Loading...

Mbowe, Lissu WAHOJI KUHUSU UHALALI wa mawaziri.




Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu wamesema Baraza la Mawaziri la Rais John Magufuli linatekeleza majukumu yake bila uhalali wa kisheria.

Wakizungumza katika mahojiano kwa nyakati tofauti, wanasiasa hao wamebainisha maeneo ambayo wanadai Rais amekiuka sheria kuwa ni kushindwa kuchapisha mwongozo wa majukumu ya wizara kwenye gazeti la Serikali na kuteua mawaziri ambao wameendelea na kazi kabla ya kuapishwa kuwa wabunge.

Kutokana na hali hiyo, wamesema ndiyo maana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), imechelewa kuunda Baraza Kivuli la Mawaziri ambalo litaundwa katika mkutano ujao wa Bunge.

Akizungumza mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro jana, Mbowe alisema baada ya Rais kuteua mawaziri alipaswa kuwakabidhi mwongozo unaoanisha majukumu ya kila wizara, lakini hajafanya hivyo.

Alisema: “Mwongozo huo huwa rasmi pale unapokuwa umetangazwa kwenye gazeti la Serikali na kupata namba, kinyume na hapo ni kuvunja uhalali wa wizara na kukosa uhalali wa kisheria.”

Rais Magufuli alitangaza Baraza lake Desemba 10, mwaka jana lenye wizara 19 likiwa na mawaziri 34.

Mbowe alisema mwongozo huo huwa ni maelekezo yanayoainisha majukumu ya kila wizara ambayo hatimaye husaidia kuundwa kwa idara mbalimbali za Serikali chini ya wizara husika.

“Rais kaunganisha wizara kadhaa, kateua makatibu wakuu katika utaratibu ambao hauko wazi sana kutokana na kukosekana kwa instrument (chombo) inayoainisha majukumu ya idara za kila wizara,” alisema.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema mwongozo uliotumika wakati wa utawala wa Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa kiasi kikubwa umebadilika chini ya JPM.

“Hadi sasa Serikali haijatoa mwongozo na bado hakuna uhakika wa mgawanyo wa majukumu ya kila wizara. Kuna mkanganyiko mkubwa wa majukumu wizarani,” alisema.

Mbowe alitolea mfano Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambayo ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika utawala uliopita, lakini sasa iko chini ya Ofisi ya Rais.

“Jambo hili limetuchelewesha katika kuunda baraza kivuli, lakini pia hali ya sintofahamu ya uchaguzi wa Zanzibar nayo imechangia kuchelewesha mchakato wa kuunda baraza kivuli,” aliongeza.

Alisema kwa kawaida, Baraza Kivuli huundwa kuakisi Baraza la Mawaziri la chama kilichoshika Dola, lakini Rais Magufuli alichelewa kutangaza Baraza lake.

Mbowe alisema Baraza Kivuli watakaloliunda litakuwa na sura ya Ukawa na litatangazwa wakati wa mkutano ujao wa Bunge endapo Serikali itatoa mwongozo huo.

“Baraza letu litakuwa dogo na litakuwa na sura ya Ukawa kwa maana litachanganya mawaziri kutoka vyama vyote vinavyounda umoja wetu. Umoja wetu ni ndani na nje ya Bunge,” alisisitiza Mbowe.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikiri kwamba mwongozo huo haujatangazwa katika gazeti la Serikali lakini akasema hiyo haizuii shughuli za Serikali kuendelea.

“Kuwa gazzeted (kutangazwa) ni habari moja, lakini Serikali inafanya kazi kwa sababu huo ni utaratibu tu wa Rais wa jinsi ya kugawanya majukumu kwenye Serikali,” alisema. “Ile kuitangaza kwenye gazeti la Serikali ni hatua ya mwisho, haizuii kazi kuendelea. Kwa hiyo itakuja tu kutoka kwenye gazeti la Serikali. Siyo kwamba haipo, ipo itatangazwa tu.”

Lissu acharuka

Wakati Mbowe akizungumzia mwongozo huo, Lissu alieleza kushangazwa na mawaziri walioteuliwa na Rais Magufuli kuanza majukumu yao wakati hawajala kiapo kuwa wabunge. Huku akinukuu Ibara ya 55(4) ya Katiba inayotaka mawaziri wote watokane na wabunge na ile ya 68 inayotaka mbunge kuapa kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake, Lissu alisema si sahihi mawaziri hao kuanza kazi kabla ya kiapo cha ubunge na kutoa maagizo mazito yanayoathiri maisha ya watu.

Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Dk Augustine Mahiga (Mambo ya Nje, Kikanda na Afrika Mashariki), Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) na Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Ufundi Stadi).

Alisema, “Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema mawaziri watatokana na wabunge na ili kuwa mbunge lazima mtu aape. Kwa maana hiyo watendaji hao siyo mawaziri kwa kuwa hawajaapa kuwa wabunge. Nashangaa kuona wanatoa maagizo halafu yanatekelezwa.”

Hata hivyo, alieleza kuwa hilo ni tatizo la mfumo na utamaduni uliojengwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere na kudai kwamba Serikali haioni tatizo kuvunja sheria.

“Wanasema (Serikali) kwani itatokea nini? Ni kweli hakitatokea chochote. Lakini hayo yangefanyika Kenya au Uganda watu wangepiga kelele na kingetokea kitu. Lakini kwa hapa kwetu ukianza kuhoji tena kwa kutumia sheria tulizotunga wenyewe, watasema huyo mchochezi, lakini kwa nini tusijifunze kuheshimu sheria?” alihoji.

Alipoulizwa endapo kuna haki yeyote inayowalinda watu walioathirika na maagizo yaliyotolewa na mawaziri hao watatu alijibu; “Wananchi wana haki ya kuwashtaki hawa mawaziri ambao wanatoa maamuzi wakati bado hawajapishwa kuwa wabunge.”

Ilivyokuwa enzi za Kikwete

Hali kama hiyo ya uteuzi wa mawaziri kabla ya kuwa wabunge ilitokea Mei 4, 2012 wakati Rais mstaafu Jakaya Kikwete alipoteua mawaziri wapya kutoka miongoni mwa wabunge aliokuwa amewateua.

Baada ya uteuzi huo, kuliibuka mjadala kwamba hatua ya Rais kuwateua wabunge wapya ambao hawajaapishwa bungeni kuwa mawaziri ni uvunjaji wa Katiba.

Mjadala huo ulimlazimu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kutoa ufafanuzi akisema Rais alifanya hivyo kwa kutumia mamlaka aliyonayo kikatiba.

“Hapa kuna mamlaka ya Rais ya uteuzi wa wabunge na masharti ya Ibara ya 66 (1) (e) yenye aina ya wabunge wasiozidi 10 watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c) za ibara ya 67 na angalau wabunge watano kati yao wakiwa wanawake, hivyo wabunge waliokuwa wameteuliwa walitokana na Ibara hiyo,” alisema.

Jaji Werema alifafanua kuwa baada ya hatua zote hizo ikumbukwe kwamba aliyeteuliwa au kuchaguliwa kuwa mbunge anakuwa mbunge ama baada ya kutangazwa na msimamizi wa uchaguzi; au baada ya kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa wale wabunge wa viti maalumu au anapochaguliwa na Baraza la Wawakilishi au anapoteuliwa na Rais akitumia mamlaka yake ya uteuzi yanayotokana na Ibara ya 66(1)(e).

“Hivyo wabunge wanaohusika hawahitaji kuapishwa kwanza bungeni ili wawe wabunge kwa kuwa kiapo cha mbunge bungeni kinamwezesha tu kushiriki shughuli za Bunge.

“Katiba ya nchi haiweki kwa Rais masharti kwamba kabla ya kumteua mbunge wa aina hiyo kuwa waziri au naibu waziri, mbunge huyo awe ameapishwa bungeni kwanza,” alieleza Jaji Werema katika ufafanuzi wake huo na kuongeza:

“Masharti mawili muhimu na ya kuzingatia ni kwamba mteule wa nafasi ya uwaziri au naibu waziri hatashika madaraka yake ila mpaka kwa mujibu wa Ibara ya 56 ya Katiba, awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”

Alitaja sharti la pili, litahusu kiapo cha uaminifu katika Bunge kabla mbunge hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge kwa masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba, hivyo kusema viapo hivyo havitegemeani na vinaweza kufanyika kwa nyakati tofauti.

Katika ufafanuzi huo, Jaji Werema alisisitiza kwamba wabunge ambao hawakuwa wameapishwa ndani ya Bunge ni wabunge na wanapoteuliwa kushika nafasi ya uwaziri au naibu waziri ni halali kwa kuwa uteuzi huo haukiuki masharti yoyote ya kikatiba au sheria. 




Source: Mwananchi
Mbowe, Lissu WAHOJI KUHUSU UHALALI wa mawaziri. Mbowe, Lissu WAHOJI KUHUSU UHALALI wa mawaziri. Reviewed by Zero Degree on 1/14/2016 05:08:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.