Loading...

Tuhuma mpya tena Bandari ya Dar.


Bandari ya Dar es Salaam

Arusha. Bandari ya Dar es Salaam imetupiwa tuhuma nzito kuwa inatumika kupitisha makontena yenye silaha kwenda Bujumbura, Burundi kwa ajili ya kuendeleza mauaji nchini humo.

Hayo yalielezwa jana na upande wa walalamikaji kutoka kwenye asasi zisizo za kiraia za Burundi, walipokutana Arusha kuanza mazungumzo ya amani ya nchi hiyo.

Makamu Rais wa shirika la FORSC, Vital Nshiriminirimana alisema licha ya Bandari hiyo kutumiwa kusafirisha bidhaa mbalimbali zikiwamo silaha za kivita za nchi hiyo, pia silaha za magendo zimekuwa zikiingizwa nchini humo bila kuwapo jina la mmiliki wa makontena hayo.

Nshiriminirimana alikuwa anaieleza kamati inayohusika na masuala ya kikanda na usuluhishi wa migogoro ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hata hivyo, Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Janeth Ruzangi ambaye kabla ya kuzungumzia suala hilo aliomba muda kuuliza katika idara mbalimbali za mamlaka hiyo, alisema kwa muda mrefu Burundi haijatumia bandari hiyo kupitisha silaha zake, licha ya kwamba silaha za nchi mbalimbali hupitishwa katika bandari hiyo.

Alisema silaha zinazopita bandarini ni zile zenye vibali pekee.

“Upitishaji wa silaha una taratibu zake na utaratibu huo upo chini ya JWTZ (Jeshi la Wananchi Tanzania). Jeshi hilo huzisindikiza silaha hizo mpaka katika mpaka wa nchi zinakokwenda.

“Kinyume na hapo hakuna silaha zinazopita bila kibali na kama kuna ushahidi wa silaha kupita bila utaratibu, wanaodai hivyo wanatakiwa kuutoa,” alisema Ruzangi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa alisema majibu yaliyotolewa na TPA ni sahihi na kusisitiza kuwa idara hiyo mpaka sasa haijapokea wala kusikia malalamiko ya aina hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga alisema: “Burundi wanapitisha mizigo yao Bandari ya Dar es Salaam, zikiwamo silaha na hilo si jambo la ajabu kwa sababu zinapita kihalali na siamini kama zinapitishwa kinyume na taratibu.”

Katika ufafanuzi wake, Nshiriminirimana alisema yuko tayari yeye pamoja na asasi nyingine kutoa ushahidi wa jinsi Serikali ya nchi hiyo inavyoshiriki kufanya mauaji ya wananchi wake, huku akimtaka Rais John Magufuli kufanya upelelezi kubaini jinsi Bandari ya Dar es Salaam inavyotumika.

"Sisi asasi zisizo za kiraia, tuna ushahidi juu wa jinsi Serikali ya Nkurunziza, wakiwamo mawaziri na maofisa wa Serikali na kijeshi wanavyoshiriki mauaji ya kikatili nchini, tumesimama kutaka Umoja wa Mataifa, Umoja na Afrika na EAC kuingilia kati hili suala hili mara moja na kulipatia ufumbuzi," alisema.

"Haitakuwa na maana kuwapo katika ya jumuiya, huku Afrika na wanajumuiya wake na umoja wakinyamaza, sisi ni miongoni mwa jumuiya, tunaomba tuungane kuikomboa nchi yetu."

Mwenyekiti wa harakati za kutetea wanawake na wasichana katika machafuko Burundi, Marie Baricako alitaka jumuiya hiyo irejee makubaliano ya Arusha ya mwaka 2000 ya kuwapo na mgawanyo wa asilimia 50 kwa 50 ya maofisa wa jeshi kutoka makabila yote.

Alisema kwa sasa upande mmoja wa Wahutu umeonekana kuwa na maofisa wengi kuliko Watutsi, jambo ambalo linaaminisha kuwa machafuko yanayoendelea huenda yakawa ya kikabila.

Pamoja na hayo, waliitaka EAC iingilie kati kuwapo kwa wanamgambo wa chama tawala 'Imbonerakure' na kumtuhumu Rais Nkuruzinza kuwatumia kuua, kuteka, kubaka na kutesa wananchi, hasa wale wanaoonekana kuwa kinyume na Serikali yake.

Alidai kuwa licha ya kuwatumia wanamgambo hao, pia amekuwa akiwavalisha mavazi ya maofisa wa jeshi na polisi na kuwapa nafasi ya kuwa walinda usalama, huku wakienda kinyume na matakwa ya kijeshi nchini humo.

Mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kikanda na usuluhishi wa migogoro EAC, Abdullah Musinyi alisema kwa sasa wameruhusiwa kikatiba kusikiliza pande zote mbili, walalamikaji na walalamikiwa ili kupata ufumbuzi wa machafuko hayo.

"Kipindi hiki ni cha kusikiliza maoni, hatuwezi kutoa kauli yoyote bila kusikiliza pande zote na kisha tutachambua na kutoa maazimio ya jumuiya," alisema Musinyi.

Alisema wameanza kusikiliza upande wa walalamikaji zikiwamo asasi zisizo za kiraia na vyama vya upinzani na baadaye watawasikiliza walalamikiwa ambao ni Serikali ya Nkurunzinza ili kupata suluhu ambayo itapelekwa bungeni kujadiliwa na kupelekwa kwa Rais wa wadau wa jumuiya hiyo.

Pia, alisema mchakato huo unategemea kukamilika kabla ya Bunge kuanza Januari 25 na kuwa iwapo upande zote zitakubali wito huo hadi mwanzoni mwa Februari, watakuwa wameshachanganua na kufikia ufumbuzi wa tatizo hilo.

Wakati huohuo, Balozi Mahiga amesema mpango wa kupeleka majeshi ya Umoja wa Afrika kulinda amani nchini Burundi umesitishwa, badala yake yanafanyika mazungumzo na Serikali ya Burundi ili kuona kama ipo haja ya kufanya hivyo.

“Tumeona Serikali ya Burundi ina nia ya kuendelea na mazungumzo ya amani na tumeona tusubiri hili kwanza.”



Source: Mwananchi
Tuhuma mpya tena Bandari ya Dar. Tuhuma mpya tena Bandari ya Dar. Reviewed by Zero Degree on 1/16/2016 03:52:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.