Loading...

Wahariri kumshauri waziri kuhusu sheria za habari.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar, es Salaam jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa. 

Dar es Salaam. Wahariri wa vyombo vya habari nchini wameunda kamati ndogo ya watu sita kuandaa mapendekezo kuhusiana na muswada wa sheria ya vyombo vya habari na kuyawasilisha kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Muswada huo huenda ukawasilishwa katika mkutano wa Bunge uliopangwa kufanyika Februari mjini Dodoma.

Kamati hiyo iliundwa jana katika mkutano wa wahariri na Waziri wa Habari, Nape Nnauye uliofanyika Dar es Salaam na jukumu lake litakuwa kutoa mapendekezo juu ya mambo muhimu yanayohitajika kuhakikisha kunakuwa na uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Kamati hiyo itasikiliza kero mbalimbali za wadau wa habari na kukusanya maoni ili kuboresha utungaji wa sheria zinazohusu habari.

Kikao cha kwanza cha kamati hiyo kitafanyika Jumatano ijayo itakapokutana na watendaji wa wizara kabla ya kukutana na waziri.

Kamati hiyo itaongozwa na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile na katibu wake atakuwa Mhariri Mkuu wa kampuni ya The Guardian, Jesse Kwayu.

Wajumbe ni Mhariri Mkuu wa Clouds Media, Joyce Shebe, Naibu Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Serikali (TSN), Tuma Abdallah, Mhariri Mkuu wa Upendo Media, Nengida Johannes na Mhariri wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Prudence Constantine.

Akizungumza na wahariri hao, Nape alisema lengo la Serikali ni kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau badala ya ubabe.

Aliitaka kamati hiyo kukutana mapema na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu tasnia ya habari yakiwamo ya muswada wa huduma ya vyombo vya habari, ambao upo chini ya wizara yake.

“Katika Bunge la Februari, muswada huu utasomwa, ni muhimu kamati ikakutana haraka kukusanya maoni ya maboresho yawasilishwe mapema ili yafanyiwe utaratibu wa kuingizwa kabla haujaanza kusomwa. Haya mambo ya kisheria yanahitaji utaratibu maalumu hivyo yakipatikana mapema itakuwa vyema zaidi,” alisema Nape.

Kuhusu Muswada wa Sheria na Haki ya kupata Habari, Nape alisema huo upo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, hivyo akasema kuna uwezekano kamati hiyo ikafanya kazi na wizara zote katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

Awali, Balile alilalamikia sheria zilizopo ambazo zinatoa mamlaka kwa waziri mwenye dhamana kufungia vyombo vya habari badala ya kumchukulia hatua mhusika aliyepotosha umma, kwa kutoa taarifa zisizo sahihi.

Balile alitolea mfano daktari kwamba akikosea anaonywa na Baraza la Madaktari yeye binafsi huku hospitali ikiendelea kutoa huduma na kulipa wafanyakazi.

“Linapokuja suala la mwandishi mmoja amekosea, gazeti zima linafungiwa na kuwanyima haki wafanyakazi wa kampuni husika huku katika nyanja nyingine anawajibishwa aliyekosea,” alisema.

Nape alisema ataisimamia sheria ya vyombo vya habari kuhakikisha inaboreshwa kwa kuvishirikisha vyombo vyote.

“Serikali ipo tayari kuboresha pale ambako hapakuwa sawa, halitapitishwa jambo linalowahusu wanahabari bila kuwahusisha wenyewe na kukubaliana kwa hoja, upande wa Serikali ukishindwa ukubali jambo lisonge mbele na wa habari ukishindwa ukubali na kusonga mbele, ”alisema.

Kuhusu malalamiko ya waandishi ya kutolewa vitambulisho vya kazi kila mwaka, Nape alisema kuwa kufikia Alhamisi awe amepewa ripoti na watendaji wa Idara ya Habari (Maelezo) akisema amekuwa akisikia malalamiko kuhusu suala hilo tangu ameingia wizarani, hivyo anahitaji kulimaliza.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Wahariri kumshauri waziri kuhusu sheria za habari. Wahariri kumshauri waziri kuhusu sheria za habari. Reviewed by Zero Degree on 1/10/2016 11:48:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.