Loading...

Sumatra lawamani kuhusu nauli elekezi.


Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya

Serengeti. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Mkoa wa Mara imedaiwa kushindwa kusimamia nauli elekezi na kusababisha wamiliki wa vyombo vya usafiri kutoza gharama wazitakazo.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Mara, Halma Abdallah alikiri wamiliki wa magari kupandisha nauli kinyemela huku akisema hajapata malalamiko rasmi ofisini.

Nauli halali ya kutoka Bunda hadi Serengeti ni Sh5,000 lakini magari hayo yamekuwa yakitoza Sh8,000.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wilayani hapa jana, wasafiri Sospeter Wema na Kisiroti Zakaria walisema nauli zinapandishwa kwa visingizio vya ubovu wa barabara kinyume na matakwa ya Sumatra.

Zakaria alisema nauli hizo hazizingatii kilometa, hivyo abiria anayesafiri kilometa 40 anatozwa nauli sawa na anayesafiri kilometa 80.

Hivi karibuni katika kikao cha Jumuiya ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Alat), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Porini aliomba madiwani na wabunge mkoani hapa kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Alisema suala la nauli linawaumiza wananchi huku kundi la wafanyabiashara likinufaika.

Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya aliwataka madiwani kulifuatilia kwa kina suala hilo kisha walitolee taarifa ikiwamo kuwakabidhi wabunge ili waweze kuwasiliana na waziri mwenye dhamana.

Alisema wakifanya hivyo, wataweza kuwabana watendaji wa mamlaka hiyo.

Ofisa wa Sumatra, Abdallah alisema: “Changamoto hiyo nimeiona baada ya kuzunguka maeneo mengi na kujionea hali halisi, nauli zinatozwa kwa kilometa, lazima zitofautiane kati ya kituo na kituo, nipo katika hatua ya mwisho ya kutoa bei zote kwa njia za Bunda, Musoma, Tarime hadi Mugumu, Musoma hadi Arusha. “Nitawakabidhi maofisa wa usalama barabarani katika maeneo yote ili waweze kusaidia wananchi wanapotozwa nje ya maelekezo ya Serikali,” alisema Abdallah.



Source: Mwananchi
Sumatra lawamani kuhusu nauli elekezi. Sumatra lawamani kuhusu nauli elekezi. Reviewed by Zero Degree on 1/17/2016 07:48:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.