Loading...

REA yazidi kuhamasisha Nishati Safi, yatoa Bilioni 4.37 kwa Jeshi la Kujenga Taifa


📌JKT yaipongeza REA utekelezaji wa miradi ya nishati safi

📌REA yaiwezesha JKT asilimia 76 ya miradi ya nishati safi

📌Watumishi 7,000 wa JKT kupatiwa Mtungi wa kilo 15 wa LPG pamoja na Jiko lake la sahani mbili kila mmoja

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 – 2034).

Hayo yamebainishwa leo Agosti 11, 2025 na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Kanali Juma Mrai wakati akifungua mafunzo kwa washiriki toka vikosi 22 vinavyonufaika na mpango wa nishati safi JKT katika bwalo la vijana 834KJ (Makutupora) jijini Dodoma.

"Hii yote ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 zihame kutoka katika matumizi ya nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia, " Ameongeza Kanali Mrai.

Aidha, ameipongeza REA kwa kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya nishati safi ili kutunza mazingira na kuepuka athari za kiafya zinazohusiana na utegemezi mkubwa wa nishati isiyo kuwa safi.

"REA imeiwezesha JKT kwa asilimia 76 Sawa na Shilingi Bilioni 4.37 ya utekelezaji wa nishati safi katika kambi 22 za JKT kwa kuzipatia mashine za kutengeneza mkaa Mbadala 60, majiko banifu 291, mifumo ya gesi ya LPG 180 na masufuria yake, Mkaa Mbadala tani 220, mafunzo kwa vijana 50,000 pamoja na mifumo ya Gesi Vunde 9." Amesisitiza Kanali Mrai.

Katika hatua nyingine, amewataka watendaji waliolengwa kutumia mashine za kutengeneza mkaa mbadala, majiko banifu na majiko ya gesi pamoja na mkaa rafiki wa mazingira unaotokana na mabaki ya mazao ya shambani kupatiwa elimu ili kuwa na uwezo wa kubaini na kutatua changamoto za nishati hiyo na hatimaye bidhaa hizo kuleta tija kwa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mha. Advera Mwijage amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo maafisa na askari wa vikosi vilivyopo katika mpango wa REA ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye maeneo yao ya kazi.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatachangia katika mlolongo mzima wa kuwa na matumizi endelevu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa sababu mafunzo haya yanatoa fursa ya kupata ujuzi utaowawezesha Kusimamia mifumo ya Nishati safi vizuri.

Aidha Amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa kwa utekelezaji mzuri wa mradi na kuahidi ushirikiano katika kuhakikisha tunakamilisha mradi huu kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mha. Mwijage amebainisha kuwa, tayari REA imeidhinisha zaidi ya milioni 800 kwa ajili ya watumishi 7,000 wa JKT kupatiwa Mtungi wa kilo 15 wa LPG pamoja na Jiko lake la sahani mbili kila mmoja ikiwa ni sehemu wa kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya Kupikia kwa mtu mmoja mmoja.









REA yazidi kuhamasisha Nishati Safi, yatoa Bilioni 4.37 kwa Jeshi la Kujenga Taifa REA yazidi kuhamasisha Nishati Safi, yatoa Bilioni 4.37 kwa Jeshi la Kujenga Taifa Reviewed by Zero Degree on 8/11/2025 05:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.