Loading...

Wajibu wa SERIKALI, JAMII KUREJESHA HADHI ya walimu.


Ubora na thamani ya mwalimu ni jambo la msingi katika mustakabali wa mwanafunzi yeyote.



Katika ngazi zote anazopitia mwanafunzi na hata hatua za makuzi ya kimwili, kiroho na kiakili, mwalimu ana nafasi ye kipekee. Ni mtu majununi pekee anayeweza kupuuza nafasi hii aliyonayo mwalimu.

Ni uwazi usiofichika kuwa ubora wa elimu pamoja na hadhi ya ualimu, vimeanguka mno katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la HakiElimu ya miaka 10 ya Serikali ya awamu ya nne katika elimu, iliyozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana, ubora wa elimu ya Tanzania umeshuka mno katika kipindi hicho kuliko wakati mwingine wowote baada ya uhuru.

Ingawa Serikali ya awamu ya nne, ilifanya jitihada kubwa za kutanua wigo kwa wanafunzi kuandikishwa katika shule kuanzia zile za awali hadi vyuo vikuu, ukweli unasalia kuwa hali ya elimu ilikuwa mbaya kwa kuangalia viwango vya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi, kidato cha nne, kidato cha sita na hata vyuo vikuu.

Wanafunzi wengi walionekana kutoiva kitaaluma, suala ambalo hata watawala wamewahi kusikika wakisema; “ wasomi wa Tanzania hawauziki ndani na nje”

Hali hiyo iliwafanya wadau wa elimu kulaumu Serikali na wengine waliwatupia makombora, walimu wenye dhamana kubwa ya kuwasaidia wanafunzi kutambua vipawa na uwezo.

Zipo sababu nyingi zilizochangia wadau kuwalaumu walimu kuwa hawatekelezi majukumu yao ipasavyo na kwamba hawana wito kama walivyo kuwa walimu wa miaka ya nyuma hasa wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere. Hata hivyo, wanaowalaumu walipaswa pia kuhoji ni kwa mazingira yapi mwalimu huwa bora?

Historia inaonyesha kuwa miaka ya 1975, thamani ya mwalimu ilikuwa juu tofauti na ilivyo sasa, mitazamo ya jamii na hata baadhi ya walimu wenyewe ni tofauti kabisa na mitazamo ya watu wa zamani.

Wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Nyerere, walimu walitembea vifua mbele kutokana na heshima waliyokuwa nayo katika jamii zilizowazunguka.

Ni vyema Serikali ya sasa ambayo imeonyesha imani kwa wananchi wake kuwa wataleta ‘mabadiliko’ makubwa katika sekta ya elimu na sekta nyingine, irejeshe hadhi ya mwalimu na kumboreshea mazingira yake ili atengeneze kilicho bora kwa masilahi ya vizazi na vizazi.

Chapisho la HakiElimu la mwaka 2010, linaeleza wazi masuala kadhaa ya kurejesha hadhi ya mwalimu ili aweze kufundisha kwa ubora na awe mahiri katika kazi yake.

Miongoni mwao ni pamoja na kuwapa walimu motisha, hasa wale waliopangwa kufundisha shule za pembezoni, kuwapandisha madaraja, kuwahakikishia fursa za kuendelea kitaaluma kwa njia ya mafunzo ya kujiendeleza kazini na njia nyinginezo.

Kuna ushahidi kwamba taaluma ya ualimu haivutii walimu bora kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mazingira duni ya kazi. Walimu wengi waliopangiwa maeneo ya vijijini na hasa yale yenye hali ngumu wanaripoti kwa idadi ndogo, na wale ambao tayari wako kule wanatafuta uhamisho kwenda katika maeneo ya mijini

‘‘Njia moja ya kuingiza motisha na ya kupunguza tabia ya utoro na kuacha kazi kwa walimu ni kuwapa miundo ya kazi ya kuvutia.

Zaidi ya mshahara ambao bado ni suala kubwa la mjadala ndani ya jamii, fursa zilizopo kwa walimu za kupandishwa cheo na maendeleo binafsi na ya kitaaluma nayo ni muhimu,’’ linasema chapisho la Unesco liitwalo: Elimu ya Msingi kwa wote barani Afrika: Changamoto ya Mwalimu.

Kazi kubwa iliyopo ni kuyatazama kwa jicho pevu mazingira ya kitaaluma, kwani hata elimu ikiwa bure, mazingira ya kufundishia na kujifunzia yakaboreshwa, ruzuku zikafika kwa wakati shuleni, kama walimu wataendelea kukosa nyumba au kuonekana watumishi wasio na umuhimu, elimu bora itaendelea kuwa suala la kusadikika.

Kama ambavyo kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ inavyoendelea kushika kasi, basi kasi hiyo pia ifumue kabisa mazingira yanayowafanya walimu wasifanye kazi kwa ufanisi.

Walimu ni kada muhimu ya utumishi, walimu ni nguzo ya maendeleo ya sekta ya elimu.

Ni wakati mwafaka kwa Serikali ya awamu ya tano kuitazama kada hii kwa jicho la karibu ili walimu wapate ari na kuwa chachu ya elimu bora shuleni na vyuoni.

Dennis Mwasalanga ni ofisa programu Idara ya Habari na Utetezi HakiElimu. Anapatikana kwenye barua pepe media@hakielimu.org



Source: Mwananchi





Wajibu wa SERIKALI, JAMII KUREJESHA HADHI ya walimu.  Wajibu wa SERIKALI, JAMII KUREJESHA HADHI ya walimu. Reviewed by Zero Degree on 1/12/2016 12:11:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.