Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), amefariki dunia baada ya kuzidiwa na maji wakati akifanya mazoezi ya kuogelea ufukweni.
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Suleiman Said ‘Yeltsin’ amefariki dunia baada ya kuzidiwa na maji wakati akifanya mazoezi ya kuogelea kwenye ufukwe wa Tanganyika Ferry uliopo jijini Dar es Salaam.
Suleiman, aliyepewa jina la utani Yelstin na wanachama wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam alipokuwa katibu mkuu wa muda mwishoni mwa miaka ya 90 akifananishwa aliyekuwa Rais wa Urusi, Boris Yeltsin kutokana na msimamo wake, alifariki dunia jana na mwili wake kuzikwa katika makaburi ya Kisutu jijini.
Msemaji wa familia hiyo, Seleman Said alisema ilikuwa kawaida kwa Yeltsin kwenda kufanya mazoezi ya kuogelea kwenye ufukwe huo kila siku asubuhi ingawa jana kwa muda huo, kabla ya kuondoka, alimwambia mke wake kuwa alikuwa anajisikia vibaya licha ya kwamba alikuwa hasikii maumivu sehemu yoyote ya mwili wake.
“Ilikuwa kawaida yake kwenda ufukweni kila siku asubuhi. Leo (jana) wakati anaogelea alikuwa na wenzake, lakini yeye alikwenda umbali mrefu. Wakati wa kurudi alizidiwa na maji na kila alipojaribu kujiokoa alishindwa. Hivyo aliokwenda nao walijaribu kumvuta lakini walishindwa kwani tayari alikuwa mzito sana kutokana na kunywa maji mengi,” alisema Said.
“Wenzake walilazimika kuwaomba watu wa mitumbwi ile midogo maarufu kama ngalawa ndiyo walitoa msaada wa kumwokoa kwani tayari misuli iliishiwa nguvu. Alifia njiani wakati akipelekwa Hospitali ya Aga Khan, kwani maji aliyokunywa yalikuwa mengi,” alieleza Said.
Mwenyekiti wa bodi ya TAA, Profesa Joseph Msambichaka alimuelezea marehemu kuwa alikuwa mchapakazi enzi za uhai wake, aliyesikiliza matatizo ya wafanyakazi pasipo kubagua wala kupendelea.
“Hili ni pigo kwetu kumpoteza kiongozi mchapakazi. Mhandisi Yeltsin hakubagua mtu katika kutekeleza majukumu yake, alimsikiliza kila mmoja kwa nafasi yake. Hivyo, hili ni pigo kubwa kwetu,” alisema Profesa Msambichaka.
ZeroDegree.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), amefariki dunia baada ya kuzidiwa na maji wakati akifanya mazoezi ya kuogelea ufukweni.
Reviewed by Zero Degree
on
1/19/2016 12:48:00 PM
Rating: