Loading...

Bakwata Dar yaunga mkono marudio ya uchaguzi Zanzibar.


Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.



Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam, limesema linaunga mkono uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuitisha uchaguzi wa marudio ili kupata ufumbuzi wa mkwamo wa kisiasa visiwani humo.

Msimamo huo ulitolewa jana na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kutoa wito kwa vyama vyote kujitokeza kushiriki mchakato huo.

“Lolote litakaloharibika Zanzibar litakuwa na athari huku Bara pia. Sisi ni ndugu hatuwezi kujitoa kwenye tatizo la upande wa pili. Jambo muhimu ni kwa vyama husika kuacha kutoaminiana na kushiriki marudio hayo,” alisema.

Sheikh Salum alizitaka pande zinazokinzana kuaminiana na kutoa wito kwa CUF kurudisha moyo na kutengua uamuzi wake wa kutoshiriki marudio hayo.

Aliitaka Serikali kuongeza mapambano dhidi ya foleni ambayo ni changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa Dar es Salaam hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

Alisema kutokana na watu wengi kutumia usafiri wa umma, muda mwingi hupotea wawapo barabarani kutokana na wingi wa magari, hivyo kuitaka Serikali kuingilia kati kuboresha miundombinu ya barabara na kuimarisha uchumi wa nchi.


 “Naiomba Serikali kuupa umuhimu unaostahili Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) ili uanze kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema mradi huo unaweza kuleta tija na kuwa mkombozi kwa wakazi wa Dar es Salaam na kupunguza uchovu utokanao na kupoteza muda mwingi barabarani, kuongeza uzalishaji na kufika kwa wakati kwenye shughuli zao.

Alitoa wito kwa Serikali kuwajengea uweo wawekezaji wa ndani kama ilivyofanya kwa kulimilikisha Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) Kampuni ya Simon Group kwa maelezo kuwa wazawa wana uwezo wa kuliletea Taifa maendeleo.

Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kubana matumizi na kuongeza ukusanyaji mapato na kubainisha matokeo chanya yameanza kuonekana akitolea mfano uboreshaji wa huduma za kijamii kama afya pamoja na elimu.


Credits: Mwananchi





ZeroDegree.
Bakwata Dar yaunga mkono marudio ya uchaguzi Zanzibar. Bakwata Dar yaunga mkono marudio ya uchaguzi Zanzibar. Reviewed by Zero Degree on 2/03/2016 10:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.