Loading...

Kesi ya ubunge yauvuruga uongozi wa Chadema Kyela.


Kyela. Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Kyela, Donald Mwaisangu amejiuzulu wadhifa huo akidai kuwa baadhi ya viongozi wa chama hicho wilayani hapo walikihujumu na kusababisha kufutwa kwa kesi ya kupinga matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Harrison Mwakyembe.

Mbali na Mwaisangu, pia wajumbe wanne wa kamati ya siasa ya chama hicho wilaya nao wametangaza kujiondoa kwa madai hayohayo.

Katika kesi hiyo, aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Abraham Mwanyamaki alikuwa akipinga ushindi wa Dk Mwakyembe na kufungua kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na aliamriwa kulipa Sh3 milioni ikiwa ni dhamana ya kesi, lakini alishindwa kulipa kiasi hicho na mahakama ikaifuta.

Akizungumza jana, Mwaisangu alisema yeye na wenzake wamefikia uamuzi huo kwa kuwa hawakubaliani na mambo yaliyojitokeza hadi kufutwa kwa kesi akidai kwamba viongozi wa chama wa wilaya na Mwanyamaki mwenyewe wanahusika kwa kuwa hawakuwashirikisha wafuasi wao juu ya mwenendo wa kesi hadi kufikia hatua ya kufutwa.

“Haingii akilini kesi ifutwe kwa kukosa Sh3 milioni, hata mazingira yenyewe yana utata kwanza viongozi wa wilaya wapo kwa ajili ya masilahi binafsi,” alisema”

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kyela, Saadati Mwambungu alipoulizwa juu ya viongozi hao kuachia ngazi na uongozi wake kutuhumiwa kuhusu kesi ya Mwanyamaki, alikana na kusema hilo ni suala la mgombea mwenyewe na hata uongozi ulisikia kwamba kesi imefutwa na ofisi yake haijapokea barua wala maelezo kutoka kwa Mwanyamaki.

“Kesho tunakaa kikao na uongozi wa mkoa kujadili hayo yote na mpasuko uliopo na baada ya hapo nitakuwa na majibu sahihi,” alisema.

Alisema kujiuzulu kwa Mwaisangu kuna lengo la kutengeneza genge la kukichafua chama na viongozi wake. 



Source: Mwananchi
Kesi ya ubunge yauvuruga uongozi wa Chadema Kyela. Kesi ya ubunge yauvuruga uongozi wa Chadema Kyela. Reviewed by Zero Degree on 1/16/2016 03:47:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.