Loading...

Miradi ya MAMILIONI YA FEDHA kunufaisha vijiji vya Karatu.


Mkurugenzi wa shirika la world vision Tanzania, Tim Andrews

Karatu. Wakazi wa vijiji vya Endesh, Kambi ya Faru na Gidamilanda wilayani hapa Mkoa wa Manyara, watanufaika na miradi ya elimu, afya na maji iliyofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania kupitia mradi wa Dream Village yenye thamani ya zaidi ya Sh620 milioni.

Akizungumza juzi mbele ya wafadhili wa miradi hiyo ya maendeleo kutoka Korea, Mratibu wa World Vision wilayani hapa, John Massenza alisema imetekelezwa kwenye maeneo ya wafugaji yaliyopendekezwa na Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Allitaja miradi hiyo kuwa ni ya zahanati iliyojengwa Kijiji cha Endesh kwa ajili ya kuhudumia wakazi 1,710 wa vitongoji vya Mohedageu na Delajida iliyogharimu Sh90 milioni na wa ujenzi wa lambo la maji kwa matumizi ya nyumbani na mifugo lenye thamani ya Sh160 milioni. Massenza alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutawapunguzia kero wakazi hao ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya na maji.

“Miradi hii ni yetu wote, tushirikiane kuitunza ili iwe endelevu,” alisema Massenza.

Pia, zimejengwa nyumba mbili za walimu, madarasa mawili na madawati kwa ajili ya Shule ya Msingi Gidamilanda, yenye thamani ya Sh170 milioni kwa lengo la kuhamasisha elimu kwa watoto wa wafugaji.

Mratibu Elimu wa Kata ya Baray, Lucas Tluway, alisema shule hiyo ilianza mwaka 2008 ikiwa na madarasa mawili.

Alisema kwa sasa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa shuleni hapo imeongezeka kutoka asilimia 40 ya awali na kufikia asilimia 90 mwaka jana.

Ofisa Tarafa a Lake Eyasi, Abdul Barie alisema Serikali haitamvulia mzazi yeyote atakayeshindwa kumpeleka shule mtoto wake au kumuachisha masomo kwa sababu ya kuchunga mifugo.

Akizungumza wakati wa kutambulisha mradi wa maji wa Kijiji cha Kambi ya Faru, Kata ya Kansay uliogharimu Sh 200 milioni Mratibu wa World Vision Endabash, Gloria Mashingia alisema utasaidia kupunguza magonjwa yanayosababishwa na maji yasiyo salama.


Source: Mwananchi
Miradi ya MAMILIONI YA FEDHA kunufaisha vijiji vya Karatu. Miradi ya MAMILIONI YA FEDHA kunufaisha vijiji vya Karatu. Reviewed by Zero Degree on 1/12/2016 12:31:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.