Loading...

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba aagiza mawakala wa pembejeo za kilimo wakamatwe na kupelekwa mahabusu.


Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba

Tunduru. Hapa kazi tu. Hiyo ni kaulimbiu inayotekelezwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba baada ya kuagiza kukamatwa kwa mawakala wa pembejeo za kilimo wilayani hapa.

Hatua hiyo imekuja baada ya waziri huyo kufanya ziara ya kushtukiza katika wilaya hiyo na kubaini udhaifu katika ugawaji wa pembejeo za ruzuku.

Mawakala waliokamatwa ni Ibrahim Ibrahim na Zubeir Namhala pamoja na Mtendaji wa Kijiji cha Nandebo ambaye anakaimu nafasi ya mtendaji wa kata hiyo, Zainabu Twaha na Ofisa Ugani wa Kijiji cha Majara, Ayubu Machemba.

Awali katika kikao kilichojumuisha watendaji wa Serikali ya vijiji hivyo, kata, mawakala hao na maofisa kilimo, Waziri Nchemba alisema tayari ana vielelezo vyote vinavyoonyesha kuna udanganyifu umefanyika na kuamuru mawakala hao wakamatwe wakiwa ndani ya kikao hicho baada ya kushindwa kujibu maswali.

Alisema amebaini kuwa wamekuwa wakifanya udanganyifu kwa kushirikiana na watendaji wa kata kuwasainisha wakulima kuwa wamepewa mbolea ya kupandia na kukuzia mazao wakati hawajapewa au wamepewa pungufu.

“Mimi mpaka naamua kuja Tunduru siyo kwamba nimejiamulia, tayari nina taarifa za udanganyifu kwenye vocha za pembejeo za kilimo. Wapo watendaji wamewasainisha wananchi kuwa wamechukua mbolea ya kupandia, kukuzia na mbegu wakati wamechukua mbolea ya kukuzia. Mimi nina picha za sahihi za waliosainishwa,” alisema Nchemba.

Waziri huyo alimtaka mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kuwafuatilia watendaji wanaofanya ubabaishaji na kuwachuja, huku akimtaka mkuu wa polisi wa wilaya na mkuu wa wilaya kufuatilia kamati zote zilizokiuka taratibu na kuzichukuliwa hatua.

Akizungumzia hilo, Mkuu wa wilaya hiyo, Agnes Hokororo alisema wakulima wengi wamepanda mbegu zao za kienyeji baada ya kuona hakuna mbegu bora zilizopelekwa na mawakala.

Ofisa Kilimo wa wilaya, Chiza Marando alisema baadhi ya mawakala siyo waaminifu kwa kuwa wameshindwa kupeleka pembejeo kwa wakati kufuatana na msimu.

Pia, aliiomba wizara kungalia njia rahisi ya kuwafikishia wakulima pembejeo.



Source: Mwananchi
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba aagiza mawakala wa pembejeo za kilimo wakamatwe na kupelekwa mahabusu. Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba aagiza mawakala wa pembejeo za kilimo wakamatwe na kupelekwa mahabusu. Reviewed by Zero Degree on 1/17/2016 09:57:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.