Loading...

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo aipiga ‘stop’ kampuni ya madini.


Kyela. Serikali imesimamisha shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe uliokuwa ukifanywa na Kampuni ya Off Route Technology iliyopo katika Kijiji cha Ngana wilayani Kyela na kuviweka chini ya uangalizi vifaa vyake hadi uchunguzi kuhusu madai mbalimbali yanayoikabili utakapokamilika.


Jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitembelea katika mgodi unaoendeshwa na kampuni hiyo na kubaini kuwa inachimba makaa hayo bila kuwa na leseni halali ya uchimbaji madini.

Waziri aliitaka kampuni hiyo kulipa kodi zote za Serikali, ikiwamo inazodaiwa na Halmashuri ya Wilaya ya Kyela tangu ianze kufanya shughuli za uchimbaji.

Ili kupata undani wa madai yanayoikabili kampuni hiyo, Profesa Muhongo aliitisha mkutano utakaohusisha Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini Magharibi na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyela Januari 18, mwaka huu chini ya uenyekiti wa katibu mkuu wa wizara hiyo.

Pia alizitaka pande zote kuwasilisha nyaraka muhimu kuhusu suala hilo ili uamuzi ufuate sheria na taratibu.

“Hakuna mtu atakayeonewa, kila upande uje na nyaraka zote na sisi wizarani huko ndani kwetu tutaulizana wenyewe kuhusu jambo hili halafu tutalitolea taarifa,”alisema.

Ofisa Mfawidhi wa TMAA, Jumanne Mohammed alisema awali wakala huo ulifanya ukaguzi na kubaini kuwa kampuni hiyo hailipi kodi muda mrefu.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo iliahidi kwamba ingelipa kodi hizo kwa awamu, jambo ambalo halijafanywa hadi sasa.

Mohammed alisema watawasilisha taarifa zilizoagizwa na waziri ili haki iweze kutendeka kwa mujibu wa sheria za nchi. Ofisa huyo alisema TMAA imekuwa ikitekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria ya madini.




Source: Mwananchi
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo aipiga ‘stop’ kampuni ya madini. Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo aipiga ‘stop’ kampuni ya madini. Reviewed by Zero Degree on 1/16/2016 03:44:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.