HII HAPA JINSI YA KUTAMBUA uzito uliopita kiasi au kupungua sana.
Jedwali la kuainisha Uwiano wa Urefu na Uzito (BMI) kutofautisha afya katika kiwango dhaifu, sahihi na iliyozidi.
Uwiano wa Uzito na Urefu wa Mwili (BMI) ni njia inayotumika kitaalamu kufahamu mtu yupo katika hali nzuri ya kiafya au la.
Kwa watu wazima, BMI ni kipimo cha kujua kama uzito unaendana na kimo. Kwa watoto wa umri wa miaka miwili na zaidi, kipimo maalumu cha BMI hutumika. Hiki ni kipimo cha kujua kama Uzito wa Mtoto unaendana na kimo, umri na jinsi.
BMI hutumika kutathimini hali ya lishe ya mtu yeyote na mtu anayeishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na ni muhimu kugundua mapema baadhi ya matatizo ya kiafya na kilishe.
Husaidia watoa huduma za afya kutoa ushauri kwa wateja wao kuepuka kupata magonjwa mengine hatari zaidi.
BMI hupatikana pale uzito katika kilogramu (Kg) unagawanywa kwa kimo (urefu) katika mita za mraba (mita kipeo cha pili). Uzito mzuri ni BMI 18 hadi 24.9. Ikizidi uzito kupita kiasi unapaswa kupunguza. Ikiwa chini ya 18 inakuwa ni chini ya uzito unaofaa hivyo juhudi za kuongezwa zinatakiwa.
Jinsi ya kupima BMI
Unachotakiwa ni kupima uzito na urefu. Kama unapima uzito, hakikisha mshale wa mizani uko kwenye sifuri wakati ukiwa hakuna chochote kinachopimwa. Anayepima uzito anatakiwa kuvaa nguo nyepesi na kuvua viatu. Anapaswa kusimama wima katikati ya mizani bila kushikiliwa au kushikilia kitu chochote. Uzito urekodiwe katika kadirio la karibu la desimali mfano kilo 20.1.
Mtu anapopima urefu, anapaswa kuvua viatu, kusimama wima, kuangalia mbele huku miguu na magoti vikiwa vimenyooka. Visigino, makalio, mabega na mgongo, vinatakiwa kugusa ukuta. Urefu urekodiwe katika kadirio la karibu la nusu sentimeta, mfano sentimeta 60.5
Ukiwa na BMI inayozidi mipaka upo katika hatari zaidi ya matatizo ya kiafya kama kisukari aina ya pili, maradhi ya moyo na saratani za aina mbalimbali.
Baadhi ya watu wazima wana maumbo makubwa yanayoweza kusababisha BMI iwe juu zaidi ya mipaka, mfano wachezaji wa Raga (Rugby) na mpira wa kikapu ambao wanaweza kuwa na uzito uliozidi sana ingawa wana miili ya kawaida. Hata hivyo hii haitaweza kutumika kwa watu wote.
BMI kwa watu wazima
BMI inazingatia kuwa watu wako na maumbo na ukubwa tofauti tofauti. Ndiyo maana mipaka (Range) ya BMI inaonyesha ni ya afya njema kwa watu wazima wa kila kimo. BMI zaidi ya mipaka ya afya njema huonyesha una uzito unaozidi kimo.
Mipaka inayotumika kwa watu wazima tu ni BMI chini ya 18.5: Huonyesha upo chini ya uzito. BMI kati ya 18.5 na 24.9: Huonyesha kuwa ni afya njema. Huonyesha uzito unaendana na kimo cha kiafya.
Kupima kiuno
Unaweza ukawa na BMI nzuri lakini bado ukawa na mafuta kuzunguka tumbo kitu kinachoweza kukuongezea hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo, kisukari aina ya pili na kiharusi au kupooza. Hivyo kupima kiuno ni njia nzuri kuangalia kama una mafuta ya ziada kuzunguka tumbo.
Ili kupima kiuno tafuta mbavu ya mwisho na juu ya nyonga na zungusha futi katikati ya mbavu ya mwisho na nyonga. Inashauriwa kutoa pumzi nje kabla ya kupima. Bila kujali kimo au BMI unapaswa kupunguza uzito ikiwa kiuno ni zaidi ya sentimita 94 kwa wanaume au sentimita zaidi ya 80 kwa wanawake.
Uzito uliopitiliza
BMI kati ya 25.0 na 29.9: Huonyesha umezidi mipaka ya kawaida, inayomaanisha uzito umezidi kawaida. Pia, ina maanisha ni mzito zaidi kuliko mtu mwenye afya njema wa kimo.
Uzito uliopita kawaida unakuweka katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kiharusi na kisukari aina ya pili.
BMI ya 30 na zaidi: Inachanganuliwa kama uzito kupita kiasi au kiriba tumbo. Kuwa na uzito kupita kiasi kunakuweka katika hatari zaidi ya matatizo ya kiafya kama nilivyoonyesha awali.
BMI ni 30 au zaidi, anapungua uzito wa kilo 6-7 katika muda wa mwezi mmoja bila hata kutumia BMI na iwapo uzito unaendelea kupungua katika muda wa zaidi ya miezi miwili.
Kupunguza uzito kuna faida nyingi ni pamoja na kuleta kuimarika kwa afya, kuondoa maumivu ya mgongo na viungo.
Funguo kubwa za kupunguza Uzito ni kupunguza vyakula vya wanga & mafuta, kufanya mazoezi ya mwili na wakati mwingine matumizi ya dawa.
Kiwango cha mazoezi ya mwili huendana na umri. Watu wazima wa kati ya umri wa miaka 18 hadi 64 wanapaswa kufanya mazoezi angalau dakika 150. Mazoezi yanayotakiwa ni kama kutembea kwa haraka na kuendesha baiskeli.
Kwa watu wazima wenye uzito uliozidi kiasi wanapaswa kufanya zaidi ya mazoezi ya kutembea kwa haraka na kuendesha baiskeli.
Unaweza pia kutumia chati ya kimo na uzito ili kujua kama uzito unaendana na kimo.
BMI kwa watoto
Kukokotoa BMI kwa mtoto, wataalamu wa afya huangalia uzito kwa kimo, umri na jinsi. Matokeo yake huitwa BMI Centile. BMI Centile ni njia nzuri kwa wataalamu wa afya kutambua kama mtoto ana uzito mzuri kiafya na kujua kama anakua kama inavyotegemewa.
BMI Centile hupatikana baada ya kupata jibu kwenye BMI ya kawaida na kulinganisha kwenye chati ya BMI ya Mtoto kulingana na jinsi yake.
Muainisho huo huweza kuonyeshwa katika kadi ya mtoto ya kupima uzito kwa kadri umri unavyoongezeka.
Baada ya kukokotoa BMI Centile, mtoto huanguka kwenye moja kati ya makundi manne.
Kama mtoto ana uzito uliozidi kiasi atakuwa katika hatari ya kuugua mara kwa mara kipindi chake cha utoto hata katika maisha ya baadaye.
Source: Mwananchi
HII HAPA JINSI YA KUTAMBUA uzito uliopita kiasi au kupungua sana.
Reviewed by Zero Degree
on
1/15/2016 02:37:00 PM
Rating: