Vita ya umeya Ilala, Kinondoni leo.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Dar es Salaam. Nini kitatokea leo? Ndilo swali unaloweza kujiuliza kuhusu uchaguzi wa mameya wa manispaa za Ilala na Kinondoni unaofanyika leo baada ya kushindikana mara mbili kutokana na vurugu na kupingwa mahakamani.
Mara ya kwanza uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Desemba 10, mwaka jana lakini ulishindikana na kusababisha mtafaruku baina ya madiwani na baadaye kutinga Mahakama Kuu baada ya CCM kutaka wabunge wake wa viti maalumu kutoka Zanzibar kushiriki. Kesi hiyo ilifunguliwa na Diwani cha Vijibweni (Chadema), Isaya Charles.
Mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi hilo la Charles Januari 8 na kubariki uchaguzi huo ufanyike kwa kuwa aliyefungua kesi hiyo hakuwa na uhalali kufanya hivyo.
Siku moja baadaye wakati madiwani wa CUF na Chadema wakijiandaa na uchaguzi katika ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni na Karimjee kwa Manispaa ya Ilala, kada wa CCM, Elias Nawela alifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuzuia uchaguzi huo.
Taarifa zilisema safari hiyo ya pili, Chadema nao waliingiza wabunge kutoka Zanzibar na kukabiliana na wenzao wa CCM.
Jumatano iliyopita Mahakama ya Kisutu ilitupilia mbali maombi ya Nawela na wakurugenzi wa manispaa hizo mbili kupanga uchaguzi huo kufanyika leo, tarehe ambayo pia iliagizwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene kuwa uchaguzi huo uwe umefanyika ili kutokwamisha shughuli za maendeleo.
Iwapo hakutatokea zuio jingine, vyama vya siasa vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, vinaingia katika uchaguzi huo vikiwa na matumaini ya kupata nafasi ya kuongoza mabaraza ya madiwani katika halmashauri za manispaa za Ilala na Kinondoni kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani kuliko CCM.
Idadi ya madiwani
Katika uchaguzi huo, Chadema ina madiwani 29, CCM 15 na CUF tisa wanatokana kuchaguliwa, viti maalumu na wabunge wanaotoka katika majimbo yaliyoko katika manispaa hiyo.
Katika uchaguzi ulioahirishwa Kinondoni kutokana na hoja za wabunge wa CCM kutoka Zanzibar, Chadema ilikuwa na madiwani 29, CCM 29 na CUF tisa.
Katika sakata la pili, Nawela alipinga uchaguzi huo wakati Chadema wakiwa wameingiza Wazanzibari na kufikia madiwani 36, CCM 31 na CUF 14
Katika Manispaa ya Ilala, madiwani wa kuchaguliwa, viti maalumu na wabunge; Chadema wapo 28, CUF saba na CCM 31.
Tayari Waziri Simbachawene ameshatoa suluhu ya utata wa madiwani wanaostahili kushiriki uchaguzi huo akisema kwa mujibu wa sheria, haiwezekani mbunge wa kuchaguliwa au viti maalumu kupiga kura nje ya halmashauri ya manispaa aliyokuwapo wakati akipendekezwa na chama chake kugombea wadhifa huo.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema madiwani wanaopaswa kupiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 ni wake wa kuchaguliwa, viti maalumu na wabunge wa majimbo yaliyopo katika halmashauri husika na wabunge wa kitaifa (viti maalumu) ambao michakato yao imeanza kwenye mkoa ambao kuna halmashauri husika.
“Ni imani yangu kwamba wakurugenzi wa manispaa hawatafanya uhuni. Kumbuka Tamisemi ipo chini ya ofisi ya Rais na kama wakiendeleza waliyoyafanya awali, tutaamini kuwa wanapata baraka kutoka kwa Rais (John) Magufuli,” alisema Mdee.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida alisema chama hicho kimejipanga kushinda umeya katika manispaa zote mbili.
“Kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa, naamini tutashinda ingawa siwezi kusema tumejipanga vipi. Najua kuna malalamiko mengine ni ya msingi na mengine hayana msingi, yale ya msingi bila shaka kanuni na taratibu zitafuatwa,” alisema.
Mgombea umeya kwa tiketi ya CCM Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta alisema: “Tutapambana, nina imani tutashinda. Najua kuwa wenzetu (Ukawa) wapo wengi kuliko sisi ila inawezekana mtu wa Chadema akanichagua. Hata Joshua (Nassari) alishinda ubunge Arumeru Mashariki wakati madiwani wengi wakiwa wa CCM.”
Boniface Jacob anayewania umeya kwa tiketi ya Chadema Manispaa ya Kinondoni alisema: “Wakitaka uchaguzi ufanyike kihalali tutawashinda na wakitaka tulete wajumbe kutoka Zanzibar tutawashinda pia. Naamini hawataleta visingizio vya kuzuia uchaguzi.” Tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992, CCM imekuwa ikishinda kata nyingi Mkoa wa Dar es Salaam na hivyo madiwani wake kuunda halmashauri, lakini katika uchaguzi wa mwaka jana imepokonywa kata nyingi na Ukawa.
Source: Mwananchi
Vita ya umeya Ilala, Kinondoni leo.
Reviewed by Zero Degree
on
1/16/2016 11:48:00 AM
Rating: