Loading...

Umeya Kinondoni kama sinema vile.


Madiwani wateule wa CCM wakijadiliana nje ya Ukumbi wa Manispa ya Kinondoni, Dar es Salaam jana, baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu kuzuia uchaguzi wa Meya.


Dar es Salaam. Wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikizuia uchaguzi wa mameya wa manispaa za Ilala na Kinondoni uliokuwa ufanyike jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, George Simbachawene amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki kuhakikisha unafanyika kabla ya Januari 16.

Juzi, Mahakama Kuu ilitupilia mbali ombi la Diwani wa Vijibweni (Chadema), Isaya Charles kutaka itoe amri ya muda ya kuzuia uchaguzi huo, lakini baadaye Mahakama ya Kisutu ilitoa zuio la uchaguzi huo kutokana na maombi yaliyowasilishwa na mkazi wa Kinondoni, Elias Nawera.

Jana, Simbachawene aliwaambia waandishi wa habari baada ya kukutana na Sadiki na viongozi wengine, akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na wa Ilala, Raymond Mushi kuwa kwa mujibu wa sheria, haiwezezekani mbunge wa kuchaguliwa au wa viti maalumu kupiga kura nje ya halmashauri ya wilaya aliyokuwapo wakati akipendekezwa na chama chake kugombea wadhifa huo.

“Napenda kuvitaka vyama vya siasa kuheshimu sheria zilizopo ili kujenga, kukuza na kudumisha demokrasia lakini pia kuondoa na kuepusha migogoro na mivutano isiyokuwa na lazima,” alisema Simbachawene.

Kauli yake imekuja baada ya vyama vya CCM na Chadema kuingiza wabunge kutoka Zanzibar kwenye vikao vya mabaraza ya madiwani ambavyo vinatakiwa kuchagua mameya. Chadema waliingiza wabunge hao jana, ikiwa ni kuiigiza CCM iliyokuwa imepeleka wabunge kutoka Zanzibar tangu mwanzoni mwa vikao hivyo na kusababisha mtafaruku uliotinga mahakamani.

Katika ombi lake, diwani huyo wa Vijibweni alitaka liwekwe zuio la muda ili kusubiri usikilizwaji wa uamuzi wa kesi yake ya kikatiba aliyoifungua katika mahakama hiyo ya kupinga wabunge wa viti maalumu CCM kutoka Zanzibar, kushiriki katika uchaguzi huo ulioshindikana kufanyika Desemba 10, mwaka jana.

Mahakama Kuu ilitupilia mbali ombi hilo kwa maelezo kuwa mtoa maombi ni diwani kutoka manispaa nyingine (Temeke), hivyo hana haki ya kisheria kupinga uchaguzi wa meya katika halmashauri ambayo yeye si mjumbe wa baraza la madiwani.

Uchaguzi huo ulitakiwa ufanyike jana, lakini haukufanyika kutokana na zuio hilo la Mahakama ya Kisutu lililoonekana kuwachanganya madiwani wa CUF na Chadema waliofika jana saa mbili asubuhi kwenye ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni na Karimjee uliopo Manispaa ya Ilala, kuhoji sababu zilizotolewa na mahakama hiyo.

Aliyefungua kesi hiyo Mahakama ya Kisutu, Elias Nawera aliwashtaki wakurugenzi wa manispaa hizo mbili. “Mahakama Kuu ilikataa ombi letu kwa kuwa aliyefungua kesi ni diwani wa Temeke na alitaka uchaguzi katika manispaa ya Ilala na Kinondoni usitishwe,” alisema.

“Ila leo (jana) inafunguliwa kesi Kisutu na mkazi wa Kinondoni lakini mahakama inazuia mpaka uchaguzi wa Ilala. Hii si sawa,” alisema Boniface Jacob, diwani wa Ubungo na mgombea wa umeya wa Kinondoni.

Madiwani hao walionyesha kushangazwa na kitendo cha madiwani wa CCM kutoka Zanzibar pamoja na mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano kujitokeza kushiriki uchaguzi huo kwa madai kuwa ni wakazi wa manispaa husika.

Mawaziri hao ni Balozi Augustine Mahiga (Mambo ya Nje), Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu) na Dk Abdallah Possi (Naibu-Ofisi Waziri Mkuu).

Kusitishwa uchaguzi

Akizungumzia kusitishwa kwa uchaguzi huo muda mfupi baada ya kuwaeleza madiwani kuhusu uamuzi wa mahakama, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema: “Mahakama imeamua, mimi sina cha kufanya na hilo halina mjadala. Nikiruhusu uchaguzi nitabanwa mimi siyo wao (madiwani).”

Alipotakiwa kujibu madai ya madiwani wa CUF na Chadema kuwa zuio hilo lililenga uchaguzi tu, si kuapishwa kwa madiwani, alisema: “Hivyo vitu vinakwenda pamoja, ukishawaapisha ni lazima ufanye uchaguzi. Nimesikia wanasema wanaweza kujiapisha wenyewe. Hilo hawawezi kufanya maana kuna taratibu za kuapishwa na zinafanywa wa vyombo vilivyoruhusiwa. Pingamizi tumelipokea leo (jana) asubuhi.” Alisema kesi itasikilizwa Januari 13.

“Kama diwani wa Kinondoni angefungua kesi hiyo Mahakama Kuu ingesikilizwa. Hoja iliyopelekwa Kisutu ina nguvu kwa sababu imefunguliwa na mkazi wa Kinondoni.

“Binafsi nikipokea amri ya Mahakama siwezi kuipinga. Zuio hili nililipata jana (juzi) jioni wakati tayari nimeshatoa taarifa kwa madiwani kufika kwa ajili ya uchaguzi.”

Alisema alipokea barua ya zuio hilo saa 12 jioni akiwa ofisini.

Ukawa yaeleza ilivyojipanga

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alizituhumu mahakama kuwa zinatumika kisiasa.

“Jumatatu tutakwenda Kisutu tutaomba kuwa sehemu ya kesi maana tunaamini aliyefungua kesi hana mamlaka ya kisheria,” alisema.

Alisema kuna mwingiliano wa kisheria na kusisitiza kuwa dhana ya elimu bure haiwezi kutekelezeka katika manispaa hizo mbili kwa maelezo kuwa tangu Julai mwaka jana hakuna baraza la madiwani lililokutana licha ya moja ya kazi zake kuwa ni kuidhinisha matumizi ya fedha mbalimbali.

“Matumizi ya fedha yanayofanyika sasa ni kinyume na sheria,” alisema Kubenea.

Akifafanua zaidi kuhusu uchaguzi huo, diwani wa Kata ya Ubungo alisema baada ya CCM kuleta wajumbe kutoka Zanzibar katika uchaguzi wa kwanza ulioahirishwa, vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi navyo viliunda mkakati wa kuleta madiwani kutoka Zanzibar, kuwaingiza kwenye uchaguzi wa jana.

Alisema zuio hilo lilikuwapo na lisingetolewa kama CCM ingeonekana inashinda katika uchaguzio huo.

Alisema idadi ya madiwani wa kuchaguliwa, viti maalumu na wabunge ambao huhesabika katika kundi la madiwani, Chadema ina madiwani 29, CCM 15 na CUF 9.

“Katika uchaguzi ulioahirishwa kutokana na hoja za madiwani Wazanzibari, Chadema tulikuwa na madiwani 29, CCM wakaongeza madiwani kutoka Zanzibar nao wakawa 29 na CUF walikuwa 9. Bado tulikuwa tumewazidi na tungeshinda.”

“Leo (jana) Ukawa tumeleta madiwani kutoka Zanzibar na wamefikia 36, CCM wao wanao 31 na CUF 14. Kwa namba hiyo bado tumewazidi. Wakiamua tufuate taratibu za uchaguzi tutashinda na wakiamua tupindishe mambo na kuingiza Wazanzibari pia tutawashinda,” alisema Jacob.

Alisema baada ya kuonekana kuwa ujanja unataka kufanyika, wamemtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuhakikisha madiwani 67 waliofika kwenye uchaguzi wa kwanza ulioahirishwa kwa hoja za ‘madiwani wa Zanzibar’, ndiyo wanapiga kura katika uchaguzi mwingine utakaopangwa.

Ilivyokuwa Ilala

Zogo na kutupiana lawama kati ya madiwani wa CCM na wa vyama vinavyounda Ukawa liliibuka baada ya Mwanasheria wa Manispaa ya Ilala, Mashauri Musimu kusoma zuio la Mahakama Kisutu.

Musimu alipewa nafasi na mkurugenzi wa manispaa hiyo, Isaya Mngurumi kutoa mwongozo wa kisheria kuhusu hatua ya uchaguzi huo.

“Zuio hili limetolewa na hatukuwa na taarifa yoyote kuhusu kufunguliwa kwa shauri hili, lakini Januari 13 tunatakiwa kufika mahakamani hapo ili kujua msingi wa kesi hii. Hivyo amri hii ni halali hatuwezi kuijadili hapa,” alisema.

Baada ya kauli hiyo, Mbunge wa Ukonga (Chadema), Waitara Mwita alisimama na kutaka kuzungumza jambo, akazuiwa na wabunge wa CCM kabla ya kutulizwa na Mngurumi na kuwaeleza kuwa hoja zao wakazitoe mahakamani.

Hatua hiyo ya kuzuia mbunge huyo kuzungumza iliwakera madiwani wengine wa Ukawa ambao walisimama na kuanza kuimba “people’s power”.

Uchaguzi huo ulijumuisha wajumbe 66 wakiwamo madiwani, wabunge wa majimbo na viti maalumu.



Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Umeya Kinondoni kama sinema vile. Umeya Kinondoni kama sinema vile. Reviewed by Zero Degree on 1/10/2016 10:02:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.