Loading...

Wafungwa Jela maisha baada ya kukamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini.


Raia wa Kenya, Josephine Mumbi Waithera (aliyejifunika), akiwa chini ya ulinzi katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi jana baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Moshi. Mahakama Kuu imewahukumu kifungo cha maisha jela, watu wawili baada ya kupatikana na hatia katika kesi mbili tofauti za kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya Sh289.2 milioni.

Washtakiwa hao waliohukumiwa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari ni Hamis Suya, mkazi wa mkoa wa Tanga na Josephine Mumbi Waithera, raia wa Kenya.

Josephine alikuwa akishtakiwa kwa kusafirisha gramu 3,249.82 za dawa hizo aina ya heroini zenye thamani ya Sh146.2 milioni kwenda Vienna, Austria kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia) wakati Suya alikamatwa akisafirisha gramu 3,191.3 za heroini zenye thamani ya Sh143 milioni kwenda jijini Arusha kwa Basi la Happy Nation.

Akitoa hukumu dhidi ya Suya, Jaji Sumari alisema upande wa mashtaka umeithibitishia Mahakama bila kuacha shaka kuwa alikutwa na dawa hizo.

Alisema hakuna ubishi kuwa tembe 249 za heroini zikiwa ndani ya begi kwenye basi hilo lililokuwa likisafiri kati ya Dar es Salaam na Arusha Novemba 27, 2012 zilikuwa za mshtakiwa huyo.

“Hoja hapa ilikuwa nani ni mmiliki wa begi lile kati ya washtakiwa hawa watatu, yaani Mussa Mgonja, Suya na Abdulaziz Makuka, lakini kulikuwa hakuna ubishi begi la dawa zile lilikutwa ndani ya basi,” alisema Jaji Sumari. 

Alisema kitendawili hicho kiliteguliwa na maelezo ya Suya aliyoandika polisi na kukiri kosa hilo na kuwa aliyatoa kwa hiari yake bila kulazimishwa.

Alisema pamoja na utetezi wa wakili Diana Solomon kuwa mshtakiwa huyo ni mgonjwa na anategemewa na familia, kifungo cha kosa hilo ni kimoja tu, nacho ni jela maisha na hakuna adhabu mbadala. 

Jaji Sumari aliwaachia huru washtakiwa Mgonja na Makuka baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha jinsi walivyotenda kosa hilo. 

Kuhusu kesi ya Josephine, Jaji alisema: “Anadai (Josephine) hakujua unga huo ulikuwa ni dawa za kulevya na kwamba alibeba unga wa dhahabu, bado hakuna ubishi unga huo anaodai ni wa dhahabu umethibitika ni dawa za kulevya.”

Jaji Sumari alisema hana shaka yoyote ya kutoamini hadithi iliyopo katika maelezo yake hayo namna begi hilo lilivyoingia mikononi mwake jijini Arusha, hivyo yeye ndiye mhusika wa dawa hizo.

Kupitia kwa wakili Raplh Njau aliyekuwa akimtetea, mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwa madai kuwa ni mzazi wa watoto wanne na anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

Hata hivyo, Jaji Sumari alisema tatizo la dawa za kulevya ni kilio cha jamii na dunia nzima, hivyo anamhukumu mshtakiwa huyo kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa wahalifu wengine wa aina hiyo.

 Katika hatua nyingine, raia wa Nigeria, Vivian Edigin amekata rufaa kupinga hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa kupatikana na hatia ya kusafirisha gramu 797.56 za cocaine zenye thamani ya Sh39.8 milioni kupitia Kia.



Source: Mwananchi
Wafungwa Jela maisha baada ya kukamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini. Wafungwa Jela maisha baada ya kukamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini. Reviewed by Zero Degree on 1/28/2016 01:24:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.