Wizara ya Afya yawataka WANAOTOA TIBA ASILI wote kujisajili.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu .
Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema inakusudia kupeleka muswada bungeni kufanya mabadiliko ya sheria au kufuta kanuni inayoruhusu matangazo kwa watoa tiba mbadala, huku ikimpa miezi mitatu tabibu, Juma Mwaka kurekebisha kasoro zote katika utoaji huduma kwenye kituo chake.
Akizungumzia uamuzi ya wizara kuhusu watoa tiba asili na mbadala jana, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema changamoto zilizobainika ni pamoja na huduma hizo kutolewa na matabibu wasiosajiliwa na mamlaka husika kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na uwepo wa vituo vinavyotoa huduma pasipo kusajiliwa.
Alisema ni makosa kutoa dawa kwa wagonjwa bila kusajiliwa na mamlaka husika pamoja na uingizaji na matumizi ya vifaa vya uchunguzi ambavyo havikusajiliwa na utoaji wa matangazo bila kufuata matakwa ya sheria.
Ummy anayeshughulikia pia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alisema wizara itahakikisha baraza na sehemu inayosimamia huduma za tiba asili na tiba mbadala inakuwa na watumishi wa kutosha.
Alisema ili kurekebisha kasoro zilizopo, wizara imejipanga kurekebisha sheria ili kuondoa kanuni inayoruhusu matangazo kwa idhini ya baraza.
“Tutahakikisha watoa huduma, dawa na vifaa tiba vyote vinasajiliwa, mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma, uwepo wa mawasiliano na wizara zinazohusika pamoja na kufanya mabadiliko ya sheria ili kuongeza kiwango cha adhabu kwa watakaokiuka,” alisema Ummy.
Ummy alipiga marufuku kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili na tiba mbadala bila kusajiliwa huku akiwataka watoa tiba wote wa mijini kujisajili ndani ya miezi mitatu kuanzia jana huku vijijini wakipewa miezi sita.
Kuhusu Dk Mwaka, Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla alisema tabibu huyo amepewa msamaha kwa kuwa katika nyaraka zake alizowasilisha ilionekana vyeti viwili alivyosomea utaalamu wa mimea kutoka Australia kwa mwaka mmoja na kingine China kwa miezi kadhaa.
Dk Kigwangalla alisema mbali na nyaraka hizo, walibaini kwamba dawa aina nane alizokuwa akizitoa zilikuwa zimesajiliwa kwa jina la tatibu Matunge Herbalist, suala ambalo halikuwa likitambulika awali kwani hakuna dawa iliyosajiliwa kwa jina lake.
Alisema zipo kasoro ambazo zilijitokeza kwa tabibu Mwaka ikiwamo kuwa na wasaidizi saba ambao hawakuwa wamesajiliwa na baraza wala kuwa na utaalamu wowote wa masuala ya kiafya yanayotambuliwa kisheria.
“Alistahili kufungiwa, lakini wizara tumeonelea tumpe miezi mitatu arekebishe kasoro zilizopo na tunamfahamisha mapema kwamba kifaa tiba anachokitumia kutambua magonjwa ‘Quontum Magnetic Analyser kwanza anayekiendesha hana taaluma yoyote, kiliingia nchini bila kibali na tumebaini kwamba hata China hakikuondolewa kwa kibali maalumu, hivi vyote arekebishe,” alisema Dk Kigwangalla.
Source: Mwananchi
Wizara ya Afya yawataka WANAOTOA TIBA ASILI wote kujisajili.
Reviewed by Zero Degree
on
1/16/2016 11:55:00 AM
Rating: