Wananchi wa Uganda watarajia amani Uchaguzi Mkuu ujao.
Mgombea Urais nchini Uganda Amama Mbabazi akinadi sera zake.
Kampala. Siku 27 zimebaki kwa raia wa Uganda kuchagua rais na wabunge katika Uchaguzi Mkuu mwezi ujao, watakawaongoza katika kipindi kingine cha miaka mitano.
Cha muhimu raia wa Uganda kuwa wavumilivu wakati wa kipindi hiki kigumu cha uchaguzi na kumchagua mtu ambaye atawasaidia kutatua kero na kuwaletea maendeleo nchini humo.
Ni kipindi cha kuepuka makundi ya vurugu kwani ndiyo mwanzo wa kutoweka kwa amani ya nchi hiyo.
Wagombea wanane wamejitokeza kuwania urais wa Uganda katika uchaguzi huo utakaofanyika Februari 18, mwaka huu.
Miongoni mwao ni Rais Yoweri Kaguta Museveni, ambaye anatetea kiti hicho baada ya kuiongoza Uganda kwa takribani miaka 30.
Akitoa hotuba yake kwa taifa wakati wa Maadhimisho ya Miaka 54 ya Uhuru wa nchi hiyo, Rais Museveni aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali itaendelea kuwalinda na mali zao wakati na baada ya uchaguzi.
Alisisitiza kuwa hakuna mtu ataruhusiwa kuvuruga amani ya nchi hiyo kwa sababu imejengwa kwa misingi imara. Pia, Kiongozi huyo aliwahakikishia waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika (AU) kuwa uchaguzi nchini humo utakuwa huru na haki.
Aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wanaowataka bila ya kuwa na wasiwasi ya kutokea kwa vurugu kama ilivyokuwa kwenye chaguzi nyingine zilizofanyika nchini humo.
Alisema haki itafuatwa na wala hakutakuwa na upendeleo na kwamba matokeo yatakayopatikana yatakubaliwa na kila mtu.
Haki za binadamu
Wiki iliyopita Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) lilisema Serikali ya Uganda inatoa vitisho dhidi ya vyombo vya habari na wanaharakati ikiwa ni juhudi za kuwanyamazisha kabla ya uchaguzi huo kufanyika.
Katika ripoti iliyopewa kichwa cha habari: ‘’Kutotoa Taarifa kwa Wananchi’’, HRW lilisema waandishi wa habari wamesimamishwa kazi kwa shinikizo la Serikali na vituo vya redio vimekuwa vikitishiwa kwa kurusha vipindi na wanachama wa upinzani kama wageni au wachambuzi wanaoelezea maoni yao kukikosoa chama tawala.
Ripoti hiyo yenye kurasa 48 ilisema wakati waandishi wa habari wa magazeti wanaofanya kazi kwa lugha ya Kiingereza wakiwa wana uhuru kidogo, waandishi wa habari wa redio hasa wanaotumia lugha za makabila ambao wasikilizaji wake wengi wako katika maeneo ya vijijini, wamekuwa wakinyanyaswa na kupewa vitisho kutoka serikalini au maofisa wa chama tawala.
Wagombea saba watashindana na Rais Yoweri Museveni ambaye ameitawala Uganda kwa miaka 30 katika uchaguzi na kuna hofu ghasia zinaweza kutawala kampeni kutokana na vitisho hivyo.
Washindani wakuu wa Museveni ni Waziri mkuu wa zamani, Amama Mbabazi na aliyekuwa daktari wa jeshi na Rais, Kizza Besigye.
Mtafiti Mwandamizi kuhusu masuala ya Afrika wa shirika hilo lenye makao yake nchini Marekani, Maria Burnett alisema uchaguzi wa haki unahitaji uwanja sawa ambapo wagombea wote wanaweza kufanya kampeni zao kwa uhuru na wapiga kura wanaweza kufanya maamuzi sahihi.
Burnett anauliza ni vipi Uganda inaweza kufanya uchaguzi wa haki kama vyombo vya habari na mashirika binafsi hayawezi kukikosoa chama tawala au viongozi wa serikali bila ya woga wowote?
Akizungumza na shirika la habari la DW, Sadabu Kaaya, mwandishi wa habari wa gazeti la ‘The Observer’ nchini Uganda ambaye amewahi kupokea vitisho anasema waandishi wa habari wanaoripoti taarifa za wapinzani wamekuwa wakibugudhiwa na kunyanyaswa.
‘’Matukio haya ni vya kweli. Kwa mfano mimi nimepoteza vifaa vyangu vya kazi. Baadhi ya waandishi tunaotumia mitandao ya kijamii tumekuwa tukivamiwa hasa wale tunaoripoti kuhusu mikutano ya wapinzani,’’ alisema Kaaya.
Mwandishi huyo aliendelea kufafanua kwamba, ‘’Jana tu (Januari 10) waandishi wa habari waliokuwa wanaripoti mkutano wa Dk. Kizza Besigye, walivamiwa na polisi wa Moroto na kunyang’anywa kamera zao na kisha kuvunjwa. Vitendo hivi vipo.’’alisema
HRW ilisema Serikali ya Uganda na maofisa wa chama tawala pia wamekuwa wakiyakandamiza mashirika ya haki za binaadamu likiwamo shirika la kutoa elimu kwa wapiga kura, ambalo limetembelewa mara kadhaa na polisi na kuzuiwa kufanya mikutano yake.
Msemaji wa Serikali, Shaban Bantariza alikanusha tuhuma hizo akisema wamekuwa wakifanya chaguzi huru na za haki kwa miaka yote na wataendelea kufanya hivyo. Anasema kama watu hawakupata taarifa sahihi, mawaziri wengi na wabunge wasingepoteza viti vyao katika uchaguzi wa awali wa hivi karibuni katika chama tawala.
Shirika hilo limesema ripoti hiyo imezingatia mahojiano yaliyofanywa kwa zaidi ya waandishi wa habari 170, wanaharakati, wanachama wa vyama vya siasa pamoja na mashuhuda.
Source: Mwananchi
Wananchi wa Uganda watarajia amani Uchaguzi Mkuu ujao.
Reviewed by Zero Degree
on
1/22/2016 12:17:00 PM
Rating: