Radi kubwa yapiga tena na kusababisha vifo vya watu wawili wakiwa shambani.
Mpanda. Wakazi wawili wa Kijiji cha Ilebula, Tarafa ya Kabungu wilayani Mpanda, wamekufa papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa kwa kupigwa na radi chini ya mti wakati mvua zikinyesha.
Waliofariki dunia katika tukio hilo lililotokea juzi saa 10 jioni ni Lupimwa Julius (30) na Remi Madirisha (32).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari aliwataja majeruhi kuwa ni Tatu Gerald, Stellah John na Filbert Pascal wakazi wa kijiji hicho.
Alisema wakazi hao wakiwa shambani ghafla mvua zilianza kunyesha zikiwa zimeambatana na kimbunga na radi.
Alisema wakazi hao walikwenda kujikinga chini ya mti uliokuwa katika eneo hili.
Kidavashari alisema wakiwa chini ya mti huo, walipigwa na radi na kusababisha vifo vya wawili papo hapo na kujeruhi wengine.
Alisema majeruhi hao walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa matibabu.
Aliwahadharisha wananchi kuwa makini katika kipindi hiki cha mvua za masika kwa kujihifadhi katika maeneo yasiyo na miti mibichi na ambayo hayawezi kusababisha madhara radi inapopiga.
Tukio kubwa la vifo vilivyotokana na kupigwa radi nchini lilitokea Feburuari 24, mwaka jana mkoani Kigoma na kuua watu wanane.
Watu hao wakiwamo wanafunzi sita, mwalimu wa Shule ya Msingi Kibirizi na mtu wa kawaida mkazi wa Bangwe mjini humo, walikufa kwa kupigwa na radi.
Katika tukio hilo watu hao walikufa papo hapo, huku wanafunzi 15 wakijeruhiwa na radi hiyo iliyoambatana na mvua kubwa zilizonyesha. Mikoa ya Kigoma na Katavi hukumbwa na matukio ya vifo vya watu na mifugo vinavyotokana radi.
ZeroDegree.
Radi kubwa yapiga tena na kusababisha vifo vya watu wawili wakiwa shambani.
Reviewed by Zero Degree
on
1/22/2016 11:15:00 AM
Rating: