Loading...

Mapinduzi YATAENZIWA demokrasia ikiruhusiwa.


John Okello akionyeshwa jinsi ya kutumia bunduki. Picha kwa msaada wa mtandao.

Wakati jua lilipokuwa linachomoza siku ya tarehe 12 Januari, 1964 watu wa Zanzibar, majirani zao na ulimwengu ulipata taarifa ya kufanyika mapinduzi katika visiwa hivyo vya karafuu.

Sasa mapinduzi yaliyouondoa madarakani utawala wa kisultani na serikali yake ya mseto ya vyama viwili, Zanzibar Nationalist Party (Hizbu) na Zanzibar and Pemba Peoples’ Party (ZPPP) iliyokaa madarakani kwa mwezi mmoja tu baada ya serikali ya Uingereza kutoa uhuru kwa visiwa vya Unguja na Pemba, yametimiza miaka 52.

Zaidi ya robo tatu ya watu milioni 1.3 wanaoishi Zanzibar walikuwa hawajazaliwa pale mapinduzi yalipofanyika kwani visiwa hivi vilikuwa na watu 300,000 tu, kati yao wageni wasiozidi 2,000.

Mapambano ya kuipindua serikali yalichukua masaa machache, lakini yalipelekea zaidi ya watu 500, wakiwamo wazee na watoto wadogo kupoteza maisha, baadhi yao kwa njia za kikatili, kama kuchomwa moto ndani ya tanuri (jiko la kukaushia nazi).

Kila ifikapo wakati kama huu maadhimisho ya siku hii huwa na sherehe na shamra shamra za kila aina za wiki nzima au zaidi, ikiwa pamoja na kuwakumbuka waliojitolea roho zao kufanikisha kufanyika kwa mapinduzi na kuzindua miradi ya maendeleo.

Madhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati Wazanzibari hawajua hatima ya visiwa vyao kisiasa.

Hii inatokana na mtafaruku wa kisiasa ulioibuka baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka jana ambao ulitarajiwa kustawisha demokrasia na badala yake kuonekana umeirudisha Zanzibar hatua kadhaa nyuma.

Wakati upande wa pili wa Muungano (Tanzania Bara) mwishoni mwa mwaka jana ilijiuzia kutumia mabilioni ya shilingi kwa sherehe za uhuru na kutumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe kupunguza matatizo katika sekta mbali mbali, kama afya, elimu na huduma za jamii, Zanzibar imejitutumua kufanya sherehe za Mapinduzi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Tofauti na ilivyokuwa miaka michache iliyopita palipokuwapo maelewano kati ya mahasimu wawili wakuu wa kisiasa wa Visiwani, CCM na CUF, sherehe za mwaka huu zimechukua sura ya kichama badala ya kitaifa.

Hii inatokana na CUF kuzisusia kwa madai kuwa Serikali inayoendelea kushika madaraka ya ya Rais Ali Mohamed Shein haina mamlaka halali ya utawala na kwamba kitendo cha kuufuta uchaguzi kilikusudiwa kukipora chama cha CUF ushindi baada ya kugundua kuwa chama hicho kilishinda katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kilichokuwapo sasa ni mvutano kati ya CCM na CUF. Wakati CCM inashikilia uchaguzi ufanyike upya, CUF ambayo inaungwa mkono na nchi nyingi za Jumuiya ya Kimatafa na taasisi zilizochunguza uchaguzi inasema hapana haja ya kurejea uchaguzi badala yake mchakato wa kutangaza matokeo uendelee na mshindi atangazwe.

Mvutano huu umeiweka Zanzibar katika hali tete na kuwa vigumu kutabiri kitakachotokea siku za usoni. Lakini baya zaidi ni kushuhudiwa matokeo mbali mbali ya watu kupigwa, nyumba kuchomwa moto, waandishi wa habari kuandamwa kama paka mwizi na uhuru wa habari na kujieleza kubanwa.

Nani aliongoza Mapinduzi?

Pamekuwapo maelezo tafauti ya nani hasa alipanga na kuyaongoza mapinduzi. Lakini vitabu vingi vya historia vinasema kuwa yaliongozwa na John Okello mzaliwa wa Uganda wa kabila la Lango na msaidizi wake ni Mkenya, Absalom Engine.

Lakini zipo taarifa kwamba watu hawa wawili walisogezwa mbele ili kama mapinduzi yasingefanikiwa basi pangejengeka dhana kwamba mpango huo ulikuwa na mkono wa kigeni na kwamba wazalendo wa Zanzibar hawakuhusika. Okello alikuja Zanzibar mwaka 1957 na wiki chache kabla ya kufanyika Mapinduzi Okello alikuwa akivunja mawe ya ujenzi Micheweni, Kaskazini Pemba. Aliletwa Unguja na mzee Lumumba ambaye alikuwa mwanachama wa Afro Shirazi Party na baadaye kuwa mstari wa mbele katika lile kundi la kwanza liliohamia kambi ya polisi ya Ziwani kufanya mapinduzi usiku wa kuamkia tarehe 12 Januari, 1964. Huyu mzee Lumumba baadaye alikuwa miongoni mwa waasisi wa chama cha CUF Visiwani.

Wapo wanaosema kiongozi wa mapinduzi ni Mzee Abeid Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar aliyeuawa kwa kupigwa risasi tarehe 7 Aprili, mwaka 1972.

Lakini zipo habari kuwa Mzee Karume aliarifiwa habari ya mapinduzi akiwa nyumbani kwake asubuhi ya Januari 12, lakini alikuwa na fununu za kutaka kufanywa vurugu usiku wa Januari 11 na kuiarifu vyombo vya usalama ili asijumuishwe na vurugu hizo zilizosababisha kufanyika mapinduzi.

Katika miaka ya kwanza ya mapinduzi hali ya Zanzibar ilikuwa ya kutisha. Leo unasikia huyu kauliwa, yule kawekwa kizuizini na wengine kuondoshwa nchini kwa nguvu na kuwaacha wake zao na watoto wao.

Kwa kiasi fulani mambo haya na mengine, hasa katika kisiwa cha Pemba na kucharazwa bakora, yamechangia misuguano ya kisiasa, chuki, uhasama na watu kutoaminiana. Baada ya juhudi za kupata mwafaka zilizotoa mwanga wa matumaini, huku watu wa Visiwani wakisema yaliyopita si ndwele tugange yajayo, pamechomoza kundi la watu lisiofurahia hali hii.

Watu hawa wamebeza kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wamediriki kutaka visiwa vya Unguja na Pemba vigawane kwa kila kimoja kuwa na serikali yake na kuanzisha vikundi vya kiaina ambavyo vimekuwa vikitishia usalama wa watu kwa kuwapiga ovyo mitaani na majumbani.

Hapana ubishi kwamba mapinduzi yamefanya hali ya maisha Visiwani kuwa bora zaidi, lakini sio kweli kwamba hali ilikuwa mbaya kama baadhi ya watu walivyoieleza.

Ninakumbuka kusoma na kucheza na watoto wa familia ya mfalme, kuwahi kubeba jeneza kwa masafa kwenda makaburini Rahaleo na mfalme na kuwaona wana wa familia ya mfalme wakitibiwa katika hospitali kuu ya Serikali ya Mnazi Mmoja.

Hata mfalme Abdalla bin Khalifa, baba wa Sultani Jemshid aliyepinduliwa alikatwa mguu katika hospitali ya Mnazi Mmoja.

Pamekuwapo maelezo kwamba serikali iliyopinduliwa ilikuwa ya Waarabu. Hii sio kweli kwani baraza la mawaziri lilikuwa na mchanganyiko wa watu wanaoishi Visiwani - Waarabu wawili, Mhindi mmoja, Wangazija wawili, Washirazi sita, watatu kutoka Unguja na watatu Pemba ,Watumbatu wawili na Wahadimu wawili.

Mawaziri wote walizaliwa Zanzibar na wengine ni wenye asili ya zaidi ya vizazi sita Visiwani na hakuna kati yao aliyekuja Zanzibar kwa biashara ya kutumia upepo wa Mansoon kutoka Arabuni na India au kuja kutoka nchi za jirani kuchuma karafuu au kufanya kazi nyengine ya kujitafutia maisha.

Ukiachilia kasoro nyingi, hasa za uvunjaki wa haki za binadamu, mapinduzi yamesaidia kuboresha huduma za elimu na afya, lakini zaidi katika miaka ya kwanza ya mapinduzi.

Hata bei za bidhaa nyingi na hasa chakula zilikuwa zikifidiwa na serikali, lakini baadaye pakawa na upungufu mkubwa wa chakula hadi kusababisha kutolewa kwa mgao.

Wapo wanaosema zamani elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi na kwamba Waswahili (Waafrika) walikuwa wananyimwa haki za masomo. Lakini ukiangalia orodha ya Waswahili walioelimika na kufikia Chuo Kikuu katika miaka ya 1940 na 1950 utashangaa hoja hii imetolewa kwa misingi gani.

Kwa mfano Rais wa pili mstaafu wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, Rais wa pili mstaafu wa Tanzania, Sheikh Ali Hassan Mwinyi, Rais wa nne wa Zanzibar, marehemu Idris Abdulwakil na aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, marehemu Sheikh Ali Khamis walipata elimu ya chuo kikuu katika miaka ya 1940 na mwanzoni mwa 1950. Je, hawa ni Waarabu au Wahindi.

Kama ni ubaguzi kufanyika basi hii ilitokea baada ya Mapinduzi kwa vile palikuwako mgao wa asilimia kwa makabila kwa wanafunzi kufaulu kupata masomo ya elimu ya juu, badala ya kipimo kuwa kufaulu kwa mwanafunzi. Hapa labda niulize wapi duniani wanafunzi hufaulu kwa mgao wa makabila yao badala ya namna walivyofanya mtihani kama sio Zanzibar ya zama zile?

Tafsiri nzuri na sahihi ya Mapinduzi ni kufanya mabadiliko yanayoleta kheri na sio balaa, mauaji na chuki. Wazanzibari wataweza tu kuyaendeleza mapinduzi ya 1964 na kuyafanya kuwa na maana kwao na vizazi vijavyo kama watafanya juhudi za kuleta maelewano mazuri zaidi miongoni mwao na sio kuwakumbatia wale wanaotaka kuleta mfarakano.

Lililo muhimu kuliko yote ni kuangalia yaliyopita kama sehemu ya historia na kuendeleza mazuri kwa kuachana na mabaya. Ni kusameheana tu kwa nia njema na thabiti na sio kuwekeana kisasi.


Source: Mwananchi
Mapinduzi YATAENZIWA demokrasia ikiruhusiwa. Mapinduzi YATAENZIWA demokrasia ikiruhusiwa. Reviewed by Zero Degree on 1/12/2016 12:28:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.