Loading...

Homoni za kuongeza asilimia 40 ya siku za kuishi yagunduliwa na wanasayansi.


Dar es Salaam. Tumaini jipya. Hivi ndivyo tunavyoweza kusema baada ya wanasayansi kugundua vichocheo (homoni) vinavyoweza kuongeza siku za kuishi kwa asilimia 40.

Hayo yamebainishwa na timu ya wanasayansi kutoka Chuo cha Tiba cha Yale, Marekani wakiongozwa na Profesa Vishwa Deep Dixit, waliobaini kuwa wingi wa homoni ya FGF21 unalinda mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya uharibifu wa seli unaosababishwa na umri.

Watafiti hao walisema kwenye ripoti yao ya kitabibu iliyochapishwa kwenye jarida la Lancet kuwa huenda utafiti huo ukawa na manufaa makubwa baadaye kwa kuimarisha kinga ya mwili kwa wazee na wagonjwa wa saratani na kisukari aina ya pili.

Homoni hiyo yenye huzalisha seli ya T (T-Cells) ambazo hutunza zaidi kinga ya mwili. Katika hali ya kawaida homoni hizo huharibika kadri mtu anavyozeeka na kupoteza uwezo wake wa kuzalisha seli muhimu zinazoupa mwili kinga.

Kwa kuwa T-Cells ndizo zinazosaidia katika mfumo wa kinga ya mwili, zinapochakaa kwa sababu ya umri, husababisha mtu kuambukizwa magonjwa kwa urahisi na kupata saratani.

Profesa Dixit alifanya majaribio ya utafiti huo kwa panya wenye kiwango cha juu cha homoni za FGF21 na wale wenye kiwango cha chini.

Matokeo ya utafiti huo yalibainisha kuwa ongezeko la kiwango cha homoni hiyo kwa panya mzee kulizifanya zisichakae na kuongeza uwezo wa kuzalisha seli nyingine mpya.

“Tumegundua kuwa kiwango cha FGF21 kwenye seli kinaongezeka mara mbili zaidi kuliko ilivyo kwenye ini, hivyo homoni hiyo hufanya kazi katika tezi zinazozalisha chembe nyeupe ya damu (thymus) kuongeza uzalishwaji wa seli ya T,” alisema.

Profesa Dixit alisema homoni ya FGF21 huzalishwa kwenye ini kama homoni ya endocrine. Kazi nyingine za homoni hiyo ni kuongeza uwezo wa utendaji wa homoni ya insulini na kusababisha uzito kupungua.

Ndiyo maana wanasayansi hao wanasema kuwa ina nguvu pia katika kupambana na kisukari aina ya pili na unene kupita kiasi.

Wanasayansi hao wameeleza kuwa baadaye wataendeleza utafiti huo na kuangalia uwezekano wa kutengeneza vidonge vya homoni hizo na kupunguza magonjwa yasababishwayo na umri au kinga ya mwili.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili, Dk Meshack Shimwela alisema anafahamu kuwa tezi ya thymus ni ya kupambana na magonjwa kwa kuwa inazalisha chembe hai nyeupe. “Inawezekana homoni hiyo ikasaidia mtu asipate magonjwa na asizeeke, lakini kuhusu suala la kuongeza siku za kuishi sina uhakika sana, nadhani hilo linahitaji utafiti zaidi,” alisema Dk Shimwela ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana.

Alisema inawezekana wakaweza kutengeneza homoni au tezi hiyo katika maabara lakini madhara yakajitokeza, kwa mfano mtu kushindwa kukua vizuri au udumavu.

Daktari wa kitengo cha uchunguzi wa magonjwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Innocent Mosha alisema tezi ya thymus inayopatikana katikati ya kifua cha binadamu ina kazi ya kuzalisha chembe hai nyeupe pamoja na seli nyingine.

Alisema huenda homoni hiyo ambayo ndani yake ina tezi za thymus ina nguvu kwa sababu chembe hai nyeupe ndizo zenye kazi kubwa katika kuukinga mwili na magonjwa.



Source: Mwananchi
Homoni za kuongeza asilimia 40 ya siku za kuishi yagunduliwa na wanasayansi. Homoni za kuongeza asilimia 40 ya siku za kuishi yagunduliwa na wanasayansi. Reviewed by Zero Degree on 1/17/2016 07:52:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.