Loading...

CUF, ACT walia na bomoabomoa.


Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Ofisa Harakati na Matukio wa chama hicho, Nurdin Msati.

Dar es Salaam. Vyama vya CUF na ACT-Wazalendo vimeijia juu Serikali kuhusu bomoabomoa na kutaka operesheni hiyo isitishwe nchi nzima kwa kuwa inakiuka misingi ya haki za binadamu.

Pia, vimeitaka Serikali kuangalia upya ugawaji wa viwanja vya Mapwepande kwa madai kuwa waliostahili kupewa walikosa, huku wajanja wachache wakipata.

Viongozi hao walitaka kuwajibishwa kwa watendaji wa Serikali walioruhusu ujenzi wa nyumba kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, wakati walikuwa na jukumu la kuzuia.

Bomoabomoa hiyo iliwakumba wananchi wanaoishi mabondeni, kwenye kingo za mito, maeneo ya wazi na fukwe za bahari na imekuwa ikilalamikiwa na wakazi wa maeneo hayo wakisema hawakupewa muda wa kujiandaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema Serikali inapaswa kuwajibika kwa madai kuwa ndiyo iliyochangia wananchi kujenga maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.

Sakaya alisema kazi ya maofisa ardhi na mipango miji ni kuhakikisha wananchi wanajenga sehemu zinazostahili kwa kuwa siyo Watanzania wote wanaofahamu taratibu na sheria.

Aliitaka Serikali ikubali kuwapatia misaada ya kibinadamu wote waliobomolewa nyumba na ambao hivi sasa wanahangaika kwa kukosa chakula, mavazi na mahali pa kuishi.

“Ukienda Mkwajuni na Jangwani utakuta familia zinaishi nje juu ya vifusi, pembezoni mwa maji machafu na chini ya vipande vya mabati na miti mchana kutwa, usiku kucha. Haya ni mazingira hatarishi yasiyostahili kwa wananchi,”alisema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo (Bara), Msafiri Mtemelwa alisema kuwa ugawaji wa viwanja vya Mabwepande uligubikwa na udanganyifu uliosababisha baadhi ya wananchi waliohamishwa mabondeni kukosa makazi.

“Serikali ifahamu kwamba miongoni mwa haki za binadamu za msingi ni pamoja na kupata sehemu sahihi ya kulala. Basi Serikali ihakikishe watu hawa wanapata maeneo haya tofauti na wanavyoishi sasa hivi,” alisema Mtemelwa.

Aliongeza kuwa hadi kufikia hatua za wananchi kubomolewa nyumba zao, kuna watu walikosa uzalendo kwa Taifa lao kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kuanzia ngazi mitaa hadi Taifa.

“Zoezi hili litakapoisha uwe mwanzo wa kuwawajibisha wale wote waliozembea kutekeleza majukumu yao hadi kufikia wananchi kujenga maeneo haya,” alisema Mtemelwa.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
CUF, ACT walia na bomoabomoa. CUF, ACT walia na bomoabomoa. Reviewed by Zero Degree on 1/10/2016 11:38:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.