Bandari yafuatilia tuhuma za kontena la sumu.
Siku moja baada ya habari za kukamatwa kwa meli yenye shehena ya kemikali za sumu nchini Pakistan inayosadikiwa kutoka Tanzania, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imesema inafuatilia taarifa hiyo ili kujiridhisha.
Menejimenti ya TPA ilitoa taarifa jana kwa vyombo vya habari kuwa kwa sasa ni vigumu kukataa au kukubali iwapo mzigo huo ulipitia katika moja ya bandari zake kwa kuwa hakuna taarifa za kina zilizobainishwa juu ya kontena hilo. Taarifa hiyo ilisema kuwa ripoti zinazotolewa mpaka sasa hazijabainisha namba ya kontena, namba ya usafirishaji wala wakala wa meli hiyo, hivyo siyo rahisi kueleza kuwa kontena hilo lilisafirishwa kupitia Tanzania au la.
Juzi, vyombo vya habari vya kimataifa ikiwamo tovuti ya The International News iliripoti kuwa mamlaka nchini Pakistan imeikamata meli yenye kiwango kikubwa cha kemikali jijini Karachi inayotumika kutengeneza milipuko ikidaiwa kutokea Tanzania.
Mzigo huo uliokuwa ndani ya kontena la ukubwa wa futi 20 lenye uzito wa tani 21.7 ukiwa na thamani ya Rupia 860 milioni za Pakistan (Sh28 bilioni), unadaiwa kukamatwa Jumamosi iliyopita.
“Tutajitahidi kutoa taarifa baada ya kubaini chanzo cha mzigo huo na masuala mengine ya kina yanayohusiana nazo,” ilisema taarifa hiyo.
Source: Mwananchi
Bandari yafuatilia tuhuma za kontena la sumu.
Reviewed by Zero Degree
on
1/15/2016 03:05:00 PM
Rating: