Maalim Seif na Ukawa wakutana kuijadili Zanzibar
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad
Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amekutana na viongozi Ukawa jijini Dar es Salaam kujadiliana nini cha kufanya baada ya mazungumzo yao na CCM Zanzibar kuonekana kukwama.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu ambaye alikuwa mmoja wa viongozi waliokutana na Maalim Seif, alisema mazungumzo hayo ni ya kupeana mawazo ya hatua gani wachukue kuhusiana na suala la Zanzibar.
“Mgogoro wa Zanzibar ni mkubwa, kwa hiyo tumejadiliana kujua tuendelee wapi katika kutatua mgogoro huo,” alisema Profesa Baregu.
Alisema katika kikao chao hakuna makubaliano rasmi ambayo wamefikia jana lakini taarifa nyingine zilizopatikana baadaye zimesema watakwenda Dodoma kuzungumza na wabunge.
Kikao hicho kilihudhuriwa na mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima.
Dar kupata Meya wa Jiji Jumamosi
Uchaguzi wa kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam unatarajiwa kufanyika Jumamosi katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee, Manispaa ya Ilala.
Hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa uchaguzi wa Mameya wa Manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke. Kati ya hizo halmashauri mbili zilikwenda kwa Ukawa na moja CCM.
Msemaji wa Halmashauri Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe alisema jana kuwa uchaguzi huo utafanyika kuanzia saa nne asubuhi.
Alisema wameshapokea maelekezo kutoka ngazi za juu yanayowataka kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika tarehe hiyo.
“Sasa hivi tunafanya maandalizi mbalimbali ikiwamo kutoa barua kwa wahusika,” alisema Makwembe.
Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Ramadhan Madabida alisema chama chake kipo imara na kimejiandaa vyema kushiriki uchaguzi na kuwataka wakazi Dar es Salaam kusubiri matokeo. “...CCM hatuandikii mate, siku ya uchaguzi ikifika wenyewe watajionea.”
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema Chadema na Ukawa kwa ujumla wamejipanga vizuri na kwamba wana uhakika wataibuka kidedea kutokana mtaji wa madiwani walionao.
Alisema kinachotakiwa ni mamlaka husika kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa demokrasia ili mshindi apatikane kihalali.
“Tutahakikisha tunakabiliana na mbinu zote chafu, zikiwamo za vitisho na rushwa kwa madiwani wetu. Tunataka kuwaonyesha jinsi gani Ukawa ilijipanga kuongoza Serikali,” alisema Makene.
Katika hatua nyingine; CCM Wilaya ya Ilala imepinga matokeo ya uchaguzi wa meya uliofanyika wiki iliyopita.
Katika uchaguzi huo, madiwani wa CCM walisusia na kuwaachia Ukawa peke yao ambapo, Charles Kuyeko (Chadema) alishinda kwa kura 31 na Omari Kumbilamoto (CUF) akachaguliwa kuwa naibu wake kwa kura 31.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Asaa Simba alisema wapo kwenye mchakato wa kumburuza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi mahakamani kwa madai ya kutotendewa haki.
“Tumeanza vikao vyetu na jopo la wanasheria wa chama ili kuangalia vifungu vya kisheria na haki zilizokiukwa kisha twende mahakamani,” alisema Simba.
Alisema CCM haikushiriki uchaguzi huo kutokana na hatua ya wabunge walioteuliwa na Rais Magufuli kugomewa kupiga kura. Alisema sababu nyingine iliyowafanya wasishiriki uchaguzi huo ni hatua ya wabunge wanane wa viti maalumu wakiwamo wanaotoka mikoa ya Zanzibar kuzuiwa kupiga kura wakati walipewa barua za mialiko na mkurugenzi wa manispaa hiyo. Aliwataja wabunge hao kuwa ni Amina Mollel, Stellah Ikupa, Mariam Ditopile, Mwamtum Dau, Asha Juma, Martha Mlata, Anjelina Malembeka, Subira Mgalu na kwamba Sophia Simba ndiye pekee aliyeruhusiwa kupiga kura.
ZeroDegree
Maalim Seif na Ukawa wakutana kuijadili Zanzibar
Reviewed by Zero Degree
on
1/20/2016 10:46:00 AM
Rating: