Loading...

Wawili wafariki, mmoja apooza kwa mshituko wa BOMOABOMOA.


Katekista wa Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Lukas lililopo Mtaa wa Kigogo Mbuyuni, Kinondoni Dar es Salaam, Mathayo Philipo akiongoza ibada ya kumwombea marehemu Moris Thomas aliyefariki kwa kile kinachodaiwa kupata mshtuko baada ya nyumba yake kuwekwa alama ya X Jumanne iliyopita.

Dar es Salaam. Watu wawili, Moris Thomas na Kobero Peter wamefariki dunia na mwanamke mjane mwenye watoto 10, Mwashamu Hassan amepooza ikidaiwa kuwa ni baada ya nyuma zao kuwekewa alama X. Wote ni wakazi wa Mtaa wa Kigogo, Mbuyuni, Kinondoni.

Tukio hilo lilitokea Jumatatu iliyopita na ilidaiwa kuwa marehemu hao na mama huyo walipatwa na mshtuko ghafla kuanguka. Kobero alipoteza maisha papohapo na Moris alipelekwa katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu ambako alikaa kwa siku moja lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya na kuhamishiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), Muhimbili ambako alifariki dunia Jumanne asubuhi.

Mjane apooza

Akisimulia mkasa huo juzi akiwa amekaa kwenye kipande cha godoro nyumbani kwake, Mwashamu alisema baada ya kuona nyumba yake ikipigwa X, alipatwa na mshtuko na kupooza ghafla kuanzia kiunoni hadi miguuni na kwamba hawezi kutembea tena.

Alisema amekuwa akiishi katika nyumba hiyo aliyoijenga na marehemu mumewe Omary Hassan kwa miaka 15 sasa.

“Hii nyumba nimeijenga na mume wangu kwa kudunduliza pesa, nikiuza karanga yeye akifanya vibarua... tumeijenga kwa Sh12 milioni,” alisema.

Alisema alikuwa akiishi kwa kutegemea nyumba hiyo yenye vyumba sita vya wapangaji na viwili alivyokuwa akiishi na watoto wake.

“Kila mwezi nilikuwa napokea Sh30,000 kwa kila chumba kutoka kwa wapangaji, sikuwa anapokea kodi ya miezi sita wala mwaka,” alisema.

Mmoja wa watoto wa mama huyo, Ibrahimu Hassan alisema ilikuwa saa 3.35 asubuhi wakati wanakunywa chai waliposhangaa kuona kundi la watu wakiwamo askari wenye bunduki waliokuwa na chupa ambazo walikuwa wakizipuliza ukutani na kuandika neno “Bomoa”.

“Tulibaki kushangaa hatujui nini kinaendelea, tuliuliza kuna tatizo gani tukaambiwa tunatakiwa kubomoa nyumba zetu, baada ya kusikia hivyo mama alianza kulalamika anajisikia vibaya,” alisema Hassan; “ilibidi tumnyanyue kumuingiza ndani ili asione kinachoendelea, tukashangaa kufika jioni mama hawezi kusimama wala kutembea.”

Hassan alisema kabla ya hali hiyo mama yao alikuwa anafanya kazi ndogondogo licha ya kuteguka mgongo kutokana na ajali na kuwekewa vyuma ambako alipewa masharti na madaktari ya kutofanya kazi nzito wala kupata mshtuko wa aina yoyote.

“Tayari mama ameshapata tatizo, hapa unavyoona tangu tukio hilo litokee hawezi kutembea, wapangaji wote wamehama, wengine walitakiwa kutulipa kodi tarehe 13 mwezi huu lakini haiwezekani,” alisema.

Hassan alisema kutokana na hali ngumu ya maisha yeye na ndugu zake hawana kipato cha kumsaidia mama yao.

“Wengi wetu tumeishia darasa la saba, tunafanya vibarua vidogo kumsaidia mama kupata pesa ya kula na kusomesha wadogo wetu,” alisema.

Majirani

Majirani wa mama huyo wamemlilia Rais John Magufuli wakitaka awaonee huruma wananchi wake akiwamo mjane huyo ambaye sasa amepata maradhi yaliyosababishwa na bomoabomoa.

“Magufuli ulisema unampenda Mungu na unawapenda watu maskini,” alisema Saumu Mohamed huku Juma Mkude akisema: “Kama hivyo unavyomuona ni mama wa watoto 10, wengine bado ni wadogo watakwenda wapi?”

Mjumbe wa nyumba kumi, Maya Hatibu alisema: “Hali yake kama unavyomuona, hawezi kutembea tena mwenyewe alikuwa anafanya vijikazi vidogovidogo vilivyokuwa vikimwingizia kipato cha kila siku.”

Nyumbani kwa Moris

Akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa Moris iliyofanyika nyumbani kwake Kigogo Mbuyuni kabla ya kusafirishwa kwenda Kijiji cha Matombo, Morogoro alikozaliwa, kaka wa marehemu, Colneus Thomas alisema mdogo wake alikuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu kwa muda mrefu na siku walipofika kuweka alama X alikuwa amekaa nje. Alisema marehemu ameacha mke na watoto watatu na kwamba nyumba hiyo ilikuwa ya urithi wa baba yao na familia yao ilikuwa ikiishi hapo tangu mwaka 1970.

Mtaa wa Mburahati – Barafu

Kazi ya kuweka alama X katika nyumba 1,934 lilikuwa ikiendelea katika Mtaa wa Mburahati – Barafu jana na wakazi wa eneo hilo walionekana kupigwa butwaa huku wakisema “Tunajuta kwa nini tumemchagua Magufuli.”

Jana, Abdallah Bulembo aliyekuwa meneja wa kampeni wa Rais John Magufuli alilishutumu Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) akisema: “NEMC wasiwe kama wameshuka kutoka mbinguni na kukuta watu wamejenga mabondeni. Wasituharibie imani ya wananchi kwa Rais.”

Pia, baadhi ya wananchi walijikuta wakiimba nyimbo za CCM: “Acha waisome nambaeeee...CCM mbele kwa mbele.”

Mama mjane, Janeth Kunambi aliketi chini na kuanza kuangua kilio baada ya nyumba yake kupigwa X. “Nitakwenda wapi sasa... nina watoto wanataka kwenda shule, nawaza wataendaje leo mnaniongezea zigo jingine nani atanitua?”

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventure Baya alisema katika mtaa huo nyumba 1,934 zimewekea alama X na watu wote wanatakiwa kuondoka kwa hiari yao.


Source: Mwananchi

Comment & Share this!!
Wawili wafariki, mmoja apooza kwa mshituko wa BOMOABOMOA. Wawili wafariki, mmoja apooza kwa mshituko wa BOMOABOMOA. Reviewed by Zero Degree on 1/09/2016 08:26:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.