Loading...

Maofisa watendaji wadaiwa kutia dosari agizo la Magufuli.


Rais John Magufuli

Tanga. Baadhi ya maofisa watendaji wa kata wanadaiwa kutia dosari uandikishaji wanafunzi wa darasa la kwanza kwa kuwatoza fedha wazazi ili wawakabidhi barua za uthibitisho wa ukazi.

Maofisa hao na wenyeviti wa Serikali za Mitaa, wanadaiwa kuwatoza wazazi hao kati ya Sh3,000 na 5,000 bila kuwapatia stakabadhi walipokwenda ofisini kwao kuchukua barua hizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walidai kitendo hicho kimewashtua kwa sababu Serikali iliwatangazia kuwa hawapaswi kutoa mchango wa aina yoyote wala karo kama alivyoagiza Rais John Magufuli.

Mzazi, Aisha Rajabu, mkazi wa Chumbageni jijini Tanga, alisema shuleni hawadaiwi fedha ya aina yoyote, lakini wanashangaa walipoambiwa wakachukue barua za uthibitisho wa ukazi ofisi za Serikali za Mitaa, ofisa mtendaji kutakiwa walipe Sh3,000.

“Huku shuleni kwa kweli tunashukuru tumepokewa vizuri na walimu na sijatoa hela yoyote, lakini kule kwa mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa nimeambiwa nilipe, halafu hawajanipatia risiti,” alisema Lilian Julius aliyekuwa akimuandikisha mwanaye kuanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Changa.

Maofisa watendaji hao katika maeneo mengine wanadaiwa kuwatoza wazazi Sh5,000 kwa ajili ya kugongewa muhuri kwenye fomu za uthibitisho pamoja na saini ya mtendaji.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdullah Lutavi, alisema utaratibu huo hautambuliki na kwamba hajapata malalamiko ya aina hiyo kutoka kwa wazazi hao.

Hata hivyo, aliahid kufuatilia na kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari. “Lazima watambue kuwa Rais aliposema elimu bure alimaanisha ni bure kweli, sasa kama kuna watu wanawatoza fedha tena wazazi kwa ajili yakukamilisha utaratibu wa kuwasajili nitahakikisha nawashughulikia,” alisisitiza Lutavi.


Source: Mwananchi
Maofisa watendaji wadaiwa kutia dosari agizo la Magufuli. Maofisa watendaji wadaiwa kutia dosari agizo la Magufuli. Reviewed by Zero Degree on 1/12/2016 12:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.