Loading...

Watoto zaidi ya 800 hawajaanza masomo.

Serengeti. Wakati Serikali ikiahidi kuwachukulia hatua za kisheria wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto shule, uongozi wilayani hapa haujatoa kibali cha watoto zaidi ya 800 wa Kitongoji cha Mchuri kuanza masomo katika majengo yaliyojengwa na wazazi wao.

Mwaka 2010 wakazi wa kitongoji hicho kilichopo Kijiji cha Kenyana, walijenga vyumba vinne vya madarasa, nyumba mbili za walimu, choo cha wanafunzi na jiko ili kuwawezesha watoto wao kuanza masomo baada ya kuchoka kutembea umbali wa kilometa 12 kwenda na kurudi shule.

Hata hivyo shule hiyo haijawahi kufunguliwa na watoto hawasomi.

Mkuu wa wilaya hiyo, Mafutah Ally alipoulizwa na gazeti hili mkakati wa kuwanusuru watoto hao ambao kila mwaka huandikishwa lakini hawaanzi masomo, alisema inawawia vigumu kuruhusu shule hiyo kuanza kwa kuwa imejengwa katika eneo la mwekezaji ambaye analimiliki kisheria tangu mwaka 1988.

“Ni changamoto, maana tukiwaruhusu wanaweza kukatalia hapo. Wangeweza kwenda shule jirani, lakini kwa umbali huo inakuwa vigumu. Nafuatilia kwa karibu ili tuone nini kinaweza kufanyika,” alisema Ally.

Alipoulizwa kama ana mawasiliano na mwekezaji kwa nini haendelezi eneo hilo, alisema hawawasiliani naye kwa kuwa hayupo nchini wala mwakilishi wake hajulikani.

“Shamba hilo halijawahi kuendelezwa wala mwekezaji hatujawahi kumuona ili kuhakikisha mgogoro huo unapata mwafaka. Sisi kama wilaya tunapendekeza ngazi za juu ili watoe uamuzi kuhusu uwekezaji huo ambao haujanufaisha wananchi,” alisema Ally.

Kaimu Ofisa Elimu wa wilaya hiyo, Wanyancha Nyakoge alisema mwongozo wa elimu unasena kuwa mtoto hapaswi kutembea kilometa sita kwenda na kurudi shuleni, na njia pekee ni kuanzisha shule karibu na mahali anapoishi.

Alisema kwamba shule iliyopo jirani iko umbali wa kilometa tisa kwenda, hivyo watoto wanaosoma huko hulazimika kutembea kilometa 18 kwenda na kurudi kwao.

“Waraka namba 5 wa mwaka 2015 unatoa mwongozo kwa maeneo ambayo shule ziko mbali, zianzishwe shule shikizi au vituo na Serikali itapeleka walimu. Kwa kuwa kuna madarasa mamlaka zinatakiwa kuruhusu ili sisi tuanzishe kituo, maana kila mwaka watoto wanaandikishwa hawasomi,” alisema Nyakoge.

Mbunge wa jimbo hilo, Marwa Ryoba alisema wanashughulikia haraka suala hilo ili kituo kiweze kuanza.


Source: Mwananchi
Watoto zaidi ya 800 hawajaanza masomo. Watoto zaidi ya 800 hawajaanza masomo. Reviewed by Zero Degree on 1/13/2016 12:48:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.