Mafuriko yaua mtoto jijini Mwanza.
Mkazi wa Mabatini jijini Mwanza akijiokoa kwa kupanda juu ya bati, baada ya eneo lao kukumbwa na mafuriko ya maji kutokana na mvua iliyonyesha jana jijini humo.
Mwanza. Mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa nne jijini hapa jana, imesababisha kifo cha mwanafunzi na uharibifu wa mali zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
Wananchi wamedai kuwa mvua hiyo, iliyonyesha kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri, haijawahi kushuhudiwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne iliyopita.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabatini, Ntobi Ntobi pamoja na kaimu kamanda wa kikosi cha Zimamoto jijini Mwanza, Hamidu Nguya walithibitisha kutokea kwa kifo cha mtoto huyo, Jenipher Joseph (6), aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mabatini.
Kamanda Nguya alisema mtoto huyo alisombwa na maji na baba yake, James Joseph walipoteleza na kuangukia mtoni wakati wakivuka daraja la Mto Mirongo uliokuwa umefurika.
“Baada ya kuanguka mtoni, baba alijikuta akimwachia mikono mtoto wake katika harakati za kujiokoa na aliposhtuka tayari mtoto yule alikuwa amesombwa na maji na juhudi za kumwokoa zilishindikana,” alisema Kamanda Nguya.
Miongoni mwa waliopoteza mali ni pamoja na Juma Said, mmiliki wa duka la vifaa vya shule na ofisi zenye thamani ya zaidi ya Sh7.5 milioni.
Licha ya ubovu wa miundombinu, eneo la Mabatini hukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na ujenzi holela uliobana kingo za Mto Mirongo.
Hadi saa 12:00 jioni jana, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kilikuwa kikiendelea na juhudi za uokoaji na kutafuta miili ya watu wanaodhaniwa kuwa wamesombwa na mafuriko hayo.
Source: Mwananchi
Mafuriko yaua mtoto jijini Mwanza.
Reviewed by Zero Degree
on
1/15/2016 02:29:00 PM
Rating: