Sakata la Zanzibar sasa kuhamia bungeni.
Maalim Seif
Dodoma. Wakati mazungumzo ya kujadili mkwamo wa kisiasa Zanzibar kati ya CCM na CUF yakionekana kukwama, suala hilo sasa litahamishiwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge na vyama vinavyounda Ukawa, Mwananchi limeelezwa.
Pia, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa watakuwapo mjini Dodoma kukutana na wabunge wa Ukawa ili kuweka mkakati wa suala hilo.
Jana alasiri, wabunge wa Ukawa walikutana katika kikao cha ndani kilichofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa uliopo bungeni mjini Dodoma, kujadili njia watakazotumia kuwasilisha suala hilo. Hata hivyo, waligoma kuweka bayana njia hizo wakisema zikijulikana ‘zitaundiwa mkakati’ wa kuwakwamisha.
“Tunakwenda kulianzisha upya suala la Zanzibar ni lazima jipu litumbuliwe. Hatusemi tutaliwasilisha kwa hoja au kanuni ipi maana tukisema watajiandaa. Tumedhamiria hivyo lazima watu watambue, palipo na msuguano pana mwendo,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Manyika muda mfupi kabla ya kuingia katika kikao hicho.
Kikao hicho kilifanyika ikiwa zimepita siku mbili tangu Maalim Seif kukutana na viongozi wakuu wa Ukawa jijini Dar es Salaam, kujadiliana nini cha kufanya baada ya mazungumzo yao na CCM Zanzibar kuonekana kukwama.
Hata hivyo, kikao hicho hakikuwa na makubaliano rasmi.
Katika kuhakikisha makubaliano na juu ya nini kifanyike yanaafikiwa, jana wabunge wa Ukawa wa vyama vya CUF, na Chadema walikutana.
Mkwamo huo wa kisiasa uliibuka baada ya baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kufuta matokeo Oktoba 28 mwaka jana na kuahidi kuitisha uchaguzi mwingine ndani ya siku 90, kitendo ambacho kilipingwa na CUF ikisema hakikubali.
Tangu wakati huo, Maalim Seif, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na marais wa zamani wa Zanzibar, Dk Salmin Amour, Ali Hassan Mwinyi na Amani Karume wamekuwa kwenye mazungumzo ambayo yanaonekana kukosa muafaka.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya alisema jana kuwa: “Kwanza tumejipanga kutafuta nafasi ya kuliingiza suala la Zanzibar bungeni. Awali, hatukupenda kulizungumzia kwa sababu tuliamini vikao vya mashauriano (vya CUF na CCM) vingezaa matunda.”
“Kama unavyoona mazungumzo hayo hayajazaa matunda. Sasa tunaingia kama CUF na kama Ukawa ili kuweka nguvu. Tutakutana kwanza kama Ukawa kupanga suala hilo tutaliwasilisha bungeni kwa staili gani.”
Hivi karibuni Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa bajeti ya uchaguzi wa marudiano visiwani humo imeshapatikana na kinachosubiriwa ni ZEC kupanga siku ya uchaguzi.
Rais John Magufuli ameshakutana na pande zote kwenye mgogoro huo, akianza na Maalim Seif na baadaye Dk Shein ambaye ameeleza wazi kuwa msimamo wa kurudia uchaguzi wa Zanzibar ni wa chama chake, CCM na hivyo kuwataka wafuasi wasubiri tarehe.
ZeroDegree.
Sakata la Zanzibar sasa kuhamia bungeni.
Reviewed by Zero Degree
on
1/21/2016 11:25:00 AM
Rating: