Loading...

Burundi yatabiriwa kukumbwa na njaa.


Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza

Bujumbura,Burundi.Wachambuzi mbalimbali wamesema endapo Burundi itakumbwa na machafuko makubwa, nchi hiyo itakabiliwa na uhaba wa chakula na dawa.



Matatizo hayo yataikumba nchi hiyo baada ya nchi kadhaa wafadhili zilizokuwa zikiisadia, kujiweka kando baada ya kuibuka mgogoro wa kisiasa.

Huku hali ya Burundi ikielezewa kuzidi kuwa mbaya, viongozi wa Bujumbura wameendelea kupinga vikali mpango wa Umoja wa Afrika wa kutuma kikosi cha kusimamia amani katika nchi hiyo.

Desemba, Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika lilipitisha uamuzi wa kutuma kikosi cha askari 5,000 kuzuia nchi hiyo kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hata hivyo Serikali ya Burundi, inapinga mpango huo ikisisitiza itakitambua kikosi hicho kuwa ni askari wavamizi, hivyo kukabiliana nacho.

Uganda ambayo ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mgogoro wa Burundi inasisitiza kuwa kwa kuwa nchi hiyo ni mwanachama wa Umoja wa Afrika, inapaswa kuheshimu uamuzi wa umoja huo na kwamba, kama ina malalamikiko au pingamizi inapaswa kuwasilisha kwa kufuata sheria.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Uganda, mgogoro huo unatarajiwa kujadiliwa katika kikao cha Umoja wa Afrika kitakachofanyika Januari 30 na 31, mwaka huu Addis Ababa nchini Ethiopia.

Burundi ilitumbukia katika machafuko na ghasia za ndani baada ya Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kuwania tena kiti cha urais kwa kipindi cha tatu mfululizo Aprili mwaka jana.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia operesheni za kulinda amani , Herve Ladsous amelitumia taarifa ya siri Baraza la Usalama na kueleza kuwa, hali ya mambo nchini Burundi ni mbaya na isiyo na uthabiti.

Taarifa hiyo ilikuwa ikijibu swali la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya dharura ya kutumwa kikosi cha kusimamia amani nchini Burundi. Ladsous alisema kuzorota hali ya kisiasa na kiuchumi nchini humo inaweza kusababishwa kukumbwa na machafuko siku za usoni.




Source: Mwananchi
Burundi yatabiriwa kukumbwa na njaa. Burundi yatabiriwa kukumbwa na njaa. Reviewed by Zero Degree on 1/15/2016 02:31:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.