Ndalichako, Necta Walivyojadili viwango vya ufaulu.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
Kilichozusha mgogoro ni mabadiliko yaliyofanywa na Necta kwenye mifumo ya mitihani kuanzia namna ya kutoa matokeo, kutahini watu binafsi na utoaji wa vyeti vipya kwa waliopoteza.
Mwaka 2014 Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kupitia kwa Katibu Mtendaji wake, Dk Charles Msonde lilitangaza kubadili mfumo wa kupanga madaraja ya matokeo ya kidato cha nne na sita, kutoka jumla ya pointi; zinazounda daraja (divisheni) kwenda Wastani wa Pointi (GPA).
Wadau wa sekta ya elimu walipinga mabadiliko hayo kwa maelezo kuwa sababu zilizotolewa na Necta hazikuwa na mashiko.
Tangu wakati huo mpaka sasa Dk Msonde anaeleza kuwa mabadiliko hayo yalitokana na mahitaji ya kisera ya uendeshaji wa Serikali kwa mfumo wa mtandao ambao unaelekeza mifumo yote ya kompyuta ya taasisi mbalimbali ibadilike.
Wimbi la malalamiko limemfanya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako aliyewahi kuwa katibu mtendaji wa baraza hilo kwa miaka tisa, kutembelea ofisi za baraza hilo kuzungumza na wafanyakazi na menejimenti kuhusu sababu za mabadiliko hayo.
“Hakikisheni mnakuwa na misingi mizuri ya kimaamuzi na msikubali kufanya maamuzi yasiyo na tija kwa taifa letu,” anasema Profesa Ndalichako.
Anaongeza: “Tunawapa wiki moja mtupe maelezo. Tunataka kujua ninyi kama baraza mliona sababu gani za msingi kubadili huu mfumo, faida zake na mliwashirikisha watu gani. Kazi ya kuhakikisha utendaji wa taasisi zetu unakuwa mzuri ndiyo imeanza.”
Katika ziara hiyo, Ndalichako aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarishi na manaibu katibu wakuu, Profesa Simon Msanjila na Dk Leonard Akwilapo.
Sababu za kwenda GPA
Dk Msonde anasema mabadiliko hayo yalifanyika ili kuendana na mfumo wa udahili wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
“Watahiniwa wetu ambao wanaomba kutahiniwa kwenye vyuo vikuu na vile vya Nacte (Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi) hawalazimiki tena kupeleka vyeti vyao ili kudahiliwa,” anasema na kuongeza:
“Hivi sasa unaomba tu hata kwa simu na mifumo inaongea yenyewe. Wakati tunatumia jumla ya pointi tulisema A ni moja, vyuo vikuu vinasema A ni tano. Unaona inachanganya na kulitakiwa kuwe na uwiano.”
Anasema GPA haijabadilisha chochote kwenye alama za ufaulu wa madaraja; I, II, III na IV na kwamba kilichofanyika ni kufuta wastani wa pointi tu, mfumo huo unaeleweka zaidi kuliko ule wa zamani ambao ulikuwa ukichanganya wazazi.
Profesa Msanjila anafafanua kuwa: “Mfumo wa udahili unangalia taaluma si GPA. Mtu kama anakwenda kusoma taaluma fulani wanatizama masomo aliyosoma tu. Kama anakwenda kusoma sayansi watatizama masomo ya sayansi aliyosoma.”
Dk Msonde anasema: “Mfumo huu unaleta faida kwa wanafunzi kuelewa kwa ngazi zote, pia unasaidia kurahisisha udahili wa vyuo vikuu. Waziri nimekupa hicho kitabu ukienda kukisoma utakuta maelezo yote kuhusu mabadiliko hayo kwani hakuna siri. Sisi tulipewa maagizo na wizara ya elimu kufanya mabadiliko haya.”
Anasema katika kitabu hicho chenye kurasa zaidi ya 100 kuna maelezo ya waziri na katibu mkuu ikiwataka kutekeleza mabadiliko hayo, walichokifanya Necta ni utekelezaji tu.
Wakati mabadiliko hayo yakifanyika Ndalichako alikuwa ameondoka katika baraza hilo na katika mkutano huo profesa huyo anatoa mfano jinsi alivyokataa kwa barua kuanzisha mtihani wa maendeleo kwa wanafunzi wanaorudia mtihani wa taifa wa sekondari.
Watahiniwa binafsi
Baada ya sakata la kubadili viwango vya ufaulu kufungwa kwa Necta kutakiwa kutoa maelezo ndani ya siku saba, Profesa Ndalichako alitaka kupata ufafanuzi wa mtihani wa maendeleo.
“Wanafunzi binafsi huonekana tu pale wanapotaka kufanya mtihani, sasa kuna ulazima gani wa kuwapima kwa mtihani wa maendeleo kabla ya kufanya mtihani wao wa mwisho?” anahoji Waziri huyo.
Anasema mtihani huo ulianzishwa kwa azimio la Musoma kati ya mwaka 1940 na 1950 lililotaka badala ya kumpima mwanafunzi aliyesoma kwa miaka saba ama minne kwa mtihani wa siku moja, ni vyema kukawa na mitihani hiyo ya katikati ambayo alama zake zitajumuishwa na ule wa taifa.
“Hebu tuelezeni kitaalamu mnapokuwa mnatunga hii mitihani ni msingi gani mnatumia kusema huu ni CA na huu ni mtihani,” anaendelea kuhoji Profesa Ndalichako.
Akijibu suala hilo, Dk Msonde anasema: “Wizara ndiyo ilielekeza mabadiliko haya. Imeeleza kuwa watahiniwa binafsi wanafeli kwa sababu wanatahiniwa kwa mtihani mmoja tofauti na watahiniwa wa shule ambao wana alama za CA.”
Anasema ndiyo maana ikaanzishwa mtihani wa pili kwa watahiniwa binafsi ambao somo moja wanafanya mitihani miwili, ule wa CA na mwingine mtihani wa mwisho.
“Necta ndiyo wana watalaam wanaotakiwa kufikiri na kuishauri wizara. CA ni upimaji endelevu haiwezekani kumpa mtahiniwa binafsi mtihani huu wakati anaonekana siku ya mwisho ya mtihani wa mwisho,” anasema Profesa Ndalichako.
Anasema kama baraza hilo likitoa sababu zisizokuwa na msingi, kuanzia mwaka huu watahiniwa binafsi hawatafanya mtihani wa CA.
“Fanyeni uamuzi kwa kuzingatia weledi na taaluma si kufuata shinikizo,” anasisitiza.
Kuhusu utaratibu mpya ulioanzishwa na baraza hilo kutoa vyeti mbadala kwa waliopoteza vyeti halisi, Profesa Ndalichako anasema: “Huu ni utaratibu mzuri kwa sababu wapo ambao nyumba zao huungua moto, kusombwa na mafuriko na kupoteza vyeti vyao. Ila katika utoaji huu wa vyeti mbadala lazima muwe makini ili kuepusha udanganyifu. Zingatieni sana picha za wahusika na mchunguze vitu vingi.”
Mpango wa kuwanyoosha walimu
Profesa Ndalichako pia alilitaka baraza hilo kuweka utaratibu wa kuwasilisha majibu ya mitihani ya wanafunzi wote ili wizara iyachambue na kubaini tatizo ni nini.
“Haiwezekani mwanafunzi ashindwe kujibu chochote katika mtihani na kuandika namba yake ya mtihani tu. Tunataka kupitia majibu yao yatatusaidia kujua ubora wa walimu wanaowafundisha,” anasema na kuongeza:
“Katika majibu hayo tunaweza kubaini kasoro za ufundishaji wa walimu kama kwa Hisabati hata Kiingereza. Nimewahi kupitia matokeo ya mtihani wa darasa la saba na kubaini kasoro kubwa ya wanafunzi kujibu hesabu za sehemu za kujumlisha,” anasema Profesa Ndalichako.
Source: Mwananchi
Ndalichako, Necta Walivyojadili viwango vya ufaulu.
Reviewed by Zero Degree
on
1/12/2016 11:22:00 AM
Rating: