Mgombea wa CHADEMA ASHINDA UDIWANI akiwa gerezani.
Sumbawanga. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulikuwa na vionjo vyake, ulivutia wengi na ulikuwa hautabiriki. Haikuwa rahisi kujua nani atakuwa mshindi katika kiti cha urais hata katika majimbo ya ubunge na udiwani.
Kauli mbinu ya ‘Mabadiliko’ ilitumika kuwateka wapigakura, aliyekuwa mgombea wa Chadema katika urais, Edward Lowassa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ndiyo viliitumia kusisitiza muda wa kufanya mabadiliko umewadia. Upande mwingine mgombea wa CCM ambaye sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli akaiiteka na kutafsiri ya M4C ya Chadema kwamba ni ‘Magufuli for Change’.
Vumbi la kampeni halikuwa la kawaida kati ya wagombea hao wawili waliokuwa wakichuana vikali kwa kuwa walikuwa na mvuto wa aina yake na sera za kipekee.
Yote tisa, kumi uchaguzi huo ulikuwa na vioja vyake kwa wakazi wa Kata ya Lusaka iliyopo Tarafa ya Laela wilayani Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa wakaandika historia ya kipekee kwa kumchagua mgombea aliyekuwa akitumikia kifungo gerezani ili awe diwani wao.
Aliyechaguliwa akiwa gerezani ni Ameri Nkulu (56), mkazi wa Kijiji cha Kizumbi, aliyekuwa mgombea wa udiwani kupitia tiketi ya Chadema, akiibwaga CCM na vyama vyingine.
Alivyohukumiwa
Oktoba 23, mwaka 2015, Nkulu alihukumiwa kwenda jela kwa miezi sita, ikiwa ni siku mbili kabla ya wananchi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Nkulu alipatikana hatia katika shitaka la kupigana na kiongozi wa CCM kwenye kata hiyo, Christian Kafwimbi baada ya kufunguliwa kesi namba 33/2015.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, Rozari Mugissa ndiye aliyemuhukumu Nkulu na mwenzake kwa kutumia kifungu cha adhabu cha 87, sura ya 16 ya Makosa ya Jinai, baada ya kuwakuta na hatia ya kupiga na kupigana hadharani.
Hata hivyo, hukumu hiyo iliyomtupa gerezani Nkulu, haikuzuia wakazi wa kata yake kumchagua kuwa diwani wa Lusaka bali walimpa ushindi kwa kura zao wakiamini akimaliza kutumikia kifungo atatoka na kuendelea kupigania maendeleo endelevu ya kata yao.
Mwanasheria kutoka Kampuni ya S. Mawalla Law Consultants, Mathias Budodi anaeleza kwamba kwa kosa la aina hiyo, sheria imetoa mbadala katika hukumu kwa mshitakiwa kutakiwa kulipa faini ya Sh 500 au kifungo cha chini ya mwaka mmoja.
Anasema kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi 2015, mtu akihukumiwa kifungo chini ya mwaka mmoja, hawezi kupoteza sifa za kuwa kiongozi wa wananchi, hivyo ndiyo sababu Nkulu ameweza kupata udiwani licha ya kuhukumiwa kwenda jela.
Akata rufaa na kuachiwa
Diwani huyo wa Kata ya Lusaka, anayetajwa kuwa mwanasiasa mkongwe asiyekubali kushindwa, aliachiwa huru Desemba 16, mwaka jana, siku 54 tangu alipohukuma kifungo na kukaa gerezani.
Akiwakilishwa na mwanasheria wa kujitegemea, Bartazari Chambi, Nkulu alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, ambako aliwasilisha hoja tatu za kukata rufaa.
Hoja yake ya kwanza ilikuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya Sumbawanga iliyomtia hatiani haikuthibitisha pasipo kuacha shaka kwamba walipigana na mwenzake hadharani, hoja ambayo Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga iliona haina mashiko.
Hoja nyingine ni kwamba mahakama ilikosea kumhukumu kifungo cha miezi sita jela, ambacho kwa kosa la aina yake ni adhabu ya juu wakati yeye alitenda kosa hilo kwa mara kwanza.
Hata hivyo, kabla kukata rufaa, Mahakama Kuu iliitisha jalada la kesi hiyo ili kujiridhisha iwapo mahakama ya chini yake ya Hakimu Mkazi ngazi ya Wilaya ya Sumbawanga kama ilitenda haki katika kutoa hukumu hiyo.
Hoja yake ya tatu alidai mahakama haikupa mbadala katika kutoa hukumu kwa kosa la aina hiyo, sheria inaelekeza hukumu ya kulipa faini ya Sh 500 au kifungo cha chini ya mwaka mmoja.
Hata hivyo, katika shauri hilo ambalo upande wa Serikali iliwakilishwa na Mwanasheria Njoloyota Mwashubila, mahakama ya juu iliona adhabu aliyopewa mshtakiwa huyo ilikuwa kubwa kuliko kosa na kwa kuzingatia kuwa hilo ni kosa la kwanza kwa mkosaji.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Kakusuro Sambo anaeleza kwamba kwa kuzingatia mazingira ya kosa na tukio, mahakama imempunguzia adhabu kutoka kifungo cha miezi sita jela hadi mwezi mmoja na siku 24, adhabu ambayo ilikwisha Desemba 16 mwaka jana.
Kwa mantiki hiyo sasa, Nkulu alikaa gerezani siku 54, badala ya miezi sita kama ambavyo iliamriwa awali na baada ya kutoka gerezani, aliapishwa na kuendelea na shughuli za kuwatumikia wananchi kwa nafasi yake ya udiwani.
Ndugu, viongozi, wananchi wamzungumzia
Mtoto wa kwanza wa Nkulu, Elizabeth Ameir Nkulu aliyezungumza kwa niaba ya familia anasema hukumu kwa baba yao iliwaathiri kisaikolojia kwani hawakutegemea kwamba ipo siku angeweza kufungwa jela.
“Mzee alikuwa kiungo katika familia ilituumiza sana, sasa tuna amani na furaha tele. Shukrani zetu ziende kwa wale wote waliofanikisha kwa namna moja au nyingine mzee wetu kutoka gerezani,” anasema.
Mbunge wa Jimbo la Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka anasema Nkulu kuchaguliwa kuwa diwani akiwa gerezani ulikuwa mpango wa Mungu na kielelezo kwamba haki ya mtu hainyang’anywi.
Mbunge huyo anawataka wakazi wa kata hiyo kuweka itikadi za kisiasa kando na kumuunga mkono Nkulu kwenye harakati zake za kuiletea maendeleo kata yao ili iwe ya mfano wa kuigwa.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Mkoa wa Rukwa, Aida Khenan anasema kitendo cha wananchi kuchagua Nkulu akiwa gerezani inaonyesha namna walivyo na imani naye, hivyo ni wajibu wake akiwa kiongozi wa wao kuhakikisha anamaliza kero zao kwenye afya, maji na elimu.
Mkazi wa Kijiji cha Kizumbi, Kenta Said anasema alifanya uamuzi kumchagua diwani huyo kwa kuwa katika miaka ya nyuma aliweza kuwasaidia kutatua kero mbalimbali zinazowakabili aliposhika nafasi hiyo.
Anataja matatizo yaliyowaandama ni pamoja na ukosefu wa maji, dawa kwenye zahanati na vituo vya afya hivyo wamemchagua ili akashughulikie matatizo hayo.
Mkazi wa Kata ya Lusaka, Jephari Minazi anasema diwani Nkulu ni kielelezo cha wapambanaji na wapenda maendeleo, wasiokubali kudhulumiwa haki zao akiwa mstari mbele pia kudai haki za wanyonge ndiyo sababu wanachi walichagua akiwa gerezani.
“Kumchagua Nkulu tulikuwa sahihi kwani ndiye mtu anayeweza kutatua kero zetu kwenye kata yetu ya Lusaka ambayo ina changamoto mbalimbali zikiwamo za afya, elimu na maji,” anasema.
Nkulu alonga
Alipotakiwa kueleza anavyojisikia baada ya kutoka gerezani akiwa diwani, Nkulu anasema: “Najisikia mwenye furaha na amani moyoni baada ya kushinda rufaa yangu, lakini kilichonifurahisha zaidi ni namna wananchi wa kata yangu walivyokuwa na imani nami hata kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kunichagua wakati natumikia kifungo gerezani.”
Anaongeza kwa kusema kuwa: “Wananchi wameonyesha upendo kwangu. Nina deni kubwa kwao la kuhakikisha kata inapata maendeleo endelevu na ni wajibu wangu kuhakikisha nalipa deni.”
Anasema kuchaguliwa kwake akiwa gerezani pia ni fundisho katika jamii kwamba haki itabaki kwa mwenye haki.
“Sijui kama yupo diwani au kiongozi mwingine nchini aliyechaguliwa akiwa gerezani kama ilivyokuwa kwa mimi; kama hayupo basi miye ni mfano wa kuigwa na somo kwa watawala,” anasema Nkulu. Hata hivyo, Nkulu hakuwa tayari kuzungumzia maisha ya gerezani yalivyo huku akisisitiza hawezi kukubali kuona mwananchi kwenye kata yake anafungwa jela, bali atahakikisha anasimamia haki inatendeka kwa wananchi wake wote.
Source: Mwananchi
Mgombea wa CHADEMA ASHINDA UDIWANI akiwa gerezani.
Reviewed by Zero Degree
on
1/13/2016 12:55:00 PM
Rating: