Loading...

Mapinduzi yalichochewa na matokeo ya uchaguzi 1963.


Mzee Abeid Aman Karume (Mwenye suti nyeusi), pamoja na viongozi wengine wa mapinduzi wakipungia mikono wananchi. Picha ya Maktaba.

Mzee Aboud alinukuliwa na Mohamed Ghassany katika kitabu chake Kwaheri Ukololoni, Kwaheri Uhuru akisema:

“Tuanze pale baada ya uchaguzi wa Julai 1963, watu walivyokuwa kama wamepata kiharusi. Nilivokuta mimi. Mimi binafsi nilikuwa mtumishi wa serikali bara, katika Baraza la Mji, Dar es Salaam katika miaka ya 1950. Ikaundwa TANU katika mwaka 1957. Mimi nilikuwa mwanachama wa TANU. Baada ya harakati za kisiasa zilokuwepo kule Tanganyika na hapa Zanzibar tarehe 31 Disemba 1959, nikaacha kazi kule Dar es Salaam nikaja Unguja 1960 Januari, mimi nipo Unguja.

Nimekaa nikaangalia hali ya mambo, nikajiunga na Afro-Shirazi Mei 27, 1960 na tawi langu lilikuwa Mwembetanga. Baada ya shughuli za kisiasa 1961 zikatokea fujo Unguja. Ilipotokea riot ya Unguja kwa hakika mimi nilikuwa siijui.

Nilikuwa wakala katika Kituo cha Polisi Mwera, ilipokuwa Skuli ya Mwera Jimbo la Fuoni. Mgombea wa Afro-Shirazi alikuwa Aboud Jumbe, mgombea wa Hizbu alikuwa Maalim Hilali. Baada ya muda wa kupiga kuara, kituo kufungwa tukapata habari kuna ugomvi, fujo. Hapo tukaja sisi kuchukuliwa na gari ya polisi, ikiwa chini ya usimamizi wa Major Bott, tukapelekwa Fuoni kwenye kituo cha kuhesabia kura. Mimi nikiwa wakala katika Kituo cha Kupigia Kura cha Mwera, nikawa wakala wa kuhesabu kura katika Kituo cha Fuoni.

Baada ya uchaguzi kwisha, mahesabu ya uchaguzi kumalizika, ikawa ni usiku, tukipanda ndani ya gari ileile, chini ya Major Bott, mpaka Kijangwani ilipokuwa ofisi ya Afro-Shirazi kwa mambo ya uchaguzi. Tukatuliwa pale, akaripoti Bott kwa ofisi ile kwa watu wa Jimbo la Fuoni wa Afro-Shirazi ndo hawa na watu wa Hizbu sijui kenda nao wapi, lakini sote tulipakiwa kwenye gari moja chini ya ulinzi wa polisi kwa usalama wetu. Tukaongoza, mimi nikaja zangu nyumbani nikaletwa na polisi mpaka kwangu, basi umekwisha uchaguzi ule na ghasia zile, watu wakatiwa ndani, wakafungwa, wengine wakahukumiwa miaka mingi na kundi la watu likakamatwa likajaa jela tele, wakapelekwa kisiwani wengine. Kwa bahati nzuri au mbaya, lakini kwa maisha ya kisiasa kila mtu aliyekuwa na mwamko kidogo wa kisiasa anaweza kuona kuwa ilikuwa bahati nzuri kukamatwa kwangu nikawekwa jela.

Nilikaa rumande, nikashtakiwa mahakamani kiasi ya miezi sita. Sikuweka rekodi hiyo. Niliposhtakiwa, nilishtakiwa pamoja na mtu mwengine, mimi nilikuwa mshtakiwa nambari moja, yule mwenzangu ni mshtakiwa nambari mbili. Na mashtaka yetu kwamba tumechochea na nimeongoza fujo, tangu wakati wa asubuhi, kuanzia saa 4 asubuhi mpaka saa 12 jioni.

Sote tulikuwa na shahada za memba wa kuhesabu kura au wa kituo cha kupigia kura, ASP na Hizbu. Na kwa bahati nzuri kituo cha kupigia kura chetu ofisa wake alikuwa Maalim Ali Said Al Kharusi na mgombea alikuwa Maalim Hilali kwa ZNP. Walikuwepo polisi kulinda usalama aiikuwepo Inspekta Aboud Saidi… Kwa sababu hawa wote, wagombea wa ZNP na maofisa wa polisi walikuwa ni mashahidi wangu ndani ya korti kwamba mimi sijakuwemo katika fujo za Juni na wengine polisi akiwa mmoja ni Aboud Saidi, huyu ndo aliyekuwa na dhamana ya eneo lile wakati ule. Ijapokuwa wote niliowatia hawakuitwa mbele ya mahakama, iliridhika kama mimi sijakuhusika na fujo, nitolewe, sina makosa. Mashahidi walikubali baada ya kutia saini zao. Hawakukataa kwani wananijua tangu utoto, nilipokuwa skuli lakini habari ya uchaguzi walikuwa hawajui mpaka nilipotoa hati ambazo zina saini zao. Na ile kesi ilishikwa na mwanasharia Talati. Ikawa mimi sina kesi ya kujibu, nikaachiwa huru.

Nilipomaliza tumekaa tukizungumza habari ya fujo watu kwa jumla, memba wote wa Afro-Shirazi walikuwa wamevunjika moyo na tayari kufanya ugomvi wowote kama walivoanziwa, lakini matokeo yake yalikuwa si mazuri kwa sababu wale watu wanoishi mashambani pande zote mbili, upande wa Afro-Shirazi na upande wa Hizbu, lakini kuna baadhi ya watu walikuwa si Hizbu wala si Afro-Shirazi , lakini waliathirika katika ghasia zile kwa kuumia, wengine watu wenye mashamba yao ambao ni memba wa ZNP waliwakatiakatia migomba wakawafukuza kwenye mashamba, matokeo yakawa si mazuri, uhusiano wa kijamii ukawa mbaya. Na jamaa waliokuwa Hizbu ambao wanakaa kule wanyonge wameishiwa wameumizwa, wamepigwa, wengi wamekufa. Haijulikani nani kafanya na saa ngapi imetokea, haijulikani, ni vurugu.

Ukweli wa mambo uchaguzi ulikuwa na mambo ya kupenyezana watu ambao walikuwa na haki ya jimbo lile au na wengine hawana haki ya jimbo lile. Hizo ndo sababu mpaka leo watu wanagombana hapa Unguja. Imeshakuwa sugu hiyo. Inavyosemekana ni kituo cha Gulioni kiloanza fujo ikaambukizwa na Darajani. Kituo cha kule kilianza fujo kwa sababu ya watu kutoka Funguni kuja Gulioni kupiga kura, ni karibu pale wanavuka tu. Sasa na kwa mujibu wa wakati ule watu wa Malindi walikuwa wakiogopwa kwa sababu walikuwa wana umoja, akipigwa mmoja wamepigwa wote. Hivo ndo ilikuwa watu wanawaogopa. Mimi si shahidi wa jambo hilo. Inavyosemekana, ndo ikaendelea ghasia Darajani ambako ilikuwa kubwa. Basi pale tukawa tunakaa tunafanya uchaguzi kwa kujiamini, tunajiona akilini mwetu kwamba sisi ni wababe! Hata ulipofanywa uchaguzi wa mwisho, na hapa katikati ilikuwa Serikali ya mpito, mpaka tulipokuja kwenye uchaguzi wa mwisho [Julai 1963], ZNP ikapata Serikali baada ya kuunganisha viti na ZPPP. Mimi na Ahmed Diria tuilikuwa wakala wa kuhesabu kura, kituo cha Victoria Garden, ndio uchaguzi ulikohesabiwa. Tukashindwa. Wa jimbo hilo la Darajani tukashindwa kwa voti 200 na mgombea wetu alikuwa Thabit Kombo. Mgombea wa ZNP alikuwa Ibun Saleh. Nilipofika nyumbani sikutoka nje kabisa.

Nililala nyumbani nikiwa na uchungu. Kulikuwa hakuna sababu ya kukosa jimbo. Na tukajua sababu zengine za kukosea, baadae. Siku ya pili nikenda Gongoni.



Uchaguzi au risasi?

Kujua chanzo cha mapinduzi… Sasa kwa mfano wangu, mimi nimejua mapinduzi kutokana na Saleh Saadalla, ndo alonambia; “sasa tufanye mapinduzi.” Kwa kweli zile fikra yeye alizozitoa kuhusu mapinduzi zimetokana na uchaguzi kwa ninavyozielewa mimi. Uchaguzi ule kwamba tushashindwa, lakini tulioshindwa tuna idadi kubwa ya voti kuliko waloshinda. Lakini walioshinda wana majimbo mengi zaidi kuliko sisi wenye idadi kubwa ya voti. Sasa hapa hizi ndo fikra za Saleh zilizoingia kwangu na mimi nikakubali tufanye mapinduzi.

Haijawa uchaguzi wa kura kwa mtu mmoja. Uchaguzi ulokuweko ni wa viti. Mtu mmoja, voti moja, ndo ilivyokuwa, lakini ushindi hauhesabiwi kwa mujibu wa idadi ya kura. Ukihisabiwa kwa idadi ya ushindi wa viti, majimbo, ndo aliyeshinda. Sasa ukija kuangalia idadi kubwa ya viti ilikuwa baina ya vyama viwili, mchanganyiko wa viti vya Chama cha Hizbu, mchanganyiko wa viti vya ZPPP vilipoungana pamoja, vikawa ni vingi kuliko viti vya Afro-Shirazi.

Kiti cha Mlandege wamechukuwa Hizbu. Tulipitwa kwa kura 200. Na zilikuwa hizi kura zilopita hapa, ni wapiga kura wa Kihindi, ambao hawakuipigia Afro-Shirazi. Waliipigia Hizbu. Ni wao walikuwa idadi yao mia nne. Wengi wao ni Wahindi wa jamatini. Ukichambua, kwa nini wakatupita wakati sisi tulikuwa tumewapita Hizbu kwa kura 200 kabla kufanya hesabu za Wahindi ambao walikuwa ni kura 400 Kwa sababu walikuwa Wahindi wale kutoka Mlandege njia panda, Darajani, mpaka Mlandege, kituo cha polisi. Kwa maoni ya kila mtu, uchaguzi mkuu wa Julai 1963 ulikuwa wa haki asilimia 100. Kwa fikira zangu, kila mtu anaweza kusema anavotaka. Mapinduzi yamekuja kutokana na fujo za Juni baada ya uchaguzi.


Source: Mwananchi
Mapinduzi yalichochewa na matokeo ya uchaguzi 1963. Mapinduzi yalichochewa na matokeo ya uchaguzi 1963. Reviewed by Zero Degree on 1/12/2016 12:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.