VIPIGO vyamrudisha mzungu Majimaji.
Dar es Salaam. Kocha wa Majimaji, Mika Lonnstrom amechoshwa na vipigo vya timu yake na sasa ameamua kukatisha likizo yake ya muda mrefu ili aje kuiokoa klabu hiyo kwenye janga la kushuka daraja.
Lonnstrom aliyeondoka nchini mwanzoni mwa mwezi uliopita, yuko kwenye mapumziko kwao nchini Finland na alitarajiwa kurejea nchini mwishoni mwa mwezi huu kuungana na timu hiyo ambayo kwa sasa ipo chini ya kocha msaidizi, mzalendo Hassan Banyai.
Katika kipindi chote ambacho kocha huyo hayupo nchini, Majimaji haijapata ushindi wowote kwenye Ligi Kuu na badala yake imeishia kuambulia vipigo tu kutoka kwa timu za Azam FC, Toto Africans na Prisons.
Akizungumza na gazeti hili jana, Lonnstrom alisema anatarajia kuungana na timu yake muda wowote kuanzia sasa ili kurekebisha hali ya mambo ambayo imekuwa ikienda mrama siku hadi siku.
“Nasikitika kuona Majimaji haifanyi vizuri na nimekuwa nikiifuatilia kila kukicha.
Kama mambo yakienda vizuri natarajia kuungana na timu siku yoyote kuanzia leo hii tunapozungumza hapa, ili nione ni kwa namna gani timu inarudi kwenye ubora wake wa siku zote,” alisema Lonnstrom.
Kocha huyo aliongeza kuwa ana uhakika timu yake itasalia kwenye Ligi Kuu tofauti na watu wengi wanavyohisi kuwa itashuka daraja msimu ujao.
Source: Mwananchi
Comment & Share this story!!
VIPIGO vyamrudisha mzungu Majimaji.
Reviewed by Zero Degree
on
1/04/2016 02:52:00 PM
Rating: