewed by Zero Degree
on
1/22/2016 12:13:00 PM
Rating: