Loading...

Simba hii ni kiboko, miezi 17 makocha wanne.


Dylan Kerr (2015-2016)

Dar es Salaam. Juni 29, 2014 wanachama wa klabu ya Simba walichagua viongozi wapya wa kuiongoza timu hiyo wakiamini itakuwa mwisho wa timu yao kufanya vibaya, lakini badala yake wameshudia timuatimua ya makocha ikiendelea.



Licha ya kutoa ahadi nyingi za kuifanya timu hiyo iwe tishio nchini, uongozi mpya ulionekana umejikita zaidi kutimua makocha, hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imesababisha timu hiyo isifanye vizuri kwenye mashindano mbalimbali.

Simba chini ya Rais Evance Aveva imeweka rekodi ya kunolewa na makocha wanne wa kigeni ndani ya kipindi cha miezi 17, ikiwa ni sawa wa kukaa na kocha moja kwa miezi minne na siku nane.

Makocha hao wote walishindwa kuendelea kuinoa timu hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kiwango cha uwanjani kutoridhisha, kushindwana dau la usajili pamoja na utovu wa nidhamu.

Kocha wa kwanza kukatwa kichwa na uongozi wa Aveva ni Mserbia Zdravko Logalusic, ambaye walishindwa kuendelea naye kwa kile walichodai kuwa, alikuwa na utovu wa nidhamu uliopitiliza ambao ulikuwa hauiletei picha nzuri klabu hiyo.

Logalusic alifuatiwa na kocha Patrick Phiri, ambaye wengi waliamini kuwa ataipa mafanikio timu hiyo kutokana na kuifahamu vyema, lakini naye alichemsha na kutupiwa virago vyake baada ya kuanza vibaya Ligi Kuu msimu uliopita akitoka sare kwenye mechi saba mfululizo.

Baada ya Phiri, uongozi wa Simba ulimpa mkataba kocha Goran Kopunovic, ambaye angalau aliirudisha timu hiyo kwenye mstari na kuiwezesha kumaliza ikiwa kwenye nafasi ya tatu.

Hata hivyo, baada ya msimu uliopita kumalizika, Kopunovic walishindwana dau na Simba, jambo lililomfanya aingie mitini, ndipo uongozi wa timu hiyo ukaamua kumleta nchini kocha Dylan Kerr kutoka Uingereza.

Pamoja na rekodi nzuri ya Kerr ndani ya timu hiyo huku akitajwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa wachezaji wa timu hiyo, Kerr alijikuta akitupiwa virago baada ya kutolewa na Mtibwa kwenye Kombe la Mapinduzi hivi karibuni.

Kocha huyo aliondolewa akituhumiwa kuwa na mbinu mbovu za kiufundi, ukaribu na wachezaji pamoja na upangaji mbaya wa kikosi.

Kutimuliwa kwa Kerr kumesababisha kuajiriwa kwa kocha Jackson Mayanja, ambaye ameungana na timu hiyo katika kipindi ambacho uongozi wa Simba umetimiza miezi 17 (sawa na siku 6,205).

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wadau mbalimbali wa soka wameendelea kushangazwa na uamuzi wa uongozi wa Simba kumtimua Kerr, ambaye aliiongoza timu hiyo kucheza mechi 30, akishinda 19, kutoka sare sita na kufungwa tano.

“Kiufundi suala la Simba kumtimua Kerr haliwasaidii kwa sababu alishaanza kuzoeleka na wachezaji na kuanza kujenga kikosi cha ushindani. Leo hii anapokuja kocha mpya inamaanisha kuwa wachezaji watalazimika kuanza upya jambo ambalo litawaathiri,” alisema Kocha Joseph Kanakamfumu.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alisema: “Uamuzi wa kumtimua kocha ni wao, lakini sikuona sababu ya kumfukuza Kerr wakati huu, timu ipo kwenye nafasi nzuri na rekodi ya mwalimu inawasuta.

“Acha waendelee kutimua makocha, sisi tunajipanga kwa ajili ya mechi yetu Jumamosi, mkakati wetu ni ushindi, pointi tatu ndiyo muhimu kwa sasa, ‘Ya Ngoswe tuwaachie Ngoswe wenyewe’.”

Morocco atajwa Simba

Kocha wa msaidizi wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Hemmed Morocco muda wowote ataingia mkataba wa kuinoa Simba.

Habari ambazo gazeti hili ilizipata zinasema uongozi wa Simba ulikuwa na kikao na kocha Morocco hivi karibuni na kinachosubiriwa ni kusaini mkataba.

“Viongozi waliongea na Morocco tangu wakiwa Zanzibar na jana (juzi), walikutana naye rasmi, kwa kifupi kila kitu kimekamilika, bado mambo madogo ya mshahara ndiyo wanajadiliana kama watakuwa na uwezo wa kumlipa, lakini inavyoonekana hadi sasa uwezekano wa Morocco kuinoa Simba ni mkubwa,” kilisema chanzo hicho kutoka ndani ya Simba.

Mwananchi ilipozungumza na Morocco alisema: “Wewe nani kakwambia mambo hayo, hakuna bwana, mi sijapata ofa yoyote nipo tu.” Morocco atasaidiana na kocha Mganda, Jackson Mayanja kuinoa Simba.



Source: Mwananchi
Simba hii ni kiboko, miezi 17 makocha wanne. Simba hii ni kiboko, miezi 17 makocha wanne. Reviewed by Zero Degree on 1/15/2016 02:41:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.