Loading...

Waziri aifungia kampuni ya simu na kuwapeleka vigogo wa kampuni hiyo kizimbani.


Waziri wa Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameifungia kampuni ya Six Telecom kutoa huduma kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh7.247 bilioni. Pia, viongozi wa kampuni hiyo wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Waziri Mbarawa alitangaza uamuzi huo jana akisema kampuni hiyo imekiuka taratibu na kusababisha hasara hiyo, saa chache kabla ya vigogo hao kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Profesa Mbarawa alisema Novemba 8, mwaka jana Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano (TCRA) iliipa kampuni hiyo hadi Januari 13 kujieleza kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria lakini haikufanya hivyo.

Wafikishwa kortini

Saa chache baada ya tamko la waziri huyo, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), wa kampuni hiyo, Hafidh Shamte au Rashid Shamte, Ofisa Fedha Mkuu, Raphael Onyango; Mhasibu, Said Ally na Ofisa Masoko, Noel Chacha walipandishwa kizimbani.

Wengine ni msimamizi wa masuala ya mitandao, Tinisha Max na Mkuu wa Kitengo cha Taarifa za Kibiashara, Vishno Konreddy, wote wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi dhidi ya TCRA.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka mawili ya udanganyifu na kuisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,836,861.99 (zaidi ya Sh7 bilioni).

Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori alisema washtakiwa hao kwa pamoja, walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Mei 2010 na Januari mwaka huu.

Katika shtaka la kwanza, Nyantori alidai kuwa kati ya vipindi hivyo, ndani ya jiji la Dar es Salaam, washtakiwa hao katika kujipatia manufaa ya kifedha au kwa masilahi binafsi, walitoza kiwango cha chini cha gharama za kupiga simu za kimataifa.

Alifafanua kuwa washtakiwa hao walitoza cha chini ya zaidi ya kiwango cha chini cha Dola za Marekani, senti 25 kwa dakika na kwamba walishindwa kulipa kodi ya mapato kwa TRCA kiasi cha Dola za Marekani 3,836,861.99.

Katika shtaka la pili, Nyantori alidai kuwa katika kipindi hicho, walitoza kiwango cha chini zaidi kiwango cha chini cha kupokea simu za kimataifa cha Dola za Marekani senti 25 na kushindwa kulipa kodi ya mapato kwa TCRA.

Alisema kwa vitendo hivyo, washtakiwa hao waliisababishia TCRA hasara.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote, kukubali au kukana mashtaka yanayowakabili.

Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwaambia washtakiwa hao kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka hajatoa kibali cha kufanya hivyo na kwamba Mahakama Kuu ndiyo yenye uwezo wa kuisikiliza.

Nyantori aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuomba ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mawakili wa utetezi Majura Magafu, Shayo Brayson na Emmanuel Augustino waliomba upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi. Hakimu Mwijage aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 28 kwa kutajwa na kuamuru washtakiwa wapelekwe rumande hadi tarehe hiyo.



Source: Mwananchi
Waziri aifungia kampuni ya simu na kuwapeleka vigogo wa kampuni hiyo kizimbani. Waziri aifungia kampuni ya simu na  kuwapeleka vigogo wa kampuni hiyo kizimbani. Reviewed by Zero Degree on 1/16/2016 04:00:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.