Loading...

USALAMA wa wateja wa benki shakani.

Wateja wakipata huduma kwenye moja ya matawi ya
Wateja wakipata huduma kwenye moja ya matawi ya benki.

Moshi. Hali ya taharuki imeanza kuwakumba wateja wa taasisi za fedha nchini, hasa benki kutokana na kuibuka kwa matukio ya wateja kuporwa wanapotoka kuchukua fedha.

Katika siku za karibuni kumekuwapo na matukio ya watu mbalimbali kuporwa fedha na watu wenye silaha, ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka benki, hali ambayo inajenga wasiwasi juu ya sehemu ambazo majambazi hao hupata taarifa za watu wanaokwenda benki kuchukua fedha.

Wateja wa benki mbalimbali wanatupia lawama uongozi wa benki kwa kufumbia macho matumizi ya simu za mikononi ndani ya benki, huku ikihisiwa baadhi yao ndio ambao hutoa siri kwa majambazi.

Hofu miongoni mwa wateja ilizidi zaidi baada ya majambazi kumuua kwa risasi meneja wa operesheni wa Zantel, Gabriel Kamukala muda mfupi baada ya kuchukua Sh10 milioni benki.

Kamukala aliuawa Desemba 28 saa 4:00 asubuhi jijini Dar es Salaam na kumekuwapo na matukio ya aina hiyo katika miji mingine mikubwa kama Arusha, Mwanza na Moshi.

Jana kulikuwapo na ujumbe unaosambazwa katika mitandao ya kijamii, ukiwaonya wateja kutothubutu kuchukua fedha kupitia matawi ya benki zilizopo eneo moja jijini Dar es Salaam.

“Benki zote za (jina limehifadhiwa) zina majambazi. Wanakupiga picha na wahudumu wanawaeleza umebeba kiasi gani. Usipende kutoa pesa utakimbizwa na pikipiki,” unasema ujumbe huo.

Mkurugenzi wa kampuni ya Destination Travel ya mjini Moshi, Rogatus Lucas alisema uporaji wa fedha kwa wateja wanaotoka benki usipodhibitiwa, unaweza kuhamia mikoa mingine.

Lucas alitaka sheria iwe ni msumeno, kama hairuhusiwi kutumia simu ukiwa ndani ya benki, basi agizo hilo litekelezwe na si kwa wateja tu hata watunza fedha ili kudhibiti kuvuja kwa siri.

“Tujiulize ni nani wanaotoa siri hizi? Kama baadhi ni wafanyakazi wa benki, basi wasiruhusiwe kutumia simu na kama ni wateja wazizime kabla ya kuingia benki,” alisisitiza Lucas.

Mkurugenzi wa benki ya CRDB mkoani Kilimanjaro, Francis Mollel alitupia lawama wateja kuwa wanapuuza matangazo hayo.

“Hata pale kwangu (tawi la Moshi) kuna matangazo, lakini utakuta bado mteja anaongea na simu. Unawaambia tunazuia hii kwa faida yako, lakini hawakuelewi,” alisema Mollel.

Mollel aliishauri Serikali kutunga sheria kali ya kuzuia matumizi ya simu ndani ya benki na pia mtu yeyote anayechukua kiwango kikubwa cha fedha iwe lazima kuomba ulinzi wa polisi.

Kwa mujibu wa Mollel, ujio wa huduma ya utoaji na uwekaji fedha benki kwa njia ya simu, Simbanking, unaweza kudhibiti uporaji wa fedha, akisema bado matumizi yake yako chini na kusisitiza kuwa huduma hiyo ni salama zaidi kwa miamala ya fedha.

Mfanyabiashara wa jijini Arusha, Nurdin Mahmood, alisema kumekuwa na wateja feki ndani ya benki wanaokaa kwa muda mrefu bila kuhitaji huduma yoyote.

“Benki zinatakiwa ziwe makini sana na kufuatilia mienendo ya watu wa aina hii,” alisema.

Mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Capricorn, George Mberesero alisema kuna ulegevu katika usimamizi wa kanuni za benki kutokana na baadhi ya wateja kuingia na silaha kwa kuwa hakuna ukaguzi.

“Kuwepo na utaratibu wa polisi au walinzi kusimama mlangoni kuhakikisha mteja amezima simu yake au amekabidhi bastola yake, lakini siku hizi imekuwa ni holela. Watu wanaingia na silaha,” alisema.


Source:Mwananchi


Comment & Share this story!!
USALAMA wa wateja wa benki shakani. USALAMA wa wateja wa benki shakani. Reviewed by Zero Degree on 1/04/2016 03:19:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.