Mfumuko wa bei waongezeka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo alisema mfumuko wa bei za bidhaa kwa Desemba, mwaka jana umechangiwa na mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonyesha kuongezeka ikilinganishwa na bei za Desemba 2014.
Alisema mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.8 kwa Desemba ikilinganishwa na 0.5 kwa Novemba.
“Bidhaa zilionyesha kuongezeka bei katika kipindi cha Desemba ni pamoja na bei za mchele kupanda hadi kufikia asilimia 28.2, mahindi kwa asilimia 16.4, unga wa mahindi asilimia 11.1 nyama asilimia 11.3, samaki asilimia 8.9, maharagwe asilimia 9.7 na viazi kwa asilimia 20.2.”
Vilevile, alisema mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonekana kuongezeka ikilinganishwa na bei za Desemba 2014 ni pamoja na bei za mavazi kwa asilimia 4.9, huduma za afya asilimia 11.1 vyakula kwenye mighahawa asilimia 8.3 na gharama za malazi kwa asilimia 6.8.
Hata hivyo, alisema uwezo wa Sh100 ya Tanzania kununua bidhaa na huduma umefikia Sh62.02 kwa Desemba mwaka jana ikilinganishwa na Sh62.31 ilivyokuwa Novemba mwaka jana.
Alisema mfumuko wa bei za bidhaa nchini una mwelekeo unaofanana na baadhi ya bidhaa za nchi nyingine Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na ongezeko la asilimia 8.01 Kenya kutoka asilimia 7.32 kwa Novemba na Uganda ongezeko la asilimia 9.30 kutoka 9.18 Novemba mwaka jana.
Source: Mwananchi
Comment & Share this!!
Mfumuko wa bei waongezeka.
Reviewed by Zero Degree
on
1/09/2016 05:12:00 PM
Rating: