Loading...

Polisi wadaiwa ‘kumlinda’ raia wa China anayedaiwa kuwatishia amani wananchi.


Kamanda Polisi Mkoa Kilimanjaro, Ramadhan Mungi

Moshi. Polisi wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro, wanadaiwa kumlinda raia wa China, anayetuhumiwa kufyatua risasi kiholela na kuwatisha wananchi.

Hata hivyo, Kamanda Polisi Mkoa Kilimanjaro, Ramadhan Mungi alisema jana kuwa, hana taarifa ya tukio hilo lililotokea Julai mwaka jana lakini atalifuatilia.

“Kila mtu anatakiwa kuheshimu sheria za nchi awe ni mgeni au Mtanzania, matumizi ya silaha yana masharti yake ambayo ni lazima yaheshimiwe. Nitafuatilia jambo hili,” alisema.

Mlalamikaji katika tukio hilo, Ally Ng’anzo ambaye ni mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya Mega Copper alisema alishatoa maelezo yao polisi.

“Siku hiyo nilipigiwa simu na wafanyakazi na wananchi wanaoishi jirani na Mchina aliyefyetua risasi kwenye mgodi wangu. Nilikwenda lakini namshukuru nilikuta hakuna aliyejeruhiwa,” alisema Ng’anzo.

Alifafanua kuwa wafanyakazi walimweleza kuwa raia huyo alifyatua risasi tatu, mbili alizielekeza kwenye njia ya mgodi na nyingine alifyatua hewani na hawakujua sababu.

Hata hivyo, alisema baada ya kufungua jalada hilo, yeye na mashahidi waliandikisha maelezo yao lakini hadi sasa wanasubiri kuitwa mahakamani kutoa ushahidi.

Diwani wa Kata ya Shighatini, Enea Mrutu alisema raia huyo hana uhusiano mzuri na majirani zake lakini wanashangaa polisi kutochukua hatua dhidi yake.

“Hivi tujiulize kuna Mtanzania anaweza kwenda China akapewa kibali cha kumiliki silaha. Tuseme amepewa, anaweza kutisha watu kiasi hiki?” alihoji Mrutu.

Diwani huyo aliwataka polisi kukamilisha haraka uchunguzi wake akisema ushahidi dhidi ya Mchina huyo ulikuwa dhahiri lakini hajashtakiwa.


ZeroDegree.
Polisi wadaiwa ‘kumlinda’ raia wa China anayedaiwa kuwatishia amani wananchi. Polisi wadaiwa ‘kumlinda’ raia wa China anayedaiwa kuwatishia amani wananchi. Reviewed by Zero Degree on 1/20/2016 08:03:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.